23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania itajengwa na wenye uchu wa maendeleo

Watanzania waishio Sweden wakiwa katika hafla iliyofanyikanchini humo.
Watanzania waishio Sweden wakiwa katika hafla iliyofanyikanchini humo.

HAKUNA  kitu kinachonifurahisha kama kuona mtu ambaye unamheshimu sana na kumthamini, kupata heshima mbele ya raia na wafanyakazi wenzake. Nilifurahi sana kusoma kwa Balozi Dorah Msechu, Balozi wa Tanzania nchini Sweden na nchi za Ulaya Kaskazini kupongezwa kwa jitihada zake kwenye kituo chake cha kazi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Ukweli ni kwamba Balozi huyu pamoja na maofisa wenzake wametoa msaada mkubwa sana kwenye jumuiya yetu ya Watanzania ya Ulaya Kaskazini, kazi walizoanzisha wenzake, mabalozi waliotangulia ameweza kuzisimamia kwa moyo mmoja.

Viongozi waliopatikana katika michakato tofauti kushirikiana na ubalozi imetuwezesha kufikia katika hali nzuri. Baadhi ya Watanzania sasa wana hamu na wana uwezo wa kuchangia, kujenga na kuongoza jumuiya yetu Ughaibuni.

Msaada mkubwa sana umetoka kwenda kwa timu yetu ya Mpira wa Miguu Ughaibuni FC. Kilimanjaro ambayo sasa imepanda daraja mpaka kwenye daraja la 6. Hawa vijana wamefanikiwa sana kutangaza Tanzania na bila mwongozo, msimamo mzuri, ushauri na ushirikiano kutoka ubalozi wetu mafanikio yangepatikana lakini kwa shida sana. Kwa kutambua kwamba FC Kilimanjaro inatangaza Tanzania kupitia mpira wa miguu.

Tunashukuru sana kwa kutambua kwamba Balozi amefanya kazi nzuri sana ya kuwatafutia makazi watumishi ubalozini, lakini pia isisahaulike mchango wake mkubwa kwenye kuhamasisha Watanzania kuendelea kujipanga.

Kazi wanazofanya Balozi zetu na ubalozi nyingi huwa hazionekani kwa Watanzania wengi na ndugu zetu vijijini. Lakini hakuna kazi kubwa kama kujenga uhusiano mzuri kati ya nchi yetu na ambazo mabalozi wanamwakilisha Rais.

Haya mawasiliano ndiyo yanayofungua milango ya ushirikiano katika ngazi tofauti za jumuiya. Katika kuimarishwa uhusiano huu basi nao unaleta na kufungua milango na fursa nyingi kwa sisi ambao tunaishi Ughaibuni kuweza kudandia hilo treni la uwekezaji endelevu.

Tukumbuke msemo maarufu kwamba ’mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe na mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe. Sisi Wanaughaibuni tuna Tanzania inajengwa na wenye upendo na uchu wa kuona nchi inasonga mbele.

Hii pia itaonekana hata nje ya Tanzania. Muda huu ni vigumu kuendelea mbele bila ya watu kufunga mikanda na kuhakikisha wanamuunga mkono Rais wetu John Magufuli katika jitihahad zaek za kuijenga nchi.

Sisi wanaUghaibuni ahadi yetu kwa Rais ni kumuunga mkono kwa kila hali katika jitihada zake za kuhakikisha jasho la wakulima na wafanyakazi wanyonge halipotei bure, ni jukumu letu usiku na mchana kuona kwamba tunaijenga nchi yetu.

Kama alivyosema Rais, wapo mabalozi wanaofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanamwakilisha  vyema Raia lakini pia wapo pengine wasiotimiza wajibu wao kama wawakilishi wa Rais na hao nadhani katika awamu hii hawatakuwa na nafasi kamwe.

Wito wetu sisi WanaUghaibuni kila siku tumekuwa tukisisitiza nchi mama yetu ni mbele kuliko kitu chochote na bila kufuata itikadi za kisiasa tunamuahidi Rais wetu kuwa naye bega kwa bega kumuunga mkono katika jitihada zake na Inshallah Mwenye Mungu atalifikisha Taifa letu kule linapotakiwa kwenda.

Wanaughaibuni tunatoa wito kwa wanasiasa, wasijaribu kuichezea amani iliyopo nchini kwetu kwani amani hii haikujengwa kwa siku moja. Ni rahisi sana kwa siku moja kuivunja amani ya nchi lakini itakuwa ni ngumu kweli kweli kuirejesha hiyo tunu ya amani.

Wenzenu huku Ughaibuni tunajivunia Kisiwa cha amani ya nchi yetu na unaposikia vipo viashiria mbalimbali vya kuivuruga amani tunachanganyikiwa kweli. Tunawategemea sana katika hili ili kuona watoto na wajukuu zetu hawatulaumu.

Sisi wanaUghaibuni tunachukua fursa hii kuviomba vyombo vya habari kuhakikisha vinatumia kalamu zao kuimarisha ustawi na umoja wa Taifa letu pamoja na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Lakini pia vyombo vya habari tunawaomba kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanaibua maovu yote ya uonevu dhidi ya raia wasio na hatia yanayofanywa  na watendaji wa Serikali na watumishi wake ili hapo sasa waweze kumsaidia Rais.

Watumishi wa Serikali na katika mashirika ya umma nanyi msituangushe kama ambavyo mlizoea, fanyeni kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja na kujituma kweli kweli na kuacha udanganyifu katika kutunza mali za Taifa letu. Nchi hii ni yetu sote na tusikubali wajukuu zetu wafike kwenye makaburi yetu wakitulilia machozi ya damu huku wakiomboleza tumewaachia magofu badala ya nchi.

Rais Magufuli ameonyesha njia, sisi wanaUghaibuni kwa kushirikiana na mabalozi na watendaji katika ofisi za balozi zetu tutashirikiana naye kuhakikisha nchi inasonga mbele.

Mungu Ibariki Tanzania!

Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga..

Tengo Kilumanga Email: [email protected] Tel: +46705263303 Twitter: @tengo_k

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles