MANCHESTER, England
KLABU ya Manchester United inajiandaa kusikiliza ofa zozote zitakazowasilishwa mezani kwao kuhusiana na wachezaji wao, Paul Pogba na Jesse Lingard mwishoni mwa msimu huu, ili kupata fedha za kumsajili Jadon Sancho.
Mkurugenzi wa United, Ed Woodward, ameonya kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi kipindi cha dirisha la usajili la kiangazi kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayosababishwa na janga la virus vya Corona linaloitesa Dunia kwa sasa.
Huku thamani ya Sancho ikiwa ni pauni milioni 100 kwa mujibu wa klabu yake ya Borussia Dortmund, Manchester United watalazimika kuvunja benki ili kumpata mchezaji huyo.
Kwa bahati nzuri kwa Manchester United, hali hiyo imetokea huku Juventus wakiwa tayari kumwaga fedha ili kumrejesha Pogba katika Ligi ya Serie A ya Italia.
Mabingwa hao wa Italia wanaripotiwa kuwa tayari kutoa wachezaji kuwapeleka United kama sehemu ya mpango wao wa kumnasa Pogba, huku Aaron Ramsey, Miralem Pjanic na Adrien Rabiot wote wakitajwa.
Pamoja na hilo, huku klabu zote zikiwa katika hali mbaya ya kiuchumi, inatarajiwa bei za wachezaji kuwa chini kuliko ilivyo kawaida.
Hata hivyo, Ole Gunnar Solskjaer alitumia pauni miliioni 47kumsajili Bruno Fernandes Januari, mwaka huu, hali inayoweza kuwafanya mabosi wa United kutokuwa tayari kutumia fedha zaidi kusajili mwaka huu.
Pogba amekuwa akihaha kusaka mlango wa kutokea Old Trafford, wakati Lingard amejikuta akiwa nje ya mipango ya Solskjaer.
Gazeti la The Sun limedai kuwa Marcos Rojo, Chris Smalling na Andreas Pereira nao ni wachezaji wazuri wanaoweza kuuzwa na United.
Sancho amekuwa na kiwango kizuri msimu huu ndani ya Dortmund, akiwa amefunga mabao 17 na kutoa pasi (assist) 19 za mabao katika mechi 35 zlizocheza.
Mkataba wake wa sasa na Dortmund unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2022, lakini bado kumekuwa na sintofahamu juu ya majaliwa yake ndani ya klabu hiyo.
Baada ya kuanzia soka lake Watford na baadaye kuhamia Manchester City kama mchezaji wa timu ya vijana, Sancho alijiunga na Dortmund mwaka 2017, uhamisho ambao tayari umeshalipa.