25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

PENEZA, LUSINDE WACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENI

 

Na Fredy Azzah- Dodoma


MBUNGE wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza na mwenzake wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, wamechafua hali ya hewa bungeni jana walipokuwa wakichangia Bajeti ya Ofisi ya Utumishi na Tamisemi, baada ya mmoja kuhusisha jina la Rais katika mchango wake na mwingine kusema Chadema imejaa ufisadi.

Peneza alijikuta akizuiwa kuchangia bungeni na kulazimishwa kuketi chini huku Lusinde akiombewa taarifa kutoka kwa wabunge wa Chadema, ingawa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alikataa kuruhusu akisema: “Nimeshasema sipokei tena taarifa.”

Peneza alianza kwa kusema: “Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Mjini) jana alipochangia akitoa taarifa alisema hizi wizara ziko chini ya ofisi ya Rais, Rais mwenyewe ndiye Waziri katika wizara hizo.”

Alisema kuhusu utawala bora, Rais ameapa kulinda Katiba lakini wakati wizara inayohusika na utawala bora ikiwa chini yake, vyama vya siasa haviruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara wala Bunge kuonyeshwa moja kwa moja na runinga wakati wa mijadala.

Baada ya kauli hiyo ikiwa ni dakika ya kwanza Peneza akiwa anachangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, aliomba kupewa utaratibu akisema mbunge huyo anatumia jina la Rais jambo ambalo haliruhusiwi kikanuni.

Zungu alisimama na kusema: “Rais jina lake halitumiwi kwa dhihaki, halaumiwi wapo mawaziri unaweza kuhoji utendaji wao, huwezi kuuliza utendaji wa Rais.”

Baada ya Zungu kumwona Peneza akiendelea na mazungumzo na wabunge wengine alisema: “Nisikilize ukiendelea kusikiliza watu wengine utajiingiza kwenye makosa, utajiingiza kwenye matatizo.”

Zungu aliagiza kufutwa katika kumbukumbu za Bunge kauli za mbunge huyo ambazo ziko kinyume na kanuni.

Upendo alipopewa tena nafasi ya kuchangia, alibadilisha lugha badala ya kutumia neno Rais akatumia mkuu wa nchi katika kujenga hoja zake hali iliyofanya Mhagama asimame tena.

Hata hivyo, Zungu, hakumpa nafasi ya kuzungumza na badala yake kuwataka wote kukaa na kusema: “Natumia kanuni ya 73 hutazungumza tena (Peneza).” Kisha kumuita mchangiaji mwingine.

Kwa upande wake, Lusinde, alisema Chadema inapiga kelele kuhusu ufisadi lakini ni vyema viongozi wake wakajisafisha kwanza.

Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha ufisadi mbalimbali ndani ya chama hicho ikiwa ni pamoja na mkopo wa Sh bilioni mbili unaodaiwa kuombwa na chama hicho kwa mmoja wa wanachama wake kwa ajili ya shughuli za kichama huku kukiwa hakuna nyaraka za kuonyesha kama ulitolewa na kupokelewa.

Pia alisema ripoti hiyo inaonyesha kuwa Sh milioni 866 zililipwa kwa mwanachama kwa niaba ya chama hicho kwa ajili ya mabango ya chama bila kuambatanisha makubaliano ya kisheria.

“Wajinga ndiyo waliwao, mmeng’ang’ania maandamano wengine wanapiga fedha. Kuna shilingi bilioni mbili zilikusanywa bila kuingizwa katika akaunti ya wadhamini, kutopeleka benki kunaonyesha shilingi bilioni 24 zilitumika kwenye ununuzi bila kufuata utaratibu, badala ya kushughulikia ufisadi ndani ya chama chao wanakazana kukosoa Serikali na CCM.

“Nataka Watanzania waelewe ufisadi mkubwa uko Chadema, nipigeni makofi kwa ukweli ninaowaambia. Mna ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 10 hamna hata ofisi mikoani, mnataka kufanana na chama cha Zitto,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles