24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wakesha shambani kumsubiri Waziri Mkuu

waziri-mkuuNA MWANDISHI WETU – KITETO

ZAIDI ya wakulima 100 wilayani Chemba, mkoani Dodoma wamepiga kambi shambani wakimsubiri Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu.

Wakulima hao walifikia hatua hiyo baada ya kusubiri utatuzi wa mgogoro huo unaohusisha mashamba na Hifadhi ya Makame (WMA), kudumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi.

Wakulima hao kutoka kata za Olboloti, Mrijo, Msaada na Jangalo walifika katika mashamba hayo yaliyopo Kijiji cha Kaachini wilayani Kiteto, wakiwa na vitendea kazi kama, majembe, mapanga na trekta.

Wakizungumza na MTANZANIA juzi, wakulima hao walisema wameshindwa kulima kwa miaka miwili mfululizo, kutokana na msuguano uliopo baina yao na wafugaji, huku Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ikidaiwa kuulea mgogoro huo.

Walisema, wamekuwa wakizuiwa kulima kwa madai kuwa wamevamia eneo hilo linalodaiwa kuwa ni hifadhi, huku wakipinga madai hayo na kueleza kuwa wao wanamiliki mashamba hayo kihalali.

“Tunamtaka Waziri Mkuu, kwani tumechoshwa na ahadi zisizokuwa na utekelezaji kutoka kwa viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa ambao wanaonekana kushindwa kutatua mgogoro huo unaoleta uhasama baina yetu na wafugaji.

“Miaka miwili sasa imekatika hakuna ufumbuzi wowote, tuliambiwa wakuu wa Wilaya za Chemba na Kiteto wanakutana hakuna majibu, mara tukaambiwa wakuu wa mikoa wanakutana nao wakaenda jumla,” alisema mmoja wa wakulima hao, Said Kibinda.

“Mwanzoni mwa mwaka jana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunda tume ambayo ilikuja kuhakiki mipaka, walimaliza kazi na ripoti iliwasilishwa, lakini hadi leo wananchi wanasubiri majibu hatujapewa.

“Sasa tumeamua kuja mashambani mwetu, tutalala huku maporini hadi Waziri Mkuu Majaliwa aje asikilize kilio chetu, tuna imani naye,” alisema Kibinda.

Alisema pamoja na kufanya jitihada za kuwasilisha nyaraka katika ofisi za serikali kuonesha uhalali wa umiliki wa maeneo hayo, lakini wameonekana kupuuzwa.

Kwa upande wake Logo Hila (58) alisema, hayuko tayari kuondoka kwenye eneo hilo kwa kuwa uvumilivu wa kusubiri maamuzi ya Serikali kwa miaka miwili mfululizo bila mafanikio umemshinda.

“Mimi nimeathirika kiuchumi kutokana na mgogoro huu, nilikopa trekta Suma JKT hadi sasa nimeshindwa kulipa marejesho kwa mtindo huu sisi wakulima mbona tunanyanyasika sana?,” alihoji.

Kwa upande wake Shabani Maslahi, alisema njia pekee ya kumaliza mgogoro huo ni viongozi kupitia mikataba ya umiliki wa mashamba baina ya wakulima na vijiji pamoja na kuangalia historia ya hifadhi hiyo.

“Wakati hifadhi hiyo inaanzishwa watu walikuwepo aidha yalikua ni makazi au ni mashamba lakini watu walikuwepo. Sasa kusema tu eneo hili ni hifadhi bila kuangalia haki za watu siyo sahihi na wala hii si haki,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto (DC), Tumaini Magessa, alisema suala hilo liko mezani kwake na kwamba jitihada zinafanyika kuhakikisha wananchi hao wanapata majibu juu ya mgogoro huo.

“Hakuna sababu ya wananchi wale kushindana na Serikali, kumbuka eneo hilo limesajiliwa kuwa Hifadhi ya WMA, tuangalie tu haki kwa maana ya wao walipataje maeneo hayo na serikali tutaona namna ya kuwasaidia,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles