24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

CHADEMA YAGUSA JIPU KWA BUNGE


Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelituhumu Bunge kwa madai ya kuvunja sheria kwa kuomba fedha za ziada nje ya bajeti yake iliyoidhinishwa bila kupitisha maombi hayo bungeni kama katiba inavyotaka.
Chadema imesema Bunge limevunja katiba, ibara ya 137 (3), (a) na (b) huku wakidai pia Waziri wa Fedha amevunja ibara ya 136 na 137 (3) kwa kutoa fedha za ziada nje ya bajeti iliyopitishwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema kati ya Juni 21 na Agosti 15, mwaka huu, Katibu wa Bunge aliandika barua tatu tofauti akiomba zaidi ya Sh bilioni 9 kwa Waziri wa Fedha na kwa Katibu Mkuu Hazina kugharimia bajeti ya ziada.
“Tangu wakati huo hadi Agosti 15, Serikali ilishatoa shilingi bilioni 7 kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina bila kufuata masharti ya katiba na inategemewa itaendelea kutoa shilingi bilioni 2.5 kulipia gharama za posho ya jimbo ya Juni ambayo haijalipwa kwa ukamilifu,” alisema Dk. Mashinji.
Alisema fedha zilizotolewa kama bajeti ya ziada zilitumika kulipa posho za jimbo, kujikimu, vikao, saa za ziada kwa watumishi na posho ya kamati maalumu kwa kipindi cha Mei hadi Juni.
“Katiba inamtaka waziri kuwasilisha bungeni maombi ya bajeti ya ziada na baada ya Bunge kuyakubali, atawasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
“Hatutaki kuamini kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amehusika kuidhinisha malipo haya, maana hata kwenye mawasiliano yaliyopo hajawahi kupewa nakala,” alisema.
Alisema Bunge likiwa kama mhimili unaojitegemea, linapaswa kujiendesha bila kuwa tegemezi kwani ndilo linalopitisha bajeti yake na ya Serikali.
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/17 Bunge liliidhinisha Sh bilioni 92.7 kwa matumizi ya kawaida, Sh bilioni 23.80 mishahara, Sh bilioni 68.27 matumizi mengineyo na Sh bilioni 7 miradi ya maendeleo.
“Bunge ni taasisi ambayo kalenda yake na idadi ya wajumbe vinafahamika, hivyo wanapopitisha bajeti wanakuwa wakijua ni kiasi gani kitahitajika katika mwaka husika wa fedha.
“Tukianza kupuuza katiba, maana yake tunarudi kwenye hali ya kuangalia nani ana nguvu na ataamua nini kukicha,” alisema.
Dk. Mashinji alisema pia uendeshaji wa shughuli za Bunge umekuwa ukiichanganya jamii na alitahadharisha kuwapo hatari ya kutengeneza nchi isiyofuata na kuzingatia taratibu.
“Kuna udhaifu mkubwa katika uongozi wa Bunge ukiongozwa na Spika. Kiongozi jasiri ahitaji kuongea kwa sauti kali, kutumia nguvu kubwa ama ubabe bali ni yule anayefuata taratibu tulizojiwekea.
“Ajipe muda kutafakari je, uongozi wake unaleta hali ya utengamano ama utavuruga jamii… kipimo cha uimara wa kiongozi ni kusimamia katiba,” alisema Dk. Mashinji.
Chadema imeitaka Serikali na Bunge kutoa majibu ya kina kuhusu ukiukwaji na uvunjwaji wa katiba na wale wote waliohusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
“Tunaamini kuwa haya yanaweza kumalizika kama tutakuwa na katiba mpya iliyotokana na maoni ya wananchi, tutatumia njia za kidemokrasia na kidiplomasia kuhakikisha tunapata mwafaka wa katiba mpya. Endapo hazitazaa matunda tutaomba wananchi wafanye maamuzi,” alisema.
Kutokana na madai hayo ya Chadema MTANZANIA lilimtafuta Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila ili kupata ufafanuzi, lakini simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles