Na Sheila  Katikula, Mwanza
Mafundi umeme wametakiwa kujisajili  na kupewa  leseni na Mamlaka ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji  (EWURA) ili kuzuia  ajali za moto zinazosababisha vifo na uhalibifu wa  mali sanjari na kuepuka vishoka.
Akizungumza na www.mtanzania.co.tz , Meneja wa Mamlaka  ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) Kanda ya Ziwa, George Mhina,  alisema lengo la utoaji wa leseni  za kuunganishia  mifumo ya umeme  kwa mafundi hao  itasaidia kila mtu kufikiwa na nishati hiyo kwa uhakikika na usalama.
Alisema hadi sasa zaidi ya mafundi 3,500 wamesajiliwa kwa nchi nzima na kupewa leseni ili waweze kufanya kazi kwa uhakika kwani kufanya kazi bila leseni ni kosa na adhabu zitachukuliwa ikiwemo  kifungo cha miaka mitano au faini isiyozidi sh milioni 10 au adhabu zote mbili kwa pamoja.
“Maombi ya leseni  hufanywa  mtandaoni kupitia mfumo wa Lois  katika tovuti ya mamlaka  hiyo  zinatolewa  kulingana na sifa  za mwombaji ambapo daraja A ni fundi mwenye uwezo wa kufanya kazi  zote za ufungaji na usambazaji umeme, daraja B  ufungaji umeme msongo wa  kati  hadi  volti 33,000.
“Kwa daraja C fundi anakuwa na leseni ya ufungaji umeme  usiozidi  volti 400, na mwombaji anapaswa  kuwa na nakala ya picha ya rangi ya bluu  (pasipoti), kuambatanisha Wasifu (CV)na nakala ya  vyeti vya elimu ya ufungaji  umeme  hati ya kusafiria, kitambulisho cha taifa,” alisema.
Hata hivyo Mbina amewataka wananchi kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kukagua nyaya za umeme kwenye nyumba zao ili kuweza kubaini kama zimechubuka  na kuzibadilisha  ili kuepuka majanga ya moto.Â
“Hivi karibuni tumeshuhudia shule zikiungua na kusababisha  vifo na mali kuteketea, sheria inasema  kila baada ya mwaka  mmoja unapaswa kuangalia nyaya kama zipo vizuri kwenye nyumba na kumbi za starehe na kwenye shule kila baada ya miaka mitano.
“Kwa viwandani kila baada ya miaka mitatu inashauriwa zoezi hilo ili kuepuka na changamoto hiyo ni vema kuweka utaratibu wa kukagua nyaya kama sheria zinavyosema,” alisema Mhina.
Mhina alisema kwa mjibu wa kanuni zilizowekwa na mamlaka hiyo wananchi hawapaswi kuwapa kazi ya kufunga umeme kwenye nyumba zao na viwanda kwa mafundi ambao hawana leseni ya mamlaka hiyo.