Anna Potinus
Kuelekea maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanzania yatakayofanyika Desemba 9 mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli amewataka wananchi kudumisha amani na upendo huku akiwasititiza kuachana na tabia ya ubaguzi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 7, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilomita 3.2 katika Ziwa Vitoria litakalounganisha Mkoa wa Mwanza na Geita pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66.
“Tuendelee kuitunza amani yetu tusibaguane kwasababu ya dini, sura au hata kwasababu ya hali zetu mawazo yetu wote yawe ni Tanzania moja niwaombe sana wakati tunajiandaa kusheherekea miaka 58 ya uhuru tulioupata kutoka kwa wakoloni tudumishe amana na upendo kwani palipo na amani kuna maendeleo.
“Ujenzi wa daraja hili ni udhibitisho kuwa nchi yetu sio masikini na kwamba sisi Watanznaia tukiamua tunaweza, vijana tumieni huu mradi isije ikatokea watu wa maeneo mengine wakaja kutoka mbali na kuutumia na mmesikia wale wote watakaoguswa na mradi huu watalipwa fidia na ndio maana kuna zaidi ya bilioni 3.145 zilizotengwa kwaajili ya kuwalipa wale watakaofuatwa na mradi huu,” amesema Rais Magufuli.
Ujenzi wa daraja hilo la Kigongo – Busisi utagharimu Sh bilioni 699.2 na litakuwa la kwanza kwa ukubwa kwenye eneo zima la Afrika Mashariki na la sita kwa ukubwa katika bara la Afrika.