VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
KIBAIOLOJIA binadamu anapotembea kutoka eneo moja kwenda jingine hapaswi kuinama.
Lakini kuna baadhi ya watu hasa waliofika umri wa utu uzima huwa wanainama wakati wa kutembea.
Hali hiyo hutafsiriwa na wengi kwamba ni matatizo ya uzee. Hata hivyo, wataalamu wa tiba ya mifupa, ubongo na uti wa mgongo wanasema si kweli.
Wanasisitiza hali hiyo haihusiani kabisa na uzee kwani kimaumbile mtu hapaswi kuinama kabisa kulingana na jinsi alivyoumbwa, anapaswa kusimama hata akiwa mzee.
Wanasema hali hiyo inapojitokeza ni dalili za ugonjwa wa uti wa mgongo unaoitwa kitaalamu ‘Degenerative Spine Diseases’, mtu anapaswa kutibiwa haraka vinginevyo huishia kupata ulemavu.
Doroth alivyoanza kuugua
Doroth Rugaba ni mama wa watoto watano, mkazi wa Muleba, mkoani Kagera, alipatwa na ugonjwa huo sasa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Anasimulia jinsi alivyoanza kuugua: “Nilizaliwa nikiwa sina kasoro yoyote ile lakini miaka kadhaa iliyopita nikiwa naendelea na majukumu yangu ya kazi, nikiwa muuguzi nilianza kuhisi maumivu ya mgongo na magoti.
“Fani yangu ni muuguzi, mkunga, nilianza kazi mwaka 1967 mkoani Kigoma, kisha nikahamia wilayani Musoma, mwaka 1972.
“1975 niliamua kwenda kujiendeleza kimasomo katika Chuo cha Ndanda, mkoani Lindi, ikiwa ni miaka minane tangu nilipoanza kazi hiyo.
“Nilikwenda kusoma ukunga kwa miaka mitatu, nilipohitimu nilirejea kazini katika Hospitali ya Wilaya ya Musoma (wakati huo) nikiwa muuguzi, mkunga kamili.”
Anasema baadaye alihamishiwa Dodoma ambako alifanya kazi kwa miaka kadhaa kisha kuhamishiwa Ukerewe.
“Nilikuwa nahama hivyo kumfuata marehemu mume wangu John Rugaba, aliyekuwa mkufunzi mwandamizi katika vyuo maalumu vya viongozi wa chama na Serikali.
“Mume wangu alikuwa mchumi mbobevu, alifariki mwaka 1987 baada ya kuugua ugonjwa wa ‘typhoid’ na kuzidiwa akiwa likizo nyumbani kwao Biharamulo,” anasema.
Anaongeza: “Nilifanya kazi katika mikoa mbalimbali hadi mwaka 1998 nilipohamia Kagera katika Hospitali ya Mkoa na baadae Hospitali ya Kaigara, Wilaya ya Muleba.
“Nilipokuwa kazini nilikuwa nikiwahudumia zaidi nyakati za usiku kuliko mchana na asubuhi, kwa usiku mmoja nilikuwa nazalisha wanawake zaidi ya watano.
“Siwezi kukumbuka idadi ya wanawake niliowahi kuwazalisha, ni wengi. Namshukuru Mungu aliyeniwezesha kupambania uhai wa mama na mtoto kwa miaka yote, kwani hakuna mama wala mtoto aliyewahi kupoteza maisha mikononi mwangu au kupata ulemavu.”
Anasema kabla hajastaafu alianza kuhisi maumivu ya mgongo na magoti, awali yalikuwa si makali lakini kadiri miaka ilivyosonga mbele maumivu nayo yalizidi kuongezeka maradufu.
“Ilifika wakati nilipokuwa nikikaa chini na mtu aje kuniambia niinuke nilihisi kama ananionea kwani sikuweza, nilihisi maumivu makali, niliona ananitakia kufa mapema,” anasema.
Safari ya matibabu
Anasema alihangaika kutafuta matibabu dhidi ya tatizo hilo ambako alikwenda katika Hospitali ya Ndolage baadae Hospitali ya Misheni Lubya kisha Hospitali ya Bugando.
“Maumivu yalizidi kuongezeka, sikupata nafuu, ndipo pale Bugando wakanipatia rufaa kuja kutibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili mwaka 2009,” anasema.
Dorothy anasema alipofika Muhimbili alielekezwa kwenda Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwani tatizo lake lilionekana ni la mifupa.
Mgongo umepinda
Maumivu makali aliyokuwa akihisi yalimsababishia awe anatembea huku akiwa ameinama kwa kuwa akifanya hivyo alihisi unafuu.
“Kwa hiyo nilianza kuinama kidogo kidogo, nilipoinama nilihisi nafuu lakini baadae nikajikuta siwezi tena kutembea nikiwa nimesimama, nililazimika kutembea na mkongojo, nilishangazwa na hali hiyo kwa sababu sikuwa na umri wa utu uzima kipindi hicho,” anasema na kuongeza:
“Tangu mwaka 2009 nahudhuria kliniki hapa MOI ingawa kuna wakati niliporejea nyumbani (Muleba) nilielekezwa kuhudhuria kliniki pale Bugando.
“Kipindi chote hicho nilikuwa napewa dawa za kutuliza maumivu na tiba ya mazoezi, nakumbuka wakati nikiendelea na matibabu baadhi ya wataalamu walinieleza kwamba matatizo ya mifupa huwa hayatibiki.
“Kwamba, nitaendelea kutumia dawa na tiba ya mazoezi maisha yangu yote. Kwa kweli nilikata tamaa, mazoezi yalinisaidia kupunguza maumivu ingawa kwa kiasi kidogo mno,”anasema.
Faraja mpya
Doroth anasema wakati akiendelea na tiba ya mazoezi uongozi wa MOI ulimueleza anaweza kufanyiwa upasuaji kutibu kabisa tatizo hilo jambo ambalo lilimpa faraja mpya.
“Nikaonana na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Nicephorus Rutabasibwa, akanihakikishia kwamba tatizo hilo linatibika, Agosti 29, mwaka huu nikafanyiwa upasuaji, nahisi nafuu kubwa kuliko awali,” anasema.
Anasema daktari alimdokeza alichokiona kwenye uti wake wa mgongo, pingili na mifupa, hasa sehemu ya chini ilikuwa imepinda hivyo, aliinyoosha na kumuwekea dawa.
“Sasa nina faraja na tumaini jipya kabisa, naona nimepona na natumaini ipo siku nitainuka kabisa na kutembea nikiwa wima kwa miguu yangu.
Shairi la pongezi
Anasema kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na daktari na taasisi hiyo, yeye na familia yake waliamua kuandika shairi la kuwapongeza.
“Unajua nilikuwa nimeshakata tamaa, nilihangaika hadi kutumia dawa za asili hasa zile za kuchua, sikupata nafuu lakini huduma ya upasuaji waliyonifanyia imenipa tumaini jipya,” anasema.
Daktari
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Nicephorus Rutabasibwa, anasema ugonjwa huo huwakumba watu wa jinsi zote hasa wale ambao huwa hawaishughulishi miili yao na kukaa muda mrefu katika eneo moja.
“Kwa mfano, wanaokaa ofisini kwa muda mrefu au wale ambao hufanya shughuli zinazowalazimu kuinama kwa muda mrefu,” anasema.
Utafiti
Anasema ingawa kiuhalisia tatizo hilo huwakumba watu wa jinsi zote, lakini utafiti uliofanywa kati ya Novemba, 2016 hadi Septemba, 2017 na taasisi hiyo umeonesha wanawake wanakabiliwa zaidi na tatizo hilo kuliko wanaume.
Anasema utafiti ulihusisha wagonjwa 100 waliokuwa wakipatiwa matibabu.
“Wagonjwa wengi tuliowapokea kwa matibabu walihusisha tatizo hili na uzee na hawakuwa wanajua kabisa kwamba ni ugonjwa na wanapaswa kutibiwa,” anasema.
Kwanini wanawake?
Anasema wanadhani huenda wanaume wanaokabiliwa na ugonjwa huo wanavumilia maumivu zaidi kuliko wanawake.
“Lakini pia tulipowahoji wanawake wengi walitueleza wao ni mama wa nyumbani, kwamba wana shughuli nyingi ambazo huwalazimu kuinama kwa mfano kufua, kuchota maji na nyinginezo.
“Aidha, kibaiolojia wanawake wanapokoma hedhi hupata tatizo liitwalo kitaalamu ‘osteoporosis’ ambalo hufanya mifupa yao kukosa nguvu kwa sababu huwa inakosa madini ya calcium ambayo yenyewe huimarisha mifupa.
“Hivyo, hali hiyo huongeza uwezekekano wa wanawake kupata tatizo zaidi ya wanaume. Katika utafiti huu asilimia 78 walikuwa ni wanawake,” anasema.
Anasema tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani zinaonesha watu wenye umri wa kuanzia miaka 35 wanakabiliwa na ugonjwa huo.
“Lakini kwa kuwa watu hawajui kama ni ugonjwa na kuona ni hali ya uzee, wagonjwa tunaowapokea hapa MOI wana umri kuanzia miaka 60 na kuendelea,” anabainisha.
Dalili
Anasema dalili za awali za tatizo hilo ni mtu kupata maumivu ya mwili, miguuni na wengine hushindwa kupata haja ndogo kwa wakati au kushindwa kujizuia kabisa na kujipata ikitoka yenyewe.
“Watu wanahusisha na uzee (umri mkubwa) kwani kiuhalisia kadiri umri unavyosonga mbele mifupa huishiwa nguvu na hivyo kusababisha kutokea mgandamizo katika uti wa mgongo na mshipa ya fahamu.
