Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amewataka wakaguzi katika nyanja ya utafiti kutumia mafunzo waliyopata kusimamia sheria na kanuni zitakazo waongoza katika kutekeleza majukumu kwa kulinda mazingira na afya ya Mtanzania.
Akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wakaguzi 14 waliopatiwa mafunzo ya ukaguzi wa matumizi salama ya Bio-teknolojia hasa kwenye chakula na mimea jijini Dar es Salaam jana, alisema eneo hilo nyeti limebeba thamana kubwa ya usalama maisha ya binadamu na mazingira.
“Ni waombe wakaguzi wote kuwa na weledi katika kufanya kaguzi kwani kazi hii ni ngumu kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya teknolojia. Ni vizuri mjiongeze katika kutafuta taarifa zitakazo wawewezesha kutekeleza majukumu haya,” alisema Waziri Makamba.
Alisema uwelewa wa jamii na wafanyabiashara juu ya matumizi salama ya bio-teknolojia ambayo wanabadili viumbe kuingizwa kwenye chakula au mimea kutokana na teknolojia ya ‘Genetically Modified Organism’(GMO) hivyo ni lazima kutoa elimu kwanza kwa waingizaji wa bidhaa ili kujengewa uelewa na kulinda afya za wananchi na mazingira.
Makamba alisema suala la ukaguzi wa usalama wa mimea na chakula hasa kwa mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani ni lazima wataalumu waliochaguliwa wawe na uelewa ambapo wataweza kutekeleza majukumu yao na ushirikiano unahitakija katika kufanisha jukumu hili.
“Sheria na Kanuni zipo zitakazowaongoza katika kufanya ukaguzi lakini ni lazima tuhakikishe kwanza wadau wamejengewa uelewa kabla ya kuanza kusimamia Sheria katika bidhaa zenye GMO,” alisisitiza Waziri Makamba
Kwa upende wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk. Amos Nungu, alisema mafunzo haya yatakwenda kuwaongoza wakaguzi hawa katika kutekeleza majukumu yao.
“COSTECH tumeratibu mafunzo haya kwa sababu yanalenga teknolojia hivyo tumeona ni muhimu wakaguzi wakapewa mafunzo kwanza ili wakatekeleze kaguzi zao katika vituo vya utafiti ili kuilinda nchi yetu na mabadiliko ya Bio teknolojia,” alisema Dk. Nungu.