23.5 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

KIMEWAKA TENA


MAREGESI PAUL Na RAMADHAN HASSAN
-DODOMA
KIMEWAKA. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya ripoti za kamati maalumu za uchunguzi za Bunge, kuhusu madini ya tanzanite na almasi, kuwakaanga mawaziri wa sasa na zamani kwa kueleza namna walivyohusika katika mikataba mibovu iliyosababisha hasara kwa taifa.
Ripoti hizo zilikabidhiwa kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alizikabidhi kwa Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa hafla fupi iliyohudhuriwa na wabunge, viongozi wa Serikali na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama mjini Dodoma jana.
Waziri Mkuu Majaliwa, leo atakabidhi ripoti hizo kwa Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi wa mwisho, huku hofu ya kutumbuliwa kwa vigogo hao ikitanda.
Akiwasilisha ripoti yake, Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Bunge iliyoundwa kuchunguza biashara ya madini ya tanzanite, Dotto Biteko, aliwataja mawaziri watatu wa zamani wa Wizara ya Nishati na Madini, walivyoshiriki kuiingizia hasara Serikali kupitia madini hayo.
Biteko, aliitaka Serikali iwahoji mawaziri hao, William Ngeleja, Profesa Sospeter Muhongo na George Simbachawene, ili kujua ni kwa nini walishindwa kutimiza wajibu wao.
Katika maelezo yake, Biteko alisema Profesa Muhongo anatakiwa kuhojiwa kwa sababu mwaka 2013, alitoa leseni ya ubia kwa mwekezaji wa kigeni bila kushauriana na bodi na pia hakuna vikao vilivyokaa kupitisha uamuzi wake.
Chini ya leseni hiyo, Biteko alisema mwekezaji huyo ambaye ni Tanzanite One, aliruhusiwa kupata eneo kubwa kuliko wawekezaji wengine kwa kuwa kati ya leseni 731 zilizoko Mirerani, ni hiyo moja ndiyo iliyopewa upendeleo ikiwa katika eneo la kitalu C.
“Yeye Simbachawene aulizwe ni kwa nini alitoa uhamisho wa hisa za Sky Associate bila kuhusisha wataalamu kwa sababu kamati ilishindwa kuelewa ni kwa nini alifanya hivyo.
“Kwa upande wa Ngeleja, yeye aulizwe ni kwa nini alichelewa kutekeleza matakwa ya sheria yaliyotaka kila mwekezaji wa kigeni afanye biashara ya madini kwa kushirikiana na wazawa, kwa sababu ucheleweshaji alioufanya, uliingizia hasara Serikali ya Sh. bilioni 237.
“Kifungu cha sita cha sheria, kinaweka utaratibu wa mtu au kampuni inayofanya shughuli au kazi za madini zilizotajwa katika sheria hiyo.
“Hata uchambuzi na tathmini ya kamati ulibaini kwamba Desemba 4, mwaka 2014, Kampuni ya TML iliomba ridhaa kwa Waziri wa Nishati na Madini baada ya kampuni moja kuingia mkataba na Kampuni ya Sky Associate Ltd, unaoipa nguvu kufanya kazi katika kitalu C huko Mirerani Arusha.
“Kwa muktadha huo, ridhaa iliyotolewa Januari 30, mwaka 2015 na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo, George Simbachawene, ina dosari za kisheria na ukiukwaji wa kiutendaji na utoaji wa ridhaa hii, unainyima Stamico kipaumbele cha kununua Kampuni ya TML.
“Kwa msingi huo, kamati imebaini dosari zilizofanywa za kubadilisha watoa maamuzi wa Kampuni ya TLM, zilifanyiwa kazi katika ngazi ya Wizara ya Nishati na Madini chini ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kamishna wa Nishati na Madini na idara za sheria na katika mashauriano hayo, yafuatayo yalibainika.
“Matokeo ya kuuza hisa Tanzanite One South Afrika, unaipa nguvu Kampuni ya Sky Associate katika Kampuni ya TLM na mauziano hayo yasingeweza kukamilika bila ya kupata kibali cha mheshimiwa waziri.
“Wizara ya Nishati na Madini ilitakiwa kabla ya kutoa ridhaa, ifanye upembuzi yakinifu ili kujua mbia anayeondoka kama anadaiwa chochote kabla ya kuruhusu uhamishaji wa wanahisa, lakini pia kuangalia uwezo wa mbia anayekuja na kujiridhisha maamuzi ya wale wanaouza.
“Tarehe 30 Januari, waziri aliamua kutoa ridhaa bila ya kuzingatia ushauri wa mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini na katika hilo, kuna barua ya ushauri wa mwanasheria iliyosema uuzwaji wa hisa hizo sio halali kwa sababu mtu huyo hatumfahamu.
“Pili, Kamishna wa Madini alitoa ushauri kwa waziri, kwamba hili jambo lisifanyike kwani utaratibu haujazingatiwa na pia Kamati ya Nishati na Madini ikiwa chini ya Mheshimiwa Ndassa, ilitoa ushauri ikiwataka wafuate utaratibu.
“Jambo linalosikitisha ni kwamba mheshimiwa Waziri Simbachawene aliapishwa tarehe 24 na tarehe 27 akaingia ofisini na tarehe 30, akasaini hati hiyo bila kuzingatia ushauri uliokuwapo.
“Mfumo wa utoaji wa leseni nchini, haujawahi kuwa madhubuti tangu kugunduliwa kwa madini hayo mwaka 1997 na hali hiyo inathibitishwa na utitiri wa leseni za uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo wadogo chini ya usimamizi mdogo wa Serikali.
“Kwa hiyo, matokeo ya utitiri wa leseni hizo ni utoroshwaji wa madini, uwepo wa ajira zisizokuwa rasmi kwa wafanyakazi wa migodi kwa sababu mamlaka zinazohusika na usimamizi wa tanzanite ambazo ni Stamico na Kamishna wa Madini, zimeonyesha udhaifu mkubwa wa utendaji.
“Kwa mfano mdogo tu, ni kwamba taarifa zilizopo zinaonyesha tangu mwaka 1998 hadi mwaka 2017, kiasi cha madini ya tanzanite kilichoripotiwa na wachimbaji wadogo ni kilogramu 13.2 tu yaani kwenye leseni 738 ni kilogramu 13.2 tu kwa mwaka.
“Pia, uchunguzi wa kamati yetu ulibaini asilimia 20 ya madini ya tanzanite ndiyo yanayolipiwa kodi wakati asilimia 80 yanasafirishwa nje kinyemela,” alisema Biteko.
Ili kuthibitisha wizi wa madini unavyofanyika mgodini hapo, Biteko alisema kuna video ya kamera za CCTV zilizorekodiwa Julai 20 na 21, mwaka huu zinazoonyesha hali ilivyo na alimkabidhi Spika video hiyo ili itumike wakati wa kuchukua hatua kwa wabadhirifu wa maliasili hiyo kwa kuwa wanaohusika katika wizi huo ni pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia, alisema takwimu za mauzo ya madini zinazotolewa na Tanzanite One ni tofauti na zilizoko serikalini, jambo ambalo alisema linatakiwa kufanyiwa kazi haraka ili kudhibiti mapato ya Serikali.
“Hata Stamico imeshindwa kuwa na akaunti ya pamoja na TML na jambo hili linasababisha upotevu wa fedha za Serikali bila sababu za msingi na pia Stamico wamekuwa wakisuasua kuteua wajumbe wa bodi wakati TML wana wajumbe wao katika bodi,” alisema.

MAPENDEKEZO
Pamoja na hayo, alisema kamati yake ilishauri itungwe sheria kuhusu tanzanite, kiwepo kituo kimoja cha kusimamia madini hayo, Serikali iboreshe minada na ununuzi wa madini hayo na yote yauzwe kwenye minada na pia kiwepo kituo cha kuyahifadhi kila itakapotakiwa kufanya hivyo.
Pia, alisema kamati yake inashauri akaunti za TML na taasisi zake zizuiwe kwa muda, mkataba kati ya TML na Stamico uvunjwe na viongozi wote wenye dhamana ya madini waliohusika na upotevu wa madini hayo wahojiwe.
