MAULI MUYENJWA NA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM
MWILI wa Ernest Materego aliyekuwa akigombewa mahali pa kuzikwa umewasili jijini Dar es Salaam jana tayari kwa maziko.
Materego ambaye alifariki dunia Novemba 19, mwaka huu na maiti yake kugombewa na watoto, mke na ndugu wa marehemu kuhusu wapi azikwe kiasi cha kufungua kesi mahakamani ambapo mahakama iliamua azikwe jijini Dar es Salaam badala ya Bunda ambako ndugu zake walipanga.
MTANZANIA lilifika nyumbani kwa marehemu maeneo ya Mombasa Gongolamboto, jijini Dar es Salaam ambapo lilikuta hakuna chochote kinachoendelea kuashiria kwamba kuna msiba.
Dada wa marehemu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa familia, aliyekuwapo nyumbani hapo, aliliambia MTANZANIA kuwa mwili huo ungewasili jana na kisha taratibu za maziko zianze.
“Msiba haujafanyika na hakuna chochote kinachoendelea kwa leo, tunashughulikia kupata eneo la kumzikia wakati tunawasubiri waliokwenda Bunda kurudi na mwili wa marehemu leo (jana) usiku,” alisema.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, juzi iliamuru mwili wa marehemu Ernest Materego uliosafirishwa Novemba 24, mwaka huu kwenda Bunda kwa maziko urejeshwe Dar es Salaam kwa ajili ya kuzikwa.
Marehemu Materego alifariki Novemba 19, mwaka huu jijini Dar es Salaam na Novemba 24 mdogo wa marehemu, Gonche Materego aliyekuwa akimuuguza na wenzake walisafirisha mwili huo kwa ajili ya mazishi Bunda mkoani Mara.
Watoto wa marehemu, Joyce, Edwin, Rita, Irene na mama yao mzazi, Dinah Willige (65) walipinga mahakamani wakiomba amri mwili urejeshwe wazike Dar es Salaam kwa sababu wanadai baba yao aliwaambia akifariki azikwe Dar es Salaam.
Wadaiwa akiwamo mdogo wa marehemu, Gonche, mke mdogo wa marehemu, Mwajuma Hassani (39), rafiki wa marehemu Thobias Mwita (66) pamoja na majirani walitaka mwili huo uzikwe Bunda wakidai kuwa marehemu alitaka kuzikwa kwao.