Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu Chadema amefanyiwa upasuaji mara ya pili katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Mkuu wa Idara ya Uenezi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hemedy Ally amesema tangu alipoingizwa katika chumba cha upasuaji saa nne asubuhi leo Septemba 8, hadi saa tisa alasiri alikuwa hajatoka lakini madaktari wamesema upasuaji huo unaendelea vizuri.
“Tangu jana alipofika alifanyiwa ‘stabilization’ ili aweze kukabiliana na upasuaji na zoezi hilo lilifanikiwa vizuri na madaktari wametueleza kuwa hakuna hali yoyote ya hatari na matibabu yake yanaendelea kwa mafanikio,” amesema.
Lissu aliwasili jijini Nairobi jana saa saba usiku akitokea mjini Dodoma katika Hospitali ya Mkoa ambako alipokelewa na timu ya madaktari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na kuanza kumtibu katika gari ya wagonjwa (Ambulance).
Wakati huo huo, balozi mbalimbali nchini ikiwamo Ubalozi wa Marekani na Umoja wa Nchi za Ulaya na taasisi za kitaifa na kimataifa zimeendelea kutuma salam za pole kwa Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ambapo pamoja na mambo mengine wamelaani tukio hilo na kuitaka polisi kuchukua hatua
Lissu alipigwa risasi jana nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma wakati akitokea katika kikao cha Bunge cha mchana.