Aliwataja baadhi yao kuwa ni pamoja na Edwin Ngonyani ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Ally Sameji, Gray Mwakalukwa na Zena Kongoi.
“Pamoja na hayo, leseni za wachimbaji wadogo ikihusisha leseni 735 zilizopo izifute na izitoe upya na pia ianzishwe Kampuni ya Serikali ya Madini ya Tanzanite ili kuweza kukabiliana na mianya yote ya wizi na shughuli za uchimbani kwa kuzingatia upekee wa upatikanaji wa madini hayo duniani.

RIPOTI YA ALMASI
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Bunge iliyoundwa kuchunguza biashara ya madini ya almasi, Mussa Zungu, amewasilisha ripoti ya kamati yake na kueleza jinsi Serikali inavyopoteza fedha nyingi kupitia biashara ya madini hayo.
Katika maelezo yake, Zungu alisema mkataba ulioingiwa kati ya Serikali na Kampuni ya Madini ya Almasi ya WDL, unaiingiza hasara kwa kuwa Serikali hainufaiki nao.
“Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kukuhakikishia kwamba, kamati yetu yenye wajumbe 11, ilifanya kazi kwa usiri mkubwa ndiyo maana tangu tulipoanza kazi hadi leo, hakuna taarifa zozote zilizovuja kupitia vyombo vya habari.
“Wakati wa utendaji kazi wetu, tuliwahoji watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara, wachimbaji wa madini, tulipitia ripoti za kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa juu ya madini haya zikiwamo kamati za Bomani na Masha na pia tulikusanya data mbalimbali tulizoona zinatufaa.
“Tulichogundua ni kwamba, mgodi wa almasi ulioko Mwadui Shinyanga, Serikali haijaufanyia tathmini ili kujua kiasi cha almasi kilichobaki na pia maeneo ya wachimbaji wadogo hayafanyiwi tathmini na hivyo uchimbaji huo kufanyika kiholela na kwa kubahatisha.
“Ili kudhihirisha kwamba Serikali hainufaiki na mgodi huo, kati ya leseni 219 zilizotolewa huko, ni leseni moja tu ndiyo inayolipa mrabaha kupitia wachimbaji wadogo.
“Kibaya zaidi ni kwamba, kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka huu wa 2017, Kampuni ya WDL imekuwa hailipi kodi ya Serikali kwa kisingizio kwamba inapata hasara.
“Lakini, baada ya wajumbe wa kamati kuambiwa hivyo, walijiuliza ni kwanini wenye mgodi huo hawafungi biashara na kuondoka kama kweli wanapata hasara?
“Kingine tulichogundua ni kwamba takwimu za thamani ya madini zinazouzwa nje ya nchi zilizoko Wakala wa Usimamizi wa Madini Tanzania (TMA), ni tofauti na takwimu zilizoko Wizara ya Nishati na Madini.
“Kwa mfao, kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2017, taarifa za Wizara ya Nishati na Madini zinaonyesha almasi iliyosafirishwa nje ya nchi ina thamani ya Dola za Marekani milioni 362.1 wakati takwimu za TMA zinaonyesha madini yaliyosafirishwa yalikuwa na thamani ya Dola za Marekani 374.6.
“Hata takwimu za Wizara ya Nishati na Madini zinaonyesha kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2016, mrahaba uliotolewa ni wa Dola za Marekani milioni 18 wakati taarifa za TMA zinaonyesha zilitolewa Dola za Marekani milioni 15.
“Kwa maana hiyo, uchunguzi wa kamati umeonyesha kwamba, Serikali imekuwa ikipoteza mabilioni ya shilingi kutokana na mambo kutowekwa sawa katika uchimbaji wa madini hayo,” alisema Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala (CCM).
Katika ripoti hiyo, Zungu alisema almasi inayochimbwa Tanzania ina thamani kubwa lakini inauzwa kwa bei ndogo ikilinganishwa na almasi ya daraja la chini inayochimbwa Botswana na kuuzwa kwa bei kubwa.
