Na Amina Omari-Tanga
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amemsimamisha kazi Ofisa Ardhi Kanda ya Kaskazini, Thadeus Riziki, baada ya kuuza shamba la Amboni Estate lililopo Tanga kinyume na utaratibu
Uamuzi huo alitoa jana wakati wa mkutano wa Funguka kwa Waziri wa Ardhi, ambao una lengo la kusikiliza kero na kutatua migogoro ya ardhi kwa wananchi wa Jiji la Tanga uliofanyika katika viwanja vya Tangamano.
Alisema ofisa huyo wakati akiwa na cheo cha Ofisa Ardhi wa Jiji la Tanga, aliuza shamba la Amboni kwa mwekezaji ilhali sheria ilielekeza shamba hilo liwekwe katika utaratibu wa kufutiwa hati na Rais.
“Nimeamua kumsimamisha kazi ofisa huyu ambaye nasikia hivi juzi amepandishwa na kuwa Ofisa Kanda kutokana na kubariki mauziano ya shamba ambalo lilitakiwa kufutwa,” alisema Lukuvi.
Hata hivyo Waziri alitumia fursa hiyo kuiagiza Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha shamba hilo linarudi mikononi mwa serikali kwa ajili ya kuanza taratibu za kulifutia hati.
“Lakini yule mwekezaji mkamfanyie tathmini ya mali zake zisizohamishika mjue ametumia ekari ngapi pamoja na wananchi walioko muwafanyie uthamini kwa gharama zenu bila ya kuwabughudhi kwani haya makosa mliyafanya wenyewe,” alisema.
Hata hivyo aliwataka watendaji wa jiji hilo kuhakikisha wanasimamia sheria na taratibu za ardhi kama zinavyoelekeza badala ya kuendelea kufanya kazi kwa malalamiko bila ya kuchukua hatua stahiki.
“Tanga Jiji mna maeneo mengi ya mashamba ambayo yameshindwa kuendelezwa lakini sijui kwa nini mmekuwa wagumu kufuta mashamba hayo Rais Magufuli aweze kuridhia na kuyagawa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo,” alisema Lukuvi.
Wakati akisikiliza kero za migogoro ya ardhi inaonyesha kesi nyingi zinatokana na wananchi wengi kuchukua fidia wakiwa hawajui thamani ya maeneo yao.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa aliwataka wakazi wa jiji hilo kuwasilisha kezo zao za ardhi kwa waziri huyo kwa sababu alikuwapo kwa ajili ya kuhakikisha anatatua migogoro iliyopo.