Na WAANDISHI WETU – DAR/MIKOANI
HATUA ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwataka akina mama waliotelekezewa watoto na waume zao katika mkoa wake waende kushtaki kwake ili wachukuliwe hatua za kisheria imeibua mjadala wa kitaifa.
Jambo hilo sasa linaonekana kugusa kila kona ya nchi kwani licha ya kuwalazimisha baadhi ya viongozi kulitolea ufafanuzi na wengine kulijadili kwa namna ya kumuunga mkono au kumpinga, Bunge nalo limejikuta katika mwelekeo huo huo.
Wakati juzi tu Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akilazimika kulizungumzia suala hilo na kuwataka watu wasiishie tu kuponda bali kulitazama kama jambo ambalo linaweza kuibua takwimu za awali kujua ukubwa wa tatizo na kisha kufanyiwa kazi zaidi na mifumo rasmi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk. Stephen Munga, amesema kimsingi suala hilo si la Mkoa wa Dar es Salaam pekee bali Tanzania nzima.
Askofu Munga ambaye alikuwa akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa simu, amesema suala hilo ni la kitaifa hivyo linahitajika mjadala mkubwa.
“Kwa jambo hili lililofanyika huko Dar es Salaam hakuna mtu anayeweza kukataa kuwa si jambo zuri kwani kila mmoja anajua kuna umuhimu mkubwa wa mtoto kupata matunzo ya pande zote mbili na hata sisi huku tuna maonyesho ya wiki nzima ya kuonyesha namna ya kuwa baba bora,” alisema.
Alisema ingawa limeanzishwa Dar es Salaam, ni wakati sasa wa mamlaka husika ikiwamo Ustawi wa Jamii kulisimamia na kulifanyia kazi.
“Hili ni tatizo hivyo lisiwe ni suala kama tukio tu bali mamlaka zinazohusika katika masuala haya, Ustawi wa Jamii walifanyie kazi kwa kina, wafuatilie na kujua chanzo hasa nini kama ni uchumi, au jambo jingine kwani hakuna tatizo ambalo halina kiini ya kilipoanzia,” anasema.
Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, amesema Jumatatu Aprili 16, mwaka huu Kamati ya Amani inatarajia kuwa na mkutano na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na suala hili litakuwa ni miongoni mwa mambo ambayo yatazungumziwa.
Uamuzi wa Makonda umeonekana pia kugusa pia mijadala ya Bunge la bajeti inayoendelea mjini Dodoma, kwani ni juzi tu Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima, wakati akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2018/2019, licha ya kuhoji Mkuu huyo wa Mkoa anakopata mamlaka ya kisheria kutatua jambo hilo, lakini alisema limetoa taswira jinsi ambavyo mifumo ya Serikali imeshindwa kufanya kazi yake.
Jana Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Toufiq (CCM), naye aliiomba Serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya ushauri nasaha kutokana na kina mama wengi kujitokeza katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakidai matunzo ya watoto.
Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, Mbunge huyo alisema siku za hivi karibuni mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza wakina mama waliotelekezewa watoto walijitokeza kwa wingi.
Alisema hali hiyo inatokana na ukosefu wa elimu ya ushauri nasaha na kwamba wananchi wengi hawafahamu pa kwenda pale wanapopata matatizo.
Katika hilo alihoji kama Serikali haioni umefikia wakati wa kuhabarisha jamii kupitia huduma hiyo.
“Maofisa ustawi wa jamii wapo katika maeneo mbalimbali je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga siku maalumu walau siku mbili kwa wiki na kutenga maeneo maalumu ili wapate ushauri nasaha?” aliuliza.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema ombi hilo watalifanyia kazi na kutoa rai kwa jamii kuwa huduma za ustawi wa jamii zipo katika
halmashauri na wanapokuwa na changamoto zozote waende huko.
Ukiacha Bunge, huko mkoani Iringa Mwenyekiti wa shirikisho la waganga wa tiba asilia, Simba Kasige, amemtaka Makonda kusitisha zoezi hilo kwani limelenga kuwavunjia heshima wanaume na kuvunja ndoa za baadhi ya watu.
Akizungumza jana mjini Iringa wakati wa mahojiano katika kipindi cha gari la Matangazo Radio Nuru FM, alisema kuwa zoezi hilo limeanzishwa pasipo kutafakari madhara yake na kuwa wanawake wanaokwenda kwa Makonda wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuingilia ndoa za watu.
“Sisi kama waganga wa tiba asilia tunaomba sana Serikali kutumia vizuri ofisi za umma ziwe kwa ajili ya kujenga amani na kuleta maendeleo ya Taifa si kutafuta umaarufu unaovunjia watu heshima zao, hii ni ajabu sana ni kituko kuona ofisi ya mkuu wa mkoa inatumika kuwachafua baadhi ya watu,” alisema licha ya kukiri wapo wanawake ambao wametelekezwa.
Alitoa wito kwamba wanawake wote waliokwenda kwa Makonda kudai wametelekezewa watoto majina yao yachukuliwe ili watakaobainika kuzaa wa waume za watu wafunguliwe kesi mahakamani.
Kwa mujibu wa Makonda, wanawake 480 waliofika katika ofisi yake mapema wiki hii kati yao 47 wamesema wametelekezwa na wabunge huku 14 wakieleza wametelekezwa na viongozi wa dini.
Makonda aliyasema hayo Aprili 10, alipokaribishwa kutoa salamu za mkoa, mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakati wa hafla ya uzinduzi wa chanjo ya saratani iliyofanyika katika viwanja vya Mbagala Zakhiem, Temeke jijini hapa.
“Wengine wamewataja wafanyabiashara mashuhuri ambao ukiwatazama huwezi kuamini kama wanafanya ukatili huu,” alisema.
Amesema takwimu zinaonyesha katika mwaka 2017, walizaliwa jumla ya watoto 129,347 na kwamba asilimia 60 wametelekezwa huku katika kituo kimoja kilichopo Wilaya ya Kinondoni pekee wanatunzwa watoto 274 ambao waliokotwa.
“Watoto hao waliokotwa wakiwa wametupwa kwenye mifuko ya rambo kama takataka, kina mama hawa wanateseka kulipa kodi, kununua chakula cha familia na mambo mengine.
“Kisha wengine wanasema Makonda nahusikaje humu wakati haya ni mambo ya Ustawi wa Jamii, sisi tunaendelea na nimeongeza siku za kuonana na kina mama hao,” alisisitiza.