Kwa mujibu wa Zungu, karate moja ya almasi nchini Tanzania inauzwa kwa Dola za Marekani 348 wakati kalate hiyo inauzwa kwa Dola za Marekani 1900 nchini Botswana.
Pamoja na hayo, alisema kuna upotevu wa Sh bilioni 100 zilizoingizwa katika akaunti ya Wizara ya Nishati na Madini Sh bilioni 100 kutoka akaunti ya Kanda ya Shinyanga.
“Lakini Katibu Mkuu wa Wizara Profesa James Mdoe alipoulizwa juu ya fedha hizo, alisema hazitambui licha ya kukaa katika wizara hiyo kwa muda mrefu.
“Yaani hata upotevu wa mapato ya Serikali mgodini hapo unasababishwa na Serikali kutokuwa na watumishi katika maeneo muhimu ikiwamo eneo la xray na eneo la recovery.
“Pia tuligundua almasi ya Tanzania haiuzwi kwa ukubwa wa jiwe bali inauzwa mkupuo na pia tabia ya kusafisha almasi kwa mara ya pili nchini Ubelgiji, inashusha thamani ya madini yetu hayo,” alisema Zungu.
Akizungumzia ununuzi wa mitambo mgodini hapo, alisema WDL wamekuwa wakinunua mitambo iliyokwisha tumika kwa gharama nafuu kutoka nje ya nchi na kuiambia Serikali kwamba mitambo hiyo ni mipya jambo ambalo alisema linachangiwa na wajumbe wa bodi wasiokuwa waaminifu.
Aidha Zungu alisema wakati wanachunguza biashara ya madini hayo, aligundua hata jinsi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alivyoshindwa kutambua mmoja wa mikataba ulioingiwa kati ya Serikali na WDL ambao alisema ulisainiwa nje ya nchi na kuletwa nchini.
Alisema WDL imekuwa ikikopa mikopo bila kuishirikisha Serikali ingawa ni mbia katika kuendesha mgodi huo.
“Hata kwa upande wa wajumbe wa Bodi, kuna wajumbe wawili waliteuliwa na waziri bila kufuata utaratibu, ingawa Katibu wa Wizara, Eliakim Maswi alishaagiza wajumbe wa bodi wateuliwe kwa kufuata vigezo vya utumishi wa umma.
“Hata Profesa Abdulkarim Mruma ambaye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya ukaguzi wa madini tulipomuuliza kwa nini alisaini mikataba na kuruhusu madini yapotee kizembe, alisema hakuisoma kwa sababu aliwaamini wasaidizi wake.
“Kwa kifupi, hata Maswi tulipomuuliza kuhusu uendeshaji wa WDL alisema kinachofanyika huko hakifai kwani alishafika Mwadui mara moja na Tanzanite one mara moja.
“Kwa kifupi, mgodi wa almasi wa Mwadui uko rehani kwa ridhaa ya Watanzaia wenyewe baada ya kusaini mikataba mibovu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, Zungu alisema kamati yake inapendekeza mikataba ya uchimbaji wa madini hayo ihakikiwe upya, ununuzi wa mitambo ukagulkiwe, wajumbe wa bodi wahojiwe, waliosaini mikataba wahojiwe pia serikalini arudishe asilimia 50 ya umiliki wa mgodi huo baada ya kukaa na mbia.
Hadi sasa mgodi wa Mwadui kuna tani milioni 105 za makinikia yenye thamani ya Sh trilioni 2.2.

JPM NA UAMUZI MGUMU
Kutokana na hali hiyo, leo Rais Magufuli atapokea taarifa ya uchunguzi wa madini ya tanzanite na almasi uliofanywa na kamati maalumu mbili zilizoundwa na Spika Ndugai.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilieleza kuwa ripoti hiyo itakabidhiwa kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa, Ikulu Dar es Salaam.
Hafla hiyo ya kukabidhiwa kwa taarifa hiyo, itarushwa moja kwa moja na vituo vya redio na televisheni kuanzia saa 4:00 asubuhi.
“Wananchi wote mnaombwa kufuatilia matangazo hayo kupitia vyombo vya habari na tovuti rasmi ya Ikulu ambayo ni www.ikulu.go.tz,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles