Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amewahakikishia mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kuwa Serikali yake itakuza zaidi ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo kati yao katika nyanja za maendeleo na ustawi wa jamii.
Kauli hiyo aliitoa Ikulu, Dar es Salaam juzi katika sherehe ya mabalozi wa nchi mbalimbali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Sherry Party).
Pia aliwashukuru wanadiplomasia hao kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mipango mbalimbali na kubainisha kuwa utekelezaji wake, hususani miradi ya maendeleo unafanyika kwa mafanikio makubwa.
Aliyataja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka jana kuwa ni kulinda na kudumisha amani na usalama, kusimamia vizuri uchumi uliokua kwa wastani wa asilimia saba na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano zenye uchumi unaokua kwa kasi zaidi barani Afrika.
Pia kudhibiti mfumuko wa bei uliokuwa wastani wa asilimia 3.5 na Tanzania kuibuka kinara katika kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.18.
Alisema mwaka jana Tanzania iliendelea kutekeleza miradi yake mikubwa ya miundombinu ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway – SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kuanza maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa megawati 2,100 katika Bonde la Mto Rufiji, kuendeleza miradi ya kusambaza umeme, upanuzi wa bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, ujenzi wa meli katika Ziwa Victoria, ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na ujenzi wa rada nne.
“Miradi mingine ni upanuzi wa huduma muhimu za kijamii hususani afya, elimu na maji ambapo vituo vya afya 305 na hospitali za wilaya 67 zinajengwa, kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa na kwa mwaka 2018 Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilifanya upasuaji kwa wagonjwa 1,361, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo na upatikanaji wa maji vijijini kufikia asilimia 65 na mijini asilimia 80,” alisema.
Magufuli aliyataja maeneo mengine kuwa ni kushiriki kikamilifu katika masuala ya kimataifa, kushiriki majukumu ya kulinda amani ambapo askari 1,900 wapo katika maeneo mbalimbali ya ulinzi wa amani na kuhudumia wakimbizi na kwa sasa idadi yao hapa nchini imefikia 324,420.
Pia alisema kwa mwaka huu, Tanzania imejipanga kuendeleza malengo mbalimbali yakiwamo kukuza uchumi kwa kuzingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/17 – 2020/21) unaoelekeza kufikia uchumi wa kati na kuweka mkazo katika sekta ya kilimo, utalii, usafiri wa anga na madini.
Aliwasihi mabalozi kuendelea kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji na biashara zilizopo hapa nchini na ameahidi kuwa Serikali itakuwa tayari wakati wote kuhakikisha wawekezaji watakaokuwa tayari kuwekeza wanapata ushirikiano wa kutosha kufanikisha uwekezaji huo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi hao, kiongozi wa mabalozi ambaye ni Balozi wa Comoro hapa nchini, Dk. Ahamada Mohammed, alimshukuru Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakiupata kutoka serikalini na ameahidi kuuendeleza.
Pia aliahidi kuwa mabalozi watampa ushirikiano wa kutosha Waziri mpya wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi na wapo tayari kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zikiwamo vita dhidi ya rushwa, kuboresha maisha ya watu, kujenga viwanda na kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zao.