26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

CHONDE CHONDE, KENYATTA, RAILA


TANGU Mahakama ya Rufani ya Kenya ilipofuta matokeo ya uchaguzi wa rais nchini humo, viongozi wakuu wawili -Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee na Raila Odinga wa chama cha Nasa – wamekuwa wakitoa matamshi ambayo hayaonyeshi mwelekeo mzuri.
Kenyatta, pamoja na mambo mengine amekuwa akiwashutumu majaji waliotoa uamuzi huo, hasa dhidi ya Jaji Mkuu, David Maraga, kwamba atachukua hatua uchaguzi utakapomalizika.
Raila kwa upande wake amekuwa akiishutumu Tume ya Uchaguzi (IEBC) na kufikia hatua ya kusema hatashiriki uchaguzi wa marudio ambao umekwisha kupangwa kufanyika Oktoba 17, hadi yafanyike mabadiliko makubwa katika tume hiyo, ikiwamo kuwaondoa maofisa na makamishna wanaotuhumiwa kuvuruga uchaguzi huo.
Tunatambua kwamba kila mmoja kati yao, ana haki ya kuonyesha hisia zake na kutoa mawazo yake kutokana na uamuzi wa Mahakama hayo, ikizingatiwa kuwa matokeo ya uchaguzi huo yalimpa ushindi Kenyatta na kwamba Raila alikuwa ameshindwa.
Lakini wanachopaswa kuzingatia ni kwamba wao ni viongozi wakuu katika nchi yao na wana wafuasi wengi nchini humo.
Kwa sababu hiyo kila wanahokitamka au kukitenda ni lazima kitakuwa na matokeo chanya au hasi, siyo katika nchi hiyo tu, bali hata kwa njia jirani (hasa Jumuiya ya Afrika Mashariki) na dunia nzima kwa ujumla.
Na katika ujenzi wa demokrasia ya kweli, Mahakama ni chombo ambacho kina nafasi muhimu katika usuluhishi wa migogoro na kutoa uamuzi. Katika kuyatekeleza hayo kinapaswa kisipate vitisho, kiwe huru na uamuzi kinaoutoa wakati wote unapaswa uwe wa haki na huru na uheshimiwe.
Vilevile, viongozi nao wanatakiwa kuwa na uvumilivu wa kutosha na kutumia hekima na busara zao katika kutatua migongano yoyote miongoni mwao.
Kwa sababu hiyo inatosha kusema kwamba hatma ya Kenya hivi sasa iko mikononi mwa Kenyatta na Raila, hivyo hawana budi kutumia busara na hekima zao kuhakikisha suala la namna gani uchaguzi wa marudio unafanyika, linatatuliwa kwa amani.
Viongozi hao wanapaswa kuacha jazba katika matamshi na vitendo vyao kuepuka kuamsha hasira na vitendo vya vurugu miongoni mwa wanachama wa vyama vyao na wafuasi wao.
Hakuna jambo lisiloweza kutafutiwa ufumbuzi ikiwa wataamua kukaa chini wao na wadau wengine kuyatafutia utatuzi masuala yanayolalamikiwa, hasa na chama cha Nasa.
Watambue kwamba ikitokea amani ikakosekana nchini humo, athari zake hazikuwa nchini mwao tu, bali hata katika nchi jirani, hasa Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Matarajio yetu ni kwamba hekima na busara vitawaongoza katika kufikia ufumbuzi wa amani wa tofauti za mtazamo kati yao kuhusu uchaguzi wa marudio ambao umepangwa kufanyika mwezi ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles