30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUNIA YA MKAA 500,000 HUTUMIKA DAR

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM               |              


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema ripoti ya mazingira ya mwaka 2014 inaonyesha Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa matumizi ya nishati ya mkaa.

Alisema mkoa huo hutumia tani 500,000 kwa mwaka jambo ambalo linahitaji nishati mbadala, vinginevyo kutatokea madhara makubwa nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Majaliwa alisema ripoti hiyo pia inaonyesha hekta 372,000 za misitu hukatwa nchini kwa mwaka, hivyo elimu ya uhamasishaji na teknolojia mbadala ndivyo vitakavyoiokoa misitu hiyo.

Alisema Msitu wa Kazimzumbwi uliopo Kisarawe umeathiriwa kwa sababu ya ukataji miti hovyo, kwamba asilimia 70 nishati ya mkaa unatumika Dar es Salaam tofauti na vijijini ambako wengi wanatumia kuni zilizokauka na kuanguka zenyewe.

“Ili kuokoa mikoa mbalimbali ambayo kwa sasa imeathiriwa na ukataji miti hovyo, ni vyema mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi kuhakikisha kuanzia sasa utoaji wa vibali hivyo katika majengo makubwa ya binafsi na Serikali vizingatie mifumo ya usambazaji gesi ili kutokomeza matumizi ya nishati ya mkaa na kuni,” alisema.

Majaliwa alisema tafiti zinaonyesha majengo makubwa mengi yana matumizi makubwa ya mkaa na kuni, hivyo kitendo cha kufunga mifumo ya nishati mbadala kitasaidia kupunguza matumizi hayo.

Alisema kuanzia sasa wakuu wa mikoa wahakikishe wanatembelea taasisi za umma na binafsi ili kuwapa muda maalumu wa kubadili mifumo ya matumizi ya kuni na mkaa, kwani itasaidia kuongeza tija ya nishati mbadala na kulinda misitu iliyopo nchini.

“Ninaomba kuanzia sasa teknolojia mbadala zisambazwe nchi nzima ili watumiaji wake wabadilike, mfanye ukaguzi kila baada ya miezi sita na ifikapo 2020 mfanye ukaguzi wa kina,” alisema Majaliwa.

Alisema maadhimisho ya Siku ya Mazingira hufanyika kila mwaka Juni 5, na kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘mkaa ni gharama, tumia nishati mbadala’.

Majaliwa alisema wameamua kufanya maadhimisho hayo ndani ya Dar es Salaam kwakuwa ni kinara wa matumizi ya mkaa na wanataka kuelimisha jamii kuwa nishati mbadala ni muhimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ambaye ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema asilimia 70 ya mkaa unaokuja Dar es Salaam unatokea mkoani Pwani.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, January Makamba, alisema Mkoa wa Dar es Salaam pekee unatumia magunia ya mkaa 300,000 kwa siku.

Alisema mbali ya uwepo wa gesi asilia nchini, asilimia 90 ya Watanzania bado wanatumia mkaa na kwamba Dar es Salàam pekee inatumia asilimia 70.

“Ifike wakati jamii inapaswa kuelewa maendeleo yetu kama nchi yamefungamana moja kwa moja na mazingira hivyo utunzaji mazingira ni muhimu ,” alisema Makamba.

Alisema kuna kila sababu ya kuendelea kupiga kelele utumiaji wa nishati ya mkaa kwa sababu asilimia 70 hadi 80 ya miti inayokatwa, inatumika kuchoma mkaa tofauti na vijijini ambako wao wamekuwa wakiokota kuni zilizokauka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles