30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 19, 2021

Mchungaji Rwakatare kuzikwa na watu 10

 MWANDISHI WETU-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema familia ya Mbunge wa Viti Maalumu, Mchungaji Getrude Rwakatare imetoa maombi mawili kwa Serikali, wakitaka azikwe katika eneo la Kanisa la Mlima wa Moto na mazishi yake yafanyike kesho.

Akizungumza jana bungeni kabla ya kuahirisha Bunge, Ndugai alisema Serikali imepokea maombi hayo mawili yanayohusu sehemu ya maziko na siku ya mazishi kutoka kwa familia ya marehemu Mchungaji Rwakatare. 

“Familia imetoa ushauri wa mambo mawili kwa Serikali, imeomba mchungaji ama mama yao azikwe kwenye eneo la Kanisa la Mlima wa Moto.

“Na imeomba tarehe ya mazishi iwe Aprili 23. Kwa upande wa Serikali haina shida na ni kwamba Serikali itasimamia mazishi hayo.

”Niwajulisheni kwa hatua hii ni kwamba Serikali ndio itakayosimamia mazishi hayo na watashiriki watu wasiozidi 10, huo ndio utaratibu utakavyokuwa na sisi tunaomba ushirikiano lieleweke hili na Bunge ushiriki ni kadiri ya ushauri wa Serikali,” alisema Ndugai.

Katika taarifa yake juzi, muda mfupi baada ya taarifa za kifo cha Mchungaji Rwakatare, Ofisi ya Bunge ilisema kuwa kwa kushirikiana na familia yake inaratibu mazishi ya mbunge huyo aliyefariki dunia juzi alfajiri.

Spika Ndugai alisema hayo katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge na kwamba mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Akizungumzia kifo cha Mchungaji Rwakatare, Spika Ndugai alisema; “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Rwakatare.

“Natoa pole kwa wafiwa wote wakiwamo familia ya marehemu, ndugu, jamaa, waheshimiwa wabunge na waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”

Muda mfupi baada ya taarifa ya kifo kutolewa juzi, mtoto wa kiume wa marehemu, Muta Rwakatare, alisema kuwa majibu kutoka kwa wataalamu kuhusu ni kipi hasa kilichosababisha kifo cha mama yao, ambaye alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu, yalithibitisha kuwa ugonjwa huo ndio uliokuwa chanzo cha kifo chake.

Muta akikaririwa wakati wa mazungumzo maalumu na kituo cha EATV, alisema kuwa wanafamilia watakaa na kujua mazishi yatafanyika kwa namna gani, huku wakishirikiana kwa pamoja na Serikali.

“Amefariki na alikuwa yupo hospitali, alikuwa na matatizo kidogo ya presha, kwahiyo mpaka sasa hivi tunasubiri majibu kutoka kwa wataalamu tujue amepatwa na tatizo gani haswa,” alieleza muda mfupi kabla ya kutoa uthibitisho wa sababu za kifo hicho. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,848FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles