Na SAMWEL MWANGA, SIMIYU
RAIS Dk. Dk John,Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele cha mbio za
Mwenge kitaifa zitakazofanyika Oktoba 14, mwaka huu mkoani Simiyu.
Akizungumza na waandishi wahabari jana, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema tayari maandalizi ya kumpokea kiongozi huyo yamekamilika.
Alisema sherehe hizo zitatanguliwa na maadhimisho ya wiki ya vijana ambayo yatafunguliwa kesho na kufikia kilele Oktoba 14, mwaka huu.
Alisema katika sherehe zitahudhuriwa pia na Mama Maria Nyerere ambapo watashiriki misa ya maazimisho ya kumbukumbu ya miaka 17 ya
kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere itakayofanyikia katika Kanisa la Mtakatifu Yohana mjini Bariadi.
Alisema maadhimisho hayo, yatafunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama katika uwanja wa Sabasaba.
” Maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na kongamano la vijana litakaloendeshwa kwa siku tano kuanzia Oktoba 9, hadi Oktoba 13, mwaka huu katika kongamono hilo kutajadiliwa mada mbalimbali zinazoihusu jamii, ikiwamo kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi,” alisema.
“Kwa upande wa mkoa wetu vijana wetu wamejiandaa kuonesha shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanywa katika Halmashauri husika,”alisema.
Alisema katika wiki ya vijana kutakuwepo na zoezi la uchangiaji damu kwa hiari kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji hususan mama wajawazito, majeruhi wa ajali na watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano.
Alisema shughuli ya uchangiaji wa damu itasimamiwa na AGHAPH na Shirika la Msalaba Mwekundu.