“Uti wa mgongo ulivyoumbwa umegawanyika, ipo sehemu ya shingo ambayo inaleta nguvu kwenye mikono kuna sehemu ya uti wa mgongo wa kiuno ambayo inaleta nguvu kwenye miguu.
“Hizi ni sehemu mbili ambazo huathirika kwa sababu hutumiwa zaidi katika kuinama, kuinuka, kuangalia juu au chini,” anasema.
Anasema matatizo hayo yapo kwa miaka mingi, kadiri umri wa mtu unavyosonga mbele ndivyo anakuwa kwenye hatari ya kuugua.
“Mtu huanza kuhisi maumivu ya mgongo kidogo kidogo baadae huongezeka, miguu huuma na wakati mwingine hufa ganzi au hata kushindwa kutembea kabisa kutoka eneo moja kwenda jingine au kushika kitu chochote mkononi,” anasema.
Anasema katika utafiti huo, asilimia 58 ya wagonjwa waliohusishwa walikuwa wakihisi maumivu ya mgongo, asilimia 78 walikuwa wanashindwa kutembea umbali wa kawaida pasipo kupumzika.
“Asilimia 58 walikuwa wanakabiliwa na tatizo la ganzi kwenye miguu, asilimia 20 walikuwa wanashindwa kabisa kutembea na asilimia mbili wakiwa wanashindwa kuzuia haja ndogo.
“Mtu anapotokwa haja ndogo bila kujizuia jambo hilo si la kawaida.
“Kwenye kibofu kuna mishipa ya fahamu ‘autonomic nervous system’ ambayo hufanya kazi ya kufunga na kufungua kibofu, yaani sypathetic na parasympathetic, ipo mishipa mingine ya fahamu ‘sokatic nerves’ kazi yake ni kuminya kibofu ili kisukume nje mkojo.
“Hivyo, uti wa mgongo unapokuwa umebana ile mishipa kwenye kibofu nayo inapata shida na mtu kujikuta mkojo ukitoka bila kujitambua au anashindwa kabisa kupata mkojo, unabaki kwenye kibofu,” anasema.
Anasema hii ni dalili mojawapo ya tatizo la uti wa mgongo, ingawa wengi hudhani kushindwa kupata haja ndogo ni matatizo ya mfumo wa mkojo au saratani ya tezidume, kumbe inategemea.
Anasema tatizo hilo hutibiwa ama kwa upasuaji au tiba ya mazoezi na dawa na mtu hupona kabisa.
“Changamoto tunayokumbana nayo ni baadhi ya wagonjwa wengi kuogopa tiba ya upasuaji, kuna dhana potofu kwamba uti wa mgongo unapoguswa mgonjwa huwa haponi kabisa jambo ambalo si kweli.
“Wanapona, wanatembea tena na wanarudi kuendelea na shughuli zao kama kawaida, mara nyingi wagonjwa tunaowafanyia upasuaji ni ya asilimia 10 ya wote wenye matatizo ya mgongo tunaowapokea, si lazima kutibiwa kwa upasuaji wagonjwa wote.
“Utaona zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa tunawatibu kwa tiba ya mazoezi na dawa. Kupitia matibabu haya ndiyo tunaweza kubaini yupi anahitaji upasuaji, waje hospitalini wasiogope, tunatumia kipimo cha MRI ambacho kinatuwezesha kubaini tatizo.
“Upasuaji huchukua kati ya saa mbili hadi tatu kukamilika na mambo yakienda sawa sawa kama tulivyopanga tunao uwezo wa kuwafanyia upasuaji wagonjwa watatu hadi wanne kwa siku,” anasema.
Anasema katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu wamewafanyia upasuaji wagonjwa zaidi ya 170.
Sababu za kuinama
Anasema mtu anayekabiliwa na ugonjwa huo huinama ili kujisitiri kuondoka na maumivu anayokuwa akiyapata wakati huo.
“Ugonjwa huu hauhusiani kabisa na urefu wala ufupi ila unahusiana kabisa na uzito wa mwili, mtu anapokuwa na uzito mkubwa anakuwa kwenye hatari zaidi,” anabainisha.
Vitu vizito
Anasema hauhusiani moja kwa moja na unyanyuaji vitu vizito ingawa watu wanaonyanyua vyuma nao hukabiliwa na maumivu ya mgongo.
“Wao hupatwa na tatizo jingine la uti wa mgongo kitaalamu linaitwa ‘disc prolapse’ mtu anaponyanyua vitu vizito hali hiyo husababisha ‘disc’ zilizopo katika uti wa mgongo kupasuka na kutoka kisha kwenda kukandamiza mshipa mmojawapo wa fahamu,” anasema.
Anasema matibabu huhusisha dawa, tiba ya mazoezi na au upasuaji na kwamba mara nyingi wagonjwa wanaowafanyia upasuaji ni chini ya asilimia 10.
“Zaidi ya asilimia 80 hadi 90 huwa tunawatibu kwa mazoezi na dawa,” anasema.