27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAMA SALMA AFURAHISHWA KUFUTWA TOZO ZA KODI

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA

 

MKE wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete, amesema kitendo cha Serikali kufuta baadhi ya kodi kimeleta matumaini makubwa kwa wadau binafsi wa maendeleo ambao walikuwa wakiumizwa na utitiri wa tozo.

 

Hayo aliyasema jijini Mbeya jana, wakati wa mahafali ya pili ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari ya St Marcus, inayomilikiwa na Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo.

 

Alisema Serikali haina budi kusifiwa kwa kazi nzuri iliyoifanya ya kuhakikisha uchumi wa nchi unakua kupitia sekta ya viwanda na kilimo, lakini kubwa zaidi ni pale ilipoona umuhimu wa kuziondoa kodi hizo.

 

“Nitakuwa mchoyo wa fadhila iwapo sitaishukuru Serikali iliyoko madarakani kwa kuandaa mazingira mazuri ya kisheria, hali ya usalama na miundombinu rafiki, lengo ni kuwezesha ushiriki wa wadau wa maendeleo, wakiwamo watu binafsi kama wamiliki wa shule kwa kuondoa baadhi ya kodi ambazo zilikuwa ni changamoto kubwa kwa wawekezaji wa nje na ndani ya nchi,” alisema.

 

Alisema watu wanapotozwa kodi ya mabango kila baada ya mwaka au miezi sita, ni changamoto kubwa na wakati mwingine ilikuwa ni kikwazo kwa wawekezaji, “lakini tunaishukuru serikali kwa kuliona hili na kutambua ya kwamba wadau binafsi nao ni wasaidizi wa serikali na kuziondoa kodi hizo,” alisema.

 

Alitumia nafasi hiyo kuwaasa wazazi na walezi kutambua kuwa, msingi mkubwa wa mafanikio ya viwanda ni wao kuhakikisha wanawapeleka watoto shule ili wasome na waje kuwa wataalamu watakaoendesha viwanda hivyo.

 

Hata hivyo, alitaja changamoto kubwa inayokatisha ndoto za watoto wa kike kuwa ni mimba za utotoni, kwani takwimu za mwaka 2015/16, kitaifa zinaonyesha watu waliopatwa na tatizo hilo ni asilimia 23, lakini katika Mkoa wa Mbeya kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu, wanafunzi 76 wamekatisha masomo.

 

“Wanafunzi 76 ni wengi, wazazi tulikatae suala hili la mimba zinakatisha ndoto za watoto, jambo la kujiuliza ni kwanini watoto wapate mimba? Hii inaonyesha ni jinsi gani wazazi tumejipa likizo ya majukumu yetu, wakati umefika wa kupigana na ndoto za mtoto wa kike ili zitimie,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles