30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif kugombea urais?

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

JINA la Maalim Seif Sharrif Hamad lina rekodi ya kipekee katika siasa za Tanzania uchaguzi mkuu.

Rekodi hizo zinatokana na harakati za kisiasa za kiongozi huyo ambazo zimekuwa za ‘mshike mshike’ mara kwa mara.

Mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu watu mbalimbali na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakisema huenda kiongozi huyo akajitokeza kugombea tena urais.

Pengine utabiri huo unatokana na harakati zake za kugombea nafasi hiyo kwani tayari amegombea mara tano urais wa Zanzibar.

Maalim Seif aligombea urais wa Zanzibar katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 na iwapo mwaka huu atapitishwa itakuwa ni mara ya sita.

Nguli huyo wa siasa ambaye kwa sasa yuko Chama cha ACT – Wazalendo, anatajwa kuwa ni mwanasiasa aliyegombea urais wa Zanzibar mara nyingi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini.

SAFARI YA KUGOMBEA URAIS

Safari ya Maalim Seif kugombea urais ilianza mwaka 1995 alipopambana na mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour.

Kulingana na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), katika matokeo ya urais mwaka 1995, Salmin Amour, alishinda kwa asilimia 50.24 dhidi ya 49.76 alizopata Maalim Seif. Hata hivyo, CUF ilitangaza kutoutambua ushindi huo.

Mwaka 2000, Seif aliingia ulingoni kupambana na Amani Abeid Karume, mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume. Kwa mara nyingine, matokeo ya ZEC yalionyesha Seif aliangushwa baada ya kujikusanyia asilimia 32.96 ya kura dhidi ya asilimia 67.04 alizopata Amani Karume. Uchaguzi wa mwaka 2000, alipata asilimia chache (32.96).

Uchaguzi wa mwaka 2005, CUF walimteua Maalim Seif kupambana tena na Amani Abeid Karume wa CCM. Uchaguzi huo ulipokamilika, ZEC ilimtangaza Amani Abeid Karume kuwa mshindi baada kujikusanyia asilimia 53.18, huku Maalim Seif akijipatia asilimia 46.07 ya kura zote.

Hata hivyo waangalizi wa kimataifa walisema uchaguzi huo haukuwa huru na haki. Taarifa ya waangalizi wa Jumuiya ya Madola walisema palikuwa na kasoro nyingi na uhaba wa uhuru miongoni mwa wapigakura na wagombea. CUF ilipinga matokeo hayo.

Maalim Seif alirudi tena kwenye kinyang’anyiro cha mwaka 2010 akiwakilisha CUF dhidi ya Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM. Baada ya uchaguzi wa Oktoba 31, 2010, ZEC ilimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar kwa kupata asilimia 50.1 dhidi ya 49.1 za Seif.

Kutokana na makubaliano ya vyama hivyo kumaliza mgogoro wa muda mrefu visiwani humo, Maalim Seif alitakiwa kuwa sehemu ya serikali ambapo aliteuliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, huku Balozi Seif Ali Iddi akiwa makamu wa pili wa Rais.

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2015 yalifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Mwenyekiti wake Jecha Salum Jecha. ZEC ilitangaza pia uchaguzi wa marudio utafanywa Machi 20, mwaka uliofuata.

Licha ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, Maalim Seif aliitisha mkutano wa waandishi wa habari Oktoba, 2015 na kusema yeye ndiye mshindi wa kiti cha urais Zanzibar na alikataa kushiriki uchaguzi wowote wa marudio.

MUDA UTAONGEA

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, iwapo atagombea urais katika Uchaguzi Mkuu, Maalim Seif hakukubali wala kukataa badala yake alisema kuwania urais si uamuzi wake binafsi bali unatokana na uamuzi wa wanachama kwa hiyo siku ikifika ukweli utawekwa wazi.

Maalim Seif anasema suala la kugombea si la kuamua tu, lazima wewe mwenyewe ujipime na kujitathmini je, una uwezo au huna uwezo? Lakini huishii hapo.

“Jambo la pili, si uamuzi wako hata kama unajiona una uwezo, una wanachama wenzako, hasa viongozi wa chama, lazima mkae mshauriane, kwamba katika mazingira ya 2020 mgombea anayetufaa ni fulani, hilo la pili.

“Jambo la tatu ni maoni ya wananchi wenyewe, wanasemaje je, Maalim aendelee au siendelee, kwa hiyo mimi mpaka sasa hivi bado sijakata shauri kwamba niendelee ama nisiendelee itategemea mazingira hayo niliyoyataja,” anasema.

Maalim anasisitiza katika maoni yanayotolewa na wanachama kuhusu hata kiongozi wa juu ni dhihirisho la Uhuru uliopo ndani ya Chama cha ACT Wazalendo mwanachama yeyote hata yule wa ngazi ya chini kabisa anaweza kutoa maoni kwa uhuru bila woga.

Anasema hana wasiwasi wala hakati tamaa kwa kuwa Zanzibar wameiondoa CCM mara mbili chini ya uongozi wake kwa hiyo ana uhakika CCM inaweza kung’oka hata upande wa Tanzania Bara.

Anasema alipokuwa CUF kila mwaka wa uchaguzi wamekuwa wakiongeza kura na kura za CCM zimekuwa zikipungua na kwamba huenda watawala ndiyo hawaridhiki kutokana na sera yao ya mamlaka kamili na hilo ni suala lililopo kwenye mkataba wa Muungano unaoweka wazi kuwepo kwa mamlaka tatu.

Maalim anasema anaamini katika mashirikiano ya vyama vya siasa katika kuiondioa CCM madarakani, suala ambalo tayari Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wameshaweka wazi, lakini pia anaamini kuwa kuna umuhimu wa maridhiano ya kisiasa ili kulifanya Taifa liondoke kwenye mkwamo wa kisiasa uliopo kwa sasa.

Hata hivyo, wafuasi wa Maalim Seif wanaamini kuwa kiongozi huyo ana uwezo wa kuongoza Zanzibar na mategemeo hayo ndiyo chanzo cha Maalim Seif kuwa jabali la kisiasa visiwani Zanzibar hadi leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles