26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kuongoza wageni kunawakwamua vijana kuondokana na umaskini Zanzibar

Faraja Masinde -Zanzibar

RIPOTI ya pamoja iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Benki Kuu (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya Uhamiaji na Tume ya Utalii ya Zanzibar (ZCT ), ya mwaka 2018 inaonyesha kuwa kiwango cha mapato yanayotokana na sekta ya utalii kimeongezeka kwa asilimia 7.13 ikilinganishwa na mwaka 2017.

Mapato hayo yametajwa kufikia kiasi cha Dola za Marekani bilioni 2.43 mwaka 2018 kutoka Dola bilioni 2.19 mwaka 2017, huku watalii waliotembelea Tanzania wakiongezeka kufikia milioni 1.49 ikilinganishwa na mwaka 2017 ambapo walikuwa ni milioni 1.33.

Ripoti ya wageni wa kimataifa wanaotoka na kuingia ya mwaka 2017 iliyotolewa na (NBS), watalii waliotembelea nchini mwaka 2016 walikuwa ni milioni 1.2 ambapo idadi hiyo imegawanywa katika ukanda huku watalii kutoka Ulaya wakiwa wengi zaidi wakifuatiwa na Bara la Asia na Pacific kisha Amerika, Afika na Mashariki ya Kati.

Kama hiyo haitoshi, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, siku chache zilizopita alifafanua kuwa Kampuni ya China National Travel Service Group Corporation (CTS), iko mbioni kuwekeza nchini katika sekta ya utalii, uwekezaji ambao utahusisha ujenzi wa hoteli Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.

Sekta ya utalii nchini inatajwa kuchangia asilimia12 ya ajira za moja kwa moja ambazo ni zaidi ya milioni moja, huku Watanzania wakiwa ni 467,000 sawa na asilimia 4.3 ya ajira zote.

Pamoja na yote haya, ni wazi kuwa unapotaja sekta ya utalii nchini huwezi kuviacha visiwa vya Zanzibar ambavyo vimekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea utalii.

Kwa nyakati tofauti, visiwa hivyo vimekuwa kivutio kwa wageni wengi na hata kusaidia kamisheni ya utalii visiwani humo kuvuka malengo waliyojiwekea kama alivyonukuliwa kamishna wa utalii visiwani humo, Khamis Mbeto, mapema mwaka huu.

“Kamisheni hiyo kwa sasa tayari imevuka malengo iliyoelekeza kuwa ifikapo mwaka 2020 Zanzibar itakuwa na watalii 500,000 ambapo kwa sasa tayari idadi ya watalii inakaribia kufikia 600,000 kabla ya mwaka 2020,” anasema Mbeto.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa idadi kubwa ya watalii waliotembelea visiwa hivyo vyenye marashi ya karafuu, wamekuwa wakihitaji kupatiwa taarifa za kutosha kutoka kwa wenyeji wao watakao waongoza.

Lakini changamoto imekuwa ni kwamba siyo kila mtu anaweweza kutoa taarifa sahihi kwa wageni na kuwashibisha maarifa ya kutosha juu ya visiwa hivi ikiwamo kama yanavyokuwa matarajio yao wakati wa kupanga safari hizo, kwani siyo kila mtu anaweza kujua historia ya visiwa hivyo vyema, achilia mbali changamoto ya lugha ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya wageni wanaofika visiwani humo hutumia lugha tofauti mbali na Kiswahili.

Hii inasababisha baadhi ya wanaoongoza wageni kushindwa kuwapa taarifa sahihi zenye kuwawezesha kukata kiu yao ya kuufahamu vyema Mji wa Zanzibar.

Hata vijana wa visiwa hivyo waliokuwa wakitamani kwenda darasani na kupata maarifa kwa ajili ya kuwasaidia kuongoza wageni kikamilifu ikiwamo kujiajiri waliishia kutamani kutokana na kushindwa kujimudu kifedha.

Changamoto hiyo na nyinginezo ndizo zilizoisukuma Taasisi ya kimataifa ya Tui CareFoundation kuanzisha chuo cha Kawa Training Centre, kilichopo Mji Mkongwe kwa lengo maalumu la kusaidia maeneo muhimu ikiwamo kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaotaka kuongoza wageni.

Tangu kuwapo kwa chuo hicho ni wazi kuwa imekuwa na mwamko katika kuchochea utalii visiwani humo, kwani vijana wengi wa kike na wa kiume waliohitimu chuoni hapo wamekuwa ni msaada mkubwa katika kuwaongoza wageni na kuchangia pato la taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi wa chuo hicho, kilichopo Mji Mkongwe, Suzanne Degeling, anafafanua kuwa uwapo wa chuo hicho umekuwa na msaada mkubwa katika kufanikisha shughuli za utalii visiwani humo.

“Kwa kweli hili ni jambo la kujivunia kuona kwamba vijana wengi ambao awali walikuwa na ndoto ya kuwa waongoza watalii wametimiza ndoto zao na kuwa sehemu ya uchumi wa Zanzibar.

“Baada ya kufika hapa miaka kadhaa iliyopita nikitokea nyumbani Uholanzi, nilibaini kuwa vijana wengi wanapenda kazi ya kuongoza wageni lakini hawana maarifa ya kutosha, nikalazimika kuanzisha chuo hiki kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali kwa nia moja tu ya kuwasaidia vijana kutimiza ndoto zao,” anasema Suzzane.

Anasema licha ya kwamba mwanzo huwa mgumu, alipata nguvu baada ya kuungwa mkono na Shirika la Tui Care Foundation, lenye makao makuu yake nchini Ujerumani ambalo limejikita kuhamasisha utalii sehemu mbalimbali ulimwenguni.

“Hivyo, walikuwa na ndoto za kutaka kuongoza watalii lakini walikuwa hawajui ni kwa namna gani wanaweza kuifanya kazi yao kwa ustadi mkubwa, hapo ndipo nikafikia hatua ya kuanzisha chuo hiki ili kuwasaidia vijana jambo ambalo limekuwa na mchango mkubwa kwao na jamii kwa ujumla,” anasema Suzzane.

Anafafanua kuwa pamoja na kwamba awali ilikuwa ni ngumu kwa vijana wa Zanzibar kutumia fursa hiyo ya uwapo wa chuo hiko, lakini kwa sasa anafurahi kuona wengi wamekuwa na mwamko na kwa kiwango kikubwa wameweza kufanikiwa kupitia chuo hicho.

“Awali wengi walikuwa wakiogopa kujiunga na chuo kwa sababu hawakuwa na fedha, nikatoa fursa kwa wenye nia ya dhati kuja kusoma kwa mkopo kwa kuwa lengo langu lilikuwa ni kuwaona wao wakifanikiwa kufikia malengo yao, fedha sikuzipa kipaumbele.

“Leo nafurahia kuona kwamba maendeleo yameendelea kuwa mazuri, vijana wengi wameajiriwa na kujiajiri kupitia chuo hiki japo mwamko wa wasichana umekuwa ni hafifu ukilinganisha na wavulana ambao wamekuwa wengi zaidi.

“Tunajitahidi kuona kuwa tunaondoa hii dhana ya kuamini kuwa kazi ya kuongoza watalii inapaswa kufanywa na wanaume pekee, tunaendelea kuwajengea vijana mtazamo wa kimataifa zaidi,” anasema Suzzane.

Anasema anaamini kuwa kuandaa waongoza watalii waliobora kupitia chuo hicho ndiyo mwendelezo mzuri wa kuendelea kuwa na idadi kubwa ya wageni kwani wanapokuja na kupewa taarifa sahihi basi ni wazi kuwa wataenda kuwa mabalozi wazuri kwa wengine na hivyo kufanya ongezeko la pato la uchumi wa Zanzibar.

“Tunawasaidia vijana kuwa sehemu ya uchumi wa nchi yao kwa kuchangia pato la taifa, ambapo kupitia ada wanazolipa kama waongozaji wageni zinaingia serikalini na hivyo kusaidia katika shughuli nyingine za maendeleo, hatimaye kuinua uchumi kwa ujumla.

“Lakini mwisho wa yote nashukuru ushirikiano mkubwa ambao nimeendelea kuupata kutoka serikalini, ambao nao kwa kauli thabiti wanaunga mkono jitihada za Kawa,” anasema Suzzane.

Mkurugenzi Mtendaji wa Masuala ya Nje na Maendeleo wa TUI Care Foundation, Alexander Panczuk, anafafanua kuwa wamekuwa bega kwa bega na chuo hicho cha Kawa ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa fedha na vifaa vya kufundishia ili kuwasaidia vijana kuhitimu na kuwa sehemu ya uchumi wa Zanzibar.

“Tumekuwa na jukumu la kuimarisha maeneo mbalimbali ya utalii duniani, ndiyo maana hatukusita kuonyesha ushirikiano wetu kwenye chuo hiki ili kuimarisha utalii wa Zanzibar na uchumi wa visiwa hivi kwa ujumla kupitia pato linalotolewa na wahitimu wa chuo hiki pale watakapoanza kuongoza wageni,

“Tutaendelea kuboresha mazingira mazuri zaidi ya utalii kwa sababu kwa kufanya hivyo tunakuwa tumeisaidia nchi husika katika kuongeza mapato yake na hivyo kunyanyua uchumi wake,” anasema Panczuk.

Miongoni mwa wanafunzi walionufaika na uwapo wa chuo hicho ni Ally Mussa Jappe(24), ambaye anasema kuwa ni miongoni mwa vijana walionufaika na uwapo wa chuo hicho ambacho mbali na kupata mafunzo chuoni hapo, pia amekuwa mwalimu wa chuo hicho pamoja na muongoza watalii mahiri, jambo ambalo limebadilisha maisha yake kwa kiwango kikubwa.

“Baada ya kumaliza elimu yangu ya sekondari, nilisikia juu ya kuwapo kwa chuo hiki cha Kawa Training Centre, nikasema ni sehemu ambayo naweza kupata uzoefu ikiwamo kuimarisha Kiingereza change. Nilijiunga hapa kwa nia ya kufahamu lugha na urithi wetu ambao tunao hapa Zanzibar.

“Nafurahi kuona nimeweza kuwa sehemu ya vijana waonachangia pato la taifa kupitia sekta hii ya utalii, lakini mbali na kuingiza fedha pia imenisaidia kunijengea mtazamo wa kimataifa ninaoupata kutoka kwa wageni mbalimbali ninaowaongoza,” anasema Jappe.

Anaongeza kuwa mbali na kufanikiwa kupata elimu na kuwa mwalimu chuoni hapo, anakiri kwamba Kawa wamekuwa na muunganiko wa kimataifa unaowasaidia vijana wengi kutimiza ndoto zao huku akigusia mtazamo wa wazazi.

“Kumekuwa na changamoto mbalimbali zikiwamo kuwa na waongoza watalii wasiofuzu vyema mafunzo ya kuongoza watalii, lakini pia mtazamo hasi kutoka kwa wazazi wanaoamini kuwa kusomea masuala ya utalii ni uhuni.

“Niwahimize wazazi kuwapa msukumo zaidi watoto wao kwani elimu ndiyo msingi na urithi pekee wanaoweza kuwaachia, tofauti na mali na fedha, thamani ya elimu ni kubwa zaidi,” anasema Jappe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles