KIGALI, RWANDA
KUNDI jipya la waasi, Vuguvugu la Mabadiliko ya Demokrasia Rwanda (MRDCD), limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa nchini hapa, likisema ni mwanzo wa safari ya kumng’oa Rais Paul Kagame.
Hata hivyo, mamlaka za Rwanda zimetupilia mbali uvumi kuhusu kuwapo ukosefu wa usalama maeneo yanayozunguka msitu wa Nyungwe, ambako MRCD inasemekana kuwa na ngome yake.
Akiongea na wenyeji wa Wilaya wa Nyaruguru, Inspekta Mkuu wa Polisi, Emmanuel Gasana, alisema licha ya majambazi wachache kuvuka na kuingia Rwanda na kuwapora watu eneo hilo, hali hiyo ilikuwa imedhibitiwa na vikosi vya usalama.
Hata hivyo, msemaji wa kundi hilo, Meja Callixte Sankara, alisema ni mwezi mzima sasa tangu wapiganaji wake washambuliane na wanajeshi wa Rwanda katika msitu wa Nyungwe kusini mwa nchi.
Walisema kundi lao limehusika na mashambulizi ya mwezi uliopita katika Kijiji cha Nyabimata karibu na msitu huo.
Akijitangaza kama naibu kamanda na msemaji wa kundi hilo, Meja ni askari mshirika wa zamani wa Rais Kagame.
Meja Sankara, alikuwa na Kagame kwenye lililokuwa kundi la waasi wa Rwanda Patriotic Front (RPF), ambalo sasa ni chama tawala nchini hapa.
Alikuwa askari mwenye cheo cha chini baada ya RPF kushinda vita ya msituni na kuchukua hatamu za uongozi kufuatia kifo cha Rais Juvenal Habyarimana kwenye shambulzi la ndege.
Haijulikani sababu zilizomkosanisha na utawala wa Kagame, lakini alifungwa jela na mahakama ya kijeshi kwa kipindi kisichojulikana kutokana na kile kilichotajwa kama utovu wa nidhamu.
Baadaye inadaiwa alitorokea Tanzania alikotiwa mbaroni.
Juhudi za utawala wa Kigali wa kutumia hati bandia za kuitaka Tanzania kumrudisha Meja Sankara nchini Rwanda, ziligonga mwamba na hatimaye Serikali ya Tanzania ilimwachilia huru na kumwezesha kusafiri uhamishoni Ufaransa.
Meja Sankara aliye na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Rwanda, kama ilivyo kwa Kagame, naye anatokea kabila la Tutsi na ni mjomba wa kiongozi wa upinzani aliye kizuizini nchini Rwanda, Diane Rwigara.
Licha ya mamlaka kukanusha, kumekuwa na taarifa kuhusu ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo ndani ya Rwanda.