|Editha Karlo, Kigoma
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Hospitali ya Wilaya ya Kasulu kwa wizi wa dawa.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza iundwe tume kuwachunguza watumishi hao kutokana na tuhuma hizo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Umoja Mjini Kasulu, Waziri Mkuu amesema akiwa ziarani mkoani Kigoma alitembelea hospitali hiyo na kukutana na malalamiko na kero nyingi ikiwamo watumishi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiiba dawa na vifaa mbalimbali na kuziuza katika maduka ya mtaani.
“Nimeagiza wakati watumishi hao wamesimama kazi iundwe tume ya kuchunguza ikibainika ni kweli basi tunawafuta kazi tubaki na watumishi waaminifu.
“Hospitali yenu ya Wilaya ina matatizo sana, tukileta computer wanaiba, kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu pale dawa zinaibiwa kisha wanaenda kuuza kwenye maduka ya mjini, sasa yale maduka ya mjini yanayonunua dawa za hospitali tutayafunga,” amesema.