30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SIMULIZI YA KUSHANGAZA YA MFALME UMBERTO, ‘PACHA’ WAKE

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM


WIKI iliyopita tulishuhudia simulizi ya kushangaza lakini ya kweli kuhusu mbwa aliyekuwa akienda kuhiji asubuhi na jioni kwenye stesheni ya reli nchini Japan kwa zaidi ya miaka 10.

Mbwa huyo wa Kijapan, alifanya hivyo baada ya kifo cha bwana wake akikumbuka namna alivyokuwa akimsindikiza stesheni asubuhi na kumpokea jioni aliporudi kutoka kazini. Hiyo ilikuwa katika miaka 20 ya mwanzoni mwa 1900.

Leo katika safu yako hii, tunakuja na simulizi nyingine ya kale isiyo ya kawaida lakini pia inayoaminika kuwa ya kweli kumhusu Mfalme Umberto I wa Italia, aliyeuawa Juni 29, 1900.

Kabla ya uajabu huo wa simulizi hii, tuangalie kwanza kwa historia ya Mfalme huyo, ambaye ni wa tatu kutoka mwisho kutawala Italia.

Umberto Ranieri Carlo Emanuele Giovanni Maria Ferdinando Eugenio di Savoia alizaliwa Machi 14, 1844.

Alisimikwa ufalme baada ya kifo cha baba yake, Mfalme Victor Emmanuel wa Pili wa Italia Januari 9, 1878, akipewa Jina la Umberto wa kwanza.

Alikabiliwa na jaribio la kwanza la kumuua Novemba 17, 1878 huko Naples na mfuasi wa itikadi ya utawala huria (anarchy), Giovanni Passannante.

Anarchy ni itikadi ambayo haiamini katika utawala wa sheria na serikali, kwa maneno mengine haitaki uwapo wa mamlaka yoyote katika nchi.

Umberto aliweza kukwepa jaribio hilo na mchoraji wa ramani ya shambulio hilo akahukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha katika chumba cha gereza chenye kuta ya urefu wa mita 1,4.

Bila uwapo wa maji safi na pingu ya minyororo yenye uzito wa kilo 18, yalikuwa mateso tosha kumuua anarchist huyo katikati ya matatizo ya kisaikolojia. Adhabu ya kifo ingetolewa tu iwapo mfungwa huyo angesababisha kifo cha Umberto.

Akichukiwa mno na wana- ‘anarchists’, Mfalme Umberto I akawa mwathirika wa shambulio la pili kutoka kwao karibu na Rome Aprili 22 1897 likiendeshwa na Pietro Acciarito.

Kilichomuokoa bila shaka ni polisi kutahadharishwa mapema na baba wa Pietro kuwa macho na mwanawe huyo baada ya kuona nyendo za kutia shaka.

Mfalme Umberto I alikuwa akihudhuria mbio za farasi nje kidogo ya Jiji la Rome wakati wa maadhimisho ya 29 ya ndoa yake na mkewe Malkia Margherita.

Hata hivyo, Pietro Acciarito aliweza kufika karibu na gari la mfalme akiwa amejihami kwa kisu. Umberto aliiona silaha hiyo na hivyo aliweza kukwepa shambulio.

Pietro alikamatwa mara moja. Chunguzi dhidi ya matukio kama hayo zilikuwa kisingizio cha kuwasweka jela na kuwatesa vikali wapinzani wa kisiasa kama wanajamhuri, wasoshalisti na waasi, akiwamo Romeo Frezzi ambaye alitiwa hatiani kwa kukutwa akiwa pichani na Pietro Acciarito.

Utawala wa Umberto I ulitawala wakati wa kipindi cha mizozo ya kijamii, na ilikuwa ikitokea kote barani Ulaya na mwenendo wake ukasababisha ugumu wa kuidhibiti.

Maandamano makubwa kuhusu kupanda kwa bei ya mkate yalitokea nchini humo na Mei 7, 1898 Jiji la Milan liliwekwa chini ya udhibiti wa kijeshi na Jenerali Bava-Beccaris.

Beccaris aliamuru matumizi ya mabomu ya mpira kwa waandamanaji na mamia ya watu wakauawa na wengine maelfu kujeruhiwa.

Kinyume na maoni, mtazamo na utashi wa wengi, Mfalme Umberto I alimsifu Bava-Beccaris kwa kurudisha utulivu mjini Milan na akaenda mbali zaidi kumtunza kwa ushujaa uliotukuka!

Hata hivyo, simulizi hiyo hapo juu si kitu cha ajabu; ni sehemu ya maisha, ambayo bado tunayashuhudia katika zama hizi. Simulizi yetu ya kushangaza inaanzia hapa chini.

