Na BAKARI KIMWANGA,
SASA unatimia mwaka mmoja huku tukikumbuka kwa sauti na kivuli chako kaka Deo Filikunjombe.
Haikuwa rahisi na haitatokea kuwa hivyo kwani kila wakati ndugu, jamaa na marafiki zako huona bado tuko nawe lakini hujikuta tukibubujikwa na machozi hasa baada ya kutwaliwa kwako na muumba wetu baba wa mbinguni.
Ninapata tabu kila wakati pindi ninapovuta hisia na hata ninapokuwa bungeni mjini Dodoma au ninapokuwa ofisini kwako na pale ninapowaona wasaidizi wako hujikuta nikihisi kuwa umetoka na utarejea baada ya muda.
Duh! Kadiri ya muda unavyokwenda ndipo hujikuta nikisadiki kuwa kaka Filikunjombe haupo nasi katika ulimwengu huu.
Oktoba 15, mwaka huu unatimiza mwaka mmoja tangu ile  siku nzito katika nchi yetu na hasa kwa wapiga kura wa Ludewa walipompoteza mwakilishi wao Filikunjombe ambaye alifariki dunia kwa ajali ya helikopta katika Pori la akiba la Selous mkoani Morogoro.
Safari ya kisiasa ya Filikunjombe ilianza mwaka 2005, ambapo alitupa kete jimboni kuwania ubunge kwenye kura za maoni lakini haikuwa bahati yake na ilipofika mwaka 2010, alifanikiwa kufuzu mtihani wa kura za maoni ndani ya chama na hata alipotoka nje aliweza kuchaguliwa na wananchi wa Ludewa kuwa mbunge wao kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Matumaini makubwa ya wana Ludewa kwa marehemu Filikunjombe yaliimarika zaidi siku hadi siku kutokana na moyo wa huruma na upendo aliokuwa nao hasa katika kuwatumikia wananchi wake kwa hali na mali kuboresha maisha yao.
Marehemu Filikunjombe aliyeendelea kung’ara kwa wananchi wake hasa kutokana na misimamo yake ya kuboresha maendeleo mbalimbali ya wananchi,  ambapo katika kipindi chake cha kwanza cha ubunge  wake kuanzia 2010/2015 alikuwa ni nuru pekee kwa wananchi wa Ludewa na Taifa kwa ujumla kufanikisha yale aliyoyaamini.
Oktoba 4, mwaka jana Filikunjombe alianza kutumia usafiri wa helikopta namba 5Y-DKK Â katika mikutano yake ya kampeni kwa ajili ya kuomba kura kwa wananchi ikiwa ni dhamira yake ya kurejea tena bungeni kuendelea na kazi ya kuwatumikia wananchi wake na Taifa kwa awamu nyingine ya pili yaani mwaka 2015/2020.
Wakati wote alimaliza mikutano yake ya kampeni salama akiwa na afya njema Oktoba 12 mwaka 2015 na ilipofika Oktoba 13 aliagana na wananchi wa Ludewa katika hali ya upendo mkubwa akisema anaelekea Dar es Salaam na atarejea tena baada ya siku tatu kuhitimisha mikutano yake ya lala salama ya kufunga kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
Lakini kumbe wakati wote huo kumbe ndiyo ulikuwa ni mwanzo na mwisho wa kuagana na wananchi wake moja kwa moja katika hali ya simanzi.
Na ilipofika Oktoba 15, mwaka 2015 saa 11 jioni Filikunjombe, alianza safari ya kurejea jimboni kwake Ludewa akitokea jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa ameambatana na wasaidizi wake Casablanca Haule, Egid Nkwera pamoja na rubani wa helikopta hiyo Kapteni William Silaa.
Hata hivyo ilipotimu saa 2 usiku taarifa zikabadilika huku wengi wakihoji alipo Filikunjombe na wengine kupitia mitandao ya kijamii wakisema kuwa amepata ajali na huenda amefariki dunia.
Wengi walijipa moyo kwa kuwa ni usiku acha kupambazuke tupate ukweli wa ajali hiyo na ilipofika saa 4 asubuhi vyombo vya usalama vilitangaza kifo cha Filikunjombe pamoja na watu wote waliokuwa kwenye helikopta hiyo.
Namna kifo kilivyokatisha uhai wake
Deo Filikunjombe alikuwa ni  miongoni mwa watu wanne waliothibitika kufariki katika ajali ya helikopta iliyoanguka usiku katika Pori la akiba la Selous.
