Mwandishi Wetu, Monduli
Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, amesema amerejea nyumbani Chama Cha Mapinduzi (CCM), na si kwa jirani huku akitaka kura milioni sita alizopigiwa mwaka 2015 alipogombea urais apewe Rais John Magufuli, mwaka 2020.
Lowassa amesema hayo leo Jumamosi Machi 9, Monduli mkoani Manyara, katika mkutano wa kumpokea baada ya kurejea CCM akitokea Chadema alikohamia mwaka 2015.
“Nimekuja kueleza kwanini nimerudi nyumbani jibu lake ni rahisi tu, nimerudi nyumbani, nimerudi nyumbani basi sijarudi kwa jirani wala kwa mtu nimerudi nyumbani kwangu.
“Niligombea urais kwenye uchaguzi uliopita nilipata kura nyingi, milioni sita. Lakini sasa nawaomba Watanzania wote ambao kwa upendo wao walinipa kura hizo wazielekeze kwa Rais Dk. Magufuli.
“Tumuunge mkono ili apate nguvu ya kuliongoza taifa letu aweze kuendelea na kazi zake, tushirikane tusaidiane,” amesema Lowassa.
Pamoja na mambo mengine, Lowassa aliwashukuru viongozi na wanachama wa Chadema akisema; “kwa Chadema nawaambia ahsanteni sana viongozi na wanachama, asanteni nawashukuru sana, sina zaidi, msiniwekee maneno mdomoni, asanteni nawashukuru sana”.