Beatrice Mosses, Manyara
Chama cha Ushirika cha Mabadiliko Saccoss Ltd. cha Mjini Babati mkoani Manyara kimewakopesha wanachama wake pikipiki 15 na cherehani moja vyenye thamani ya Sh milioni 36.
Akiwakabidhi mkopo huo, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu, ambapo amewataka wanachama hao waliokopeshwa kurejesha mkopo huo kwa wakati ili wengine wakope.
“Ili chama kipate maendeleo ni wajibu wenu kurejesha mkopo kwa wakati ili na wengine nao waweze kukopeshwa.
“Mwaka jana Septemba 2018 wanachama 11 wa chama hiki walikopeshwa pikipiki, bila shaka wamerejesha vizuri ndiyo maana na ninyi leo mnapata mkopo huu, vinginevyo wenzenu hawa wasingepata mkopo”, amesema Kitundu.
Pamoja na mambo mengine, amewashauri wanachama hao kuwa waaminifu ili Mabadiliko Saccoss iwe tegemeo la wanachama kujiendeleza kimaisha na hatimaye kufikia kwenye malengo makubwa ya ujenzi wa viwanda na kuwa ushirika wa viwanda.
Naye Meneja wa Mabadiliko SACCOS, Hussein Abrima, alisema kihistoria Chama cha Mabadiliko Saccoss Ltd kimetokana na chama mama cha Embesi cha mkoani Arusha na kufungua tawi mjini Babati mkoni Manyara.
“Ili kufanikisha malengo ya ushirika kabla ya kutoa mikopo ya bodaboda, walengwa walipatiwa mafunzo ya usalama barabarani ili mkopaji anapopewa chombo hicho aweze kukitunza na kuwa na uhakika wa kurejesha mkopo,” amesema Abrima.