23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 10, 2022

Chaguzi zitakazotazamwa Afrika 2020

FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MWAKA 2020 umesheheni matukio makubwa ya kisiasa kwani mataifa mengi barani Afrika yanatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu ikiwamo Tanzania ili kumpata rais, wabunge na madiwani.

Makala haya yanaangazia chaguzi za Afrika ambazo zinatarajiwa kufanyika mwaka huu huku zikitazamwa zaidi kutokana na viongozi walioko madarakani hivi sasa.

TANZANIA

Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa kumchagua rais, wabunge na madiwani Oktoba mwaka huu, ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatarajiwa kutazamwa zaidi si tu Afrika bali na dunia nzima.

Katika uchaguzi huo Rais wa sasa, Dk. John Magufuli, kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM) anatarajiwa kuwania tena muhula wa pili kama ambavyo imezoeleka kwa miaka mingi nchini kwa rais kuongoza kwa awamu mbili.

Hata hivyo kama ilivyo ada Rais Magufuli anatarajia kukumbana na upinzani kutoka kwenye vyama vya upinzani vyenye nguvu nchini ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) ambacho ni Chama Kikuu cha Upinzani, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha ACT – Wazalendo na vingine.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Rais Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 huku mpianzani wake, Edward Lowassa aliyegombea kupitia Ukawa akipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39,97 ya kura zote.

Hata hivyo tayari Lowassa amerejea kwenye chama chake cha CCM, huku akiwahimiza wananchi kuhakikisha kuwa wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa kile alichoeleza kuwa ni kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya kwa kipindi chake.

Hivyo hiyo inaongeza shahuku ya kutaka kujua zaidi iwapo vyama hivyo vya upinzani vitakuwa na mgombea mmoja tena au kila chama kitasimama chenyewe, hili ni jambo ambalo linaongeza mvuto zaidi katika uchaguzi huu.

Licha ya kuwapo kwa mageuzi makubwa mbayo yamefanywa na Rais Magufuli lakini upinzani umekuwa ukijinasibu kwa hoja zao ambazo wanaamini kuwa zinawafanya wastahili kuchukua kijiti hicho cha uongozi kwa mwaka 2020.

Hata hivyo, Richard Ngaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine na Mchambuzi wa Siasa na Utawala bora, alinukuliwa siku chache zilizopita akisema kuwa; “Siioni UKAWA ya mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu ujao, hasa kwa kuzingatia historia ya, Zitto Kabwe (Kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo) na Chadema, na wakati huu ambapo ACT-Wazalendo kilichochukua mtaji wa zamani wa chama cha CUF visiwani Zanzibar.

“Naona vyama binafsi vikisimama kila chama peke yake ama kuunda kambi mbili, moja ikiwa na Chadema na nyingine ya ACT-Wazalendo kama kiongozi huku chama tawala CCM kikipita kiurahisi hata bila kutumia nguvu ya vyombo vya dola.

Uchaguzi huo wa Tanzania pia utaenda sambamba na ule wa Zanziabar ambako Rais wa sasa, Dk. Ali Mohamed Shein, anatarajiwa kuhitimisha muhula wake.

BURUNDI

Kwa Afrika Mashariki Burundi pia inatarajia kufanya uchaguzi wake wa rais ambapo kiongozi wa sasa ni Pierre Nkurunziza.

Pamoja na kwamba Mei 17, mwaka 2018 wananchi wa nchi hiyo walipiga kura kuunga mkono marekebisho ya kariba mpya ambayo yangemwezesha kiongozi huyo kusalia madarakani hadi 2034, lakini Rais Nkurunziza wa chama tawala cha CNDD FDD, alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa hataombakuchaguliwa tena baada ya muhula wake wa sasa kumalizika mwaka huu.

Nkurunziza alitoa kauli hiyo wakati akiidhinisha katiba mpya ya nchi hiyo katika eneo la Bugendana, Gitega.

Aidha, inakadiriwa kuwa karibu watu nusu milioni wamekimbia tangu Nkurunziza ashinde muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi uliokuwa na ghasia wa mwaka 2015.

Hata hivyo Muungano wa vyama vya upinzani nchini humo umekuwa ukiweka ngumu kwa kiongozi huyo kuendelea kusalia madarakani ambapo katika uchaguzi wa mwaka 2015 vyama hivyo vya upinzani vilimaliza katika nafasi ya pili.

NCHI NYINGINE

Nchi nyingine zinazotarajia uchaguzi mwaka huu ni pamoja na Burkina Faso ambayo itafanya uchaguzi wa rais pamoja na wabunge Novemba.

Nyingine ni Cameroon inayotarajiwa kufanya uchaguzi wa wabunge, maseneti na serikali za mitaa uchaguzi ambao umekuwa ukisogezwa mbele kwa mara mbili mfululizo kwani awali ulikuwa ufanyike mwaka 2018.

Jamhuri ya Afrika ya kati nayo inatarajia kufanya uchaguzi wake mwaka huu wa kumpata rais, ikumbukwe kuwa kwa kipindi kirefu CAR imekuwa ikiandamwa na vita.

Nchi nyingine inayotarajiwa kufanya uchaguzi mwaka huu ni pamoja na Chad ambayo itafanya uchaguzi wa wabunge Februari uchaguzi ambao ulisogezwa mbele kutoka kufanyika mwaka 2019.

Visiwa vya Comoro pia vinatarajia kufanya uchaguzi wa wabunge, huku Misri ikitarajia kufanya uchaguzi wa wawakilishi Mei mwaka huu.

Kuna Ethiopia, Gabon na Ghana inayotarajia kufanya uchaguzi wa rais na wabunge Desemba mwaka huu, sambamba na Guinea ambayo nayo inafanya uchaguzi wa rais na wabunge.

Ivory Coast itafanya uchaguzi wa rais Oktoba mwaka huu, Mali itafanya uchaguzi wa wabunge Mei na Namibia ikitarajiwa kufanya Novemba.

Pia zimo Niger, Senegal, Somalia, Visiwa vya Ushelisheli, Sudan na Togo ambazo zote zitafanya uchaguzi mkuu wa rais mwaka huu.

Hizo ni baadhi ya chaguzi za Afrika ambazo zinatarajiwa kufanyika mwaka huu huku zikitazamwa zaidi kutokana na viongozi walioko madarakani hivi sasa.

Chaguzi hizo zitatazamwa zaidi kwani kwa nchi kama Ivory Coast tumeshuhudia namna ambavyo chaguzi zake zimekuwa zikileta mvutano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles