NA CHRISTINA GAULUHANGA
DAR ES SALAAM
WAKATI mfanyabiashara maarufu Yusuph Manji akiendelea kusota mahabusu ya Keko, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Abdalah Chaurembo jana ametangaza maazimio ya Baraza la Madiwani kumvua udiwani.
Manji ambaye anakabiliwa na kesi mbili tofauti katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alikuwa Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Chaurembo alisema, Baraza la Madiwani limeridhia kuvuliwa kwa wadhifa wa Manji kwa sababu amekiuka kanuni na sheria za baraza hilo pamoja na halmashauri.
Chaurembo alisema kwa mujibu wa taratibu madiwani wanatakiwa kutoa taarifa za maendeleo ya kata zao kila baada ya miezi mitatu, lakini Manji ameshindwa kufanya hivyo kwa zaidi ya miezi tisa.
“Leo (jana), nimetangaza rasmi kumvua madaraka Yusuph Manji kwa sababu ameshindwa kutimiza kanuni na sheria za uendeshaji wa baraza, hivyo amepoteza sifa na kuanzia leo si diwani tena na sisi kama baraza tumeridhia kwa sababu ameshindwa kutekeleza sheria yeye mwenyewe,”alisema Chaurembo.
Aidha Meya huyo aliitaja sababu nyingine kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao zaidi ya miezi mitatu bila kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa baraza jambo ambalo ni kosa kisheria.
Manji amevuliwa uongozi wa kata yake akiwa anaendelea kusota rumande na wenzake watatu kutokana na kesi ya uhujumu uchumi iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi nyingine inayomkabili Manji katika mahakama ya Kisutu ni tuhuma za kutumia dawa za kulevya za Heroin.