Inaelezwa usiku wa Julai 28, 1900, Mfalme akiwa ameambatana na mlinzi wake Jeneral Emilio Ponzia-Vaglia aliingia kwenye mgahawa mdogo huko Monza karibu na Milan.

Wakati mmiliki wa mgahawa alipojitokeza kumhudumia Mfalme Umberto, wawili hao wakakutanisha nyuso na kuangaliana kwa mshangao. Ilikuwa kana kwamba walikuwa wakitazama kioo. Walifanana mno kwa kila kitu, mapacha wa aina yake!

Wawili hao wakaanza kujadiliana kuhusu kufanana kwao na haikuchukua muda ikabainika kuwa kulikuwa na mengine ya kushangaza.

Wote waliitwa Umberto, wote walizaliwa tarehe moja Machi 14, 1844. Wote walizaliwa mjini Turin na wote walioa wanawake wenye jina moja: Margherita na siku moja.

Zaidi ya hayo, mmiliki wa mgahawa huo, ambao bado upo hadi leo hii, alifungua biashara yake siku ile ile Mfalme Umberto aliyotawazwa kuwa Mfalme wa Italia.

Sehemu ya kushangaza zaidi ya simulizi hii ni kwamba siku iliyofuata Julai 29, 1900, mfalme, ambaye alialikwa Monza kuhudhuria tukio la kufunga mashindano ya sarakasi, alifahamishwa kuwa yule mmiliki wa mgahawa aliuawa saa chache zilizopita katika shambulio la kutaanisha lililoendeshwa na wasiojulikana.

Mfalme ambaye hakuwa amevaa kinga mwilini kinyume na ushauri wa walinzi wake baada ya kudai uwapo wa joto, dakika chache tu baada ya kusikia taarifa hizo, aliuawa na anarchist wakati alipoondoka jukwaani kwenda kupanda kigari chake kilichokuwa kikimsubiri baada ya kufunga mashindano hayo.

Muuaji Gaetano Bresci alidai alitaka kulipiza kisasi kwa watu waliouawa wakati wa operesheni iliyoendeshwa na Jenerali Bava-Beccaris, ambayo haisahauliki kwenye historia ya taifa hilo.

Muoano huo wa mambo umezua mjadala wa namna gani ukatokea na iwapo si simulizi iliyotiwa chumvi.

Lakini kitu kimoja bila ubishi ni kwamba maisha ya baba wa Mfalme Umberto, yaani Victor Emmanuel II yalitawaliwa na utitiri wa wanawake, tabia ambayo inaweza kuzaa sehemu ya hali hiyo.

Mbali ya wadogo zake saba, ambapo mmoja alifariki dunia akizaliwa, Mfalme Umberto alikuwa na ndugu zake wengine wawili kutoka kwa ndoa ya awali ya marehemu baba yake na wengine sita wa nje ya ndoa, akiwamo mmoja pia aliyefariki wakati akizaliwa kutoka kwa wanawake wengine wanne.

Kwa sababu hiyo, ikitokea Umberto akawa na ndugu wa kufanana, sababu za nje ya uwezo wa Mfalme zinaweza kuwatenganisha.

Maswali ya kujiuliza ni je, mfalme alikuwa na pacha wanayefanana na kwa sababu za kisiasa, mmoja wa ndugu akaondoshwa kwenda kulelewa na familia nyingine?

Inawezekanaje kwa watoto wawili kuzaliwa siku moja, mji mmoja wenye jina moja, ambao wazazi wao hawakuweza kuwaona? Je, walizalishwa na wakunga ambao waliamua kumficha au kumuuza pacha mmoja kwa familia nyingine?

Na je, tukio lenye utata la shambulio dhidi ya mmiliki wa mgahawa, ni tatizo la muuaji kumfananisha na mfalme?

Ikumbukwe, muuaji yaani Gaetano Bresci, alikuwa mhamiaji nchini Marekani ambaye aliendesha gazeti la wana-anarchy huko Paterson, New Jersey.

Alirudi nchini Italia wiki chache tu kabla ya kumuua mfalme. Je, alishuhudia mkutano wao usiku ule katika mgahawa huo? Je, aliamua kuwaua wote kuhakikisha kampata mlengwa halisi? Ni maswali yasiyo na majibu hadi leo hii.

Hata hivyo, Mfalme Umberto alifahamika kama Kiongozi wa Italia, ambaye aliitoa nchi yake kutoka upweke na kwa kujenga ushirika na nchi tatu za Austria, Hungary na Germany na alijaribu kupanua utawala wake hadi Afrika hususani Ethiopia na Ertirea.

Na Aliunga mkono sera za kizalendo na kifalme, ambazo ziliizoofisha Italia na kusababisha kifo chake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles