MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema Serikali yake haitakuwa na mchezo wala ubabaishaji, hasa kwa watumishi wa umma.
Alisema kutokana na msimamo wake huo ambao baadhi ya watu wanaujua, umefanya baadhi ya wabadhirifu ambao ni watumishi wa umma wamchukie.
Kauli hiyo aliitoa jana katika mikutano yake ya kampeni ya kuomba kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano, katika wilaya za Newala, Tandahimba na Mtwara Vijijini na baadaye kuhitimisha Mtwara Mjini, ambapo alisema sasa umefika wakati wa kuongoza Serikali kwa vitendo na si kwa maneno.
Dk. Magufuli, alisema hakugombea urais kwa makosa ila ameomba nafasi hiyo kwa ajili ya kuwafanyia kazi Watanzania.
“Katika uongozi wangu sina mchezo na sitaki ubabaishaji, nimedhamiria kuwatumikia Watanzania kwa vitendo.
“Unapoomba nafasi ya uongozi ni lazima umtangulize Mungu, nami nimefanya hivyo, kwa sasa kuna watu wanasema Magufuli mkali, ni kweli mimi mkali, hasa katika kutafuta maendeleo ya watu wote wa Mungu ambao naamini mtanichagua.
“Wapo watu serikalini ambao wamekuwa wakitupaka matope mpaka kufanya CCM ichukiwe, sasa nataka kushughulika nao. Unapokuwa na kitanda kina kunguni choma kunguni wote lala usingizi wako.
“Ikiwa mtanichagua, tutawachoma walarushwa wote kwa vitendo. Mimi ni kiboko wa mafisadi ndiyo maana baada ya kuchaguliwa wengine wamekimbia chama,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema pia kwamba, nchi ni tajiri kwa sababu ina rasilimali nyingi yakiwamo mazao ya kahawa, pamba na korosho.
“Hii nchi ni tajiri sana, kila eneo ukigeuka ni fedha, lakini kuna watu wachache wamekuwa wakichota rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi na hawa nataka kushughulika nao,” alisema.
Akizungumzia mfumo wa stakabadhi ghalani, alisema anatambua changamoto wanazozipata wakulima wa zao la korosho.
Alisema anashangazwa na suala la wakulima wa zao hilo kuhangaika kudai fedha za mazao ambayo wameyalima wenyewe.
“Ninajua kuna changamoto zinazowakabili wakulima kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani. Haiwezekani mkulima wa korosho alime kisha anasotea malipo yake.
“Ninaomba kwa hili mniamini nitashughulika nalo, haiwezekani mkulima apate tabu kwa jasho lake.
“Ninaomba mniamini ndiyo maana nasema Serikali ya awamu ya tano nitakayoiunda, Waziri wa Kilimo ajiandae. Na pia nimejipanga kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne,” alisema.
Dk. Magufuli akiwa njiani kutokea wilayani Newala, alilazimika kusimamisha msafara wake katika Kijiji cha Lidumbe na kuhani msiba.