Taarifa zilizotolewa na Meneja wa Selous, Benson Kibonde, Â kwa wakati huo zlisema helikopta hiyo ilianguka karibu na Mto Ruaha, katika Kitalu cha Uwindaji cha R3.
Alisema taarifa za ajali hiyo walizipata kwa njia ya satellite kutoka kwa mwindaji mmoja ambaye akiwa katika hema lake ndani ya Pori la Selous katika Kitalu cha R2, alisikia kishindo cha helikopta ikianguka na kuona moshi upande wa Kitalu cha R3.
Uchunguzi gizani
Licha ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kuthibitisha ajali ya chopa hiyo aina ya AS-35.
Chopa iliyopata ajali ilikuwa na namba ya usajili 5Y-DKK, mali ya Kampuni ya General Aviation Service ya jijini Dar es Salaam.
Helikopta hiyo iliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) saa 9:57 jioni na ilitarajiwa kufika Njombe saa 12:20 jioni Oktoba 15, mwaka jana .
TCAA ilisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika na kwamba wataalamu wa uchunguzi wa ajali za ndege wanaendelea na uchunguzi ingawa sasa ni mwaka mmoja unatimia bila kujua chanzo cha ajali hiyo ni nini.
Taifa linatafakari na kukosa majibu Je, kifo cha Filikunjombe kilipangwa? Je, uchunguzi umeshindwa kubaini chanzo? Au Filikunjombe alitunguliwa na majangili? Haya ni maswali yalikosa majibu hadi sasa.
Ya kukumbukwa kwa Filikunjombe
Marehemu Deo Filikunjombe alikuwa miongoni mwa wabunge vijana wenye misimamo thabiti isiyoyumbishwa.
Aina ya siasa aliyoiendesha ilivutia wengi, pamoja na kuwa mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini kwa msimamo wake alidiriki hata kukikosoa chama chake hadharani na hakusita kuweka wazi msimamo wake kwa kuangalia maslahi ya nchi.
Umahiri wake wa kusimamia ukweli ulimpa fursa kubwa ndani ya Kamati ya PAC, ambayo aliiongoza kama Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Marehemu Deo Filikunjombe amefanya mambo mengi na yenye historia ya aina yake.
Sakata la Escrow
Aliitumia vizuri nafasi yake PAC kuandaa na kuiwasilisha ripoti nzima ya sakata la ukwapuaji wa Sh. bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT).
Ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa mwishoni mwa mwaka jana, iliitikisa nchi kwa kufichua miamala iliyotumiwa kuchota fedha hizo, pia iliainisha majina ya wahusika.
Madudu ndani ya mashirika ya umma
Kutokana na uwezo mkubwa wa kusimamia ukweli pasipo kutetereka, Marehemu Filikunjombe kwa kushirikiana na timu nzima ya kamati ya PAC kwa pamoja waliweza kubaini ufisadi katika mashirika mbalimbali ya Serikali, kama vile madudu yaliyobainika ndani ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Benki ya NBC.
Maendeleo Ludewa
Katika kipindi cha miaka mitano ya ubunge wa Jimbo la Ludewa, Marehemu Filikunjombe alifanikiwa kuchochea maendeleo ya jamii katika jimbo lake.
Kwa picha iliyokuwa wazi marehemu alitazamiwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Msimamo wake
Wakati wa sakata la kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kumng’oa madarakani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Marehemu Filikunjombe hakuonyesha woga, alisimama mbele na kumnyooshea kidole Waziri Mkuu na kumwambia bayana kuwa anatetereka kuliongoza Baraza la Mawaziri.
Katika moja ya michango yake kwa mijadala ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Filikunjombe aliitaka Serikali kuchukua hoja za wapinzani na kuzifanyia kazi, jambo lililomkera Pinda.
Mawaziri wachapwe viboko
Filikunjombe pia aliwahi kuliomba Bunge kubadilisha kanuni ili aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhandisi Christopher Chiza, achapwe viboko bungeni.
Huku akiomba mwongozo kwa Spika Anne Makinda, Filikunjombe alisema kanuni hiyo iruhusu mawaziri wote wanaoshindwa kujibu maswali ya wabunge kwa ufasaha, wachapwe viboko na kutolea mfano wa Waziri Chiza kwamba, alipaswa kuchapwa viboko kwa kushindwa kujibu swali la Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM).
0715 Â 247327