NORA DAMIAN– KASULU
MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ameeleza siri ya uteuzi wa mawaziri watatu kutoka mkoani Kigoma.
Akizungumza jana, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Kiganamo, Dk. Magufuli alisema
alipoingia madarakani miaka mitano iliyopita, alikuwa na changamoto kubwa ya kuuinua Mkoa wa Kigoma hatua iliyomlazimu kuwateua katika nafasi za ubunge, kisha kuwapa uwaziri, Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia), Dk. Philip Mpango (Fedha na Mipango) na Atashasta Nditiye (Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).
“Nilifanya makusudi kuubadilisha Mkoa wa Kigoma, nikajiuliza nitafanyaje kuleta mapinduzi ya kweli.
“Mpago hakuwa mbunge, lakini mtaalamu wa fedha, nikapanga nikapangua, nikamteua kuwa mbunge, lengo akasimamie miradi ya Tanzania, lakini ni miradi ya Mkoa wa Kigoma, fedha zitakazokuwa zinapatikana asisahau Kigoma.
“Ningeweza nikachagua waziri yeyote kutoka mahali popote, mheshimiwa Mpango amefanya mambo makubwa.
“Nikamchukua Ndalichako ili ashughulikie suala la elimu, mniletee huyu mama ni mchapakazi, amenisaidia katika kutoa elimu bure kwa Watanzania wote, naomba mumpe kura nyingi.
“Nikamteua Nditiye ili asimamie ujenzi, ni mara chache kuchagua mawaziri watatu katika mkoa mmoja, nilifanya hivyo kutengeneza mipango maalumu ya kusaidia mkoa ambao ulikuwa umesahaulika,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema amejipanga kuendelea kuuinua mkoa huo ili uwe na maendeleo ya kweli.
Dk. Magufuli alisema ana mpango kabambe wa uendelezaji miundombinu ya usafiri wa barabara kwa kuziunganisha na nchi jirani ili kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara.
Nchi hizo ni Sudani Kusini, Uganda, Malawi, Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini.
“Tulianza na kilomita 50 kutoka mpakani mwa Biharamulo na Nyakanazi kuja Kakonko, kilometa zote kuna mkandarasi na tumeongeza 68 za kwenda Manyovu.
“Mipango iliyopo ni kuendelea kuipanua ili magari yanayotoka kusini mwa Sudan yapite Uganda, yapitie Mtukula, Biharamulo, Kakonko, Kasulu, Kigoma, Uvinza.
“Waende Mpanda, Sumbawanga, Tunduma, Mwanza, Zimbabwe, Afrika Kusini…kwahiyo barabara hii si ya taifa tu ni barabara ya kimataifa,” alisema Dk. Magufuli.
Alisema pia wametumia zaidi ya Sh bilioni 400 kwa ujenzi wa barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami katika mkoa huo ikiwemo barabara ya Nyakanazi – Manyovu inayoendelea kujengwa.
“Kigoma ulikuwa kama umetengwa, ulikuwa mkoa wenye shida, barabara zilikuwa mbovu, ulibaki kama uliotenganishwa na mikoa mingine.
“Umeme umeanza kuingia, mitandao inapatikana, lakini pia tunaendelea kutoa elimu bila malipo, sasa tunataka mtu anayetaka kusafiri kwa barabara kwenda Burundi asikanyage vumbi, apite kwenye lami, mtu anayetoka hapa kwenda Tabora, Dar es Salaam, Mwanza asikanyage vumbi,” alisema Dk. Magufuli.
KERO ZA WANANCHI
Dk. Magufuli aliiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kigoma kumfuatilia mkandarasi anayejenga mradi wa REA wenye thamani ya Sh bilioni 24 ambao ulianza tangu Mei 18, mwaka huu na ulitarajiwa kukamilika Oktoba.
“Mkandarasi aitwe na kamati ya ulinzi na usalama, hawezi akapewa fedha halafu acheleweshe mradi, nina uhakika huyu mkandarasi amenielewa,” alisema Dk. Magufuli.
Aliahidi pia kutatua mgogoro wa wachimbaji wadogo wa madini ya chokaa na wakala wa misitu, mgogoro wa mpaka kati ya wananchi na JKT 825 na mgogoro wa wakulima na wafugaji kutokana na kukosekana kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Alisema pia kwa Wilaya ya Kasulu, itajengwa barabara ya kilometa tano kwa kiwango cha lami na kuwekwa taa za barabarani.
“Ujambazi, utekaji bado mambo hayajaisha, ni matumaini yangu nikipewa tena miaka mitano nitafanya mambo makubwa zaidi.
“Tunaomba tena miaka mitano tukaendelee kuwa watumishi wenu katika nchi hii, msidanganywe, tushikamane kama taifa moja, tulinde amani na usalama wa taifa letu, nchi jirani zinapata shida kwa sababu hazikulinda usalama na amani,” alisema Dk. Magufuli.
Mgombea ubunge Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Ndalichako, alimuomba Dk. Magufuli kuwasaidia kuendeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Manyovu na changamoto ya uhaba wa maji.
“Changamoto nyingine tuliyonayo, maji bado hayatoshelezi, yanatoka kama matope, ni machafu sana, tuko kwenye mradi wa miji 22 inayofadhiliwa na Serikali ya India, tunaomba mradi uharakishwe,” alisema Profesa Ndalichako.