21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

OBAMA AWASHUKIA MARAIS WABABE

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

RAIS wa zamani wa Marekani, Barack Obama, amesema dunia imetumbukia katika nyakati za kushangaza, kuhofisha na zisizotabirika kutokana na ongezeko la viongozi wababe na wasioheshimu demokrasia.

Vyombo vya habari vya Magharibi vimeichukulia kauli hiyo aliyoitoa juzi wakati wa mhadhara wa kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa shujaa wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela, kuwa imemlenga mrithi wake, Donald Trump.

Siku moja kabla ya hotuba ya Obama, Trump alikutana na Rais Vladimir Putin katika mkutano ambao umemfanya ashambuliwe kutoka kila kona kwa kumwonea haya kiongozi huyo mbabe wa Urusi.

Ijapokuwa Obama hakumtaja moja kwa moja, alizungumzia sera kadhaa za Trump ikiwamo biashara ya kujilinda, kuyakana mabadiliko ya tabia nchi na kuifunga mipaka.

Kadhalika Obama alikosoa tabia ya viongozi wababe, wanaoeneza hofu na kubomoa taasisi zinazoakisi demokrasia na kuifanyia maigizo, ikiwamo kujipatia ushindi wa asilimia 90 ya kura huku upinzani ukiwa unaminywa.

“Tazama. Siasa za kibabe zinaongezeka kwa kasi isiyofikirika zikiongozwa na viongozi wanaodharau ukweli na kusema uongo, na walio wababe ambao huendeleza demokrasia ya maigizo.

“Ni wale ambao uchaguzi na baadhi ya dhana za demokrasia huendelezwa. Lakini hujaribu kudhoofisha kila taasisi au maana ya demokrasia.

“Kwahiyo tunapaswa kuacha kujifanya kuwa nchi zinazozingatia uchaguzi tu… wakati mwingine mshindi kimiujiza anapata asilimia 90 ya kura, huku upinzani wote ukiwa umefungwa au haupati nafasi ya kuonekana kwenye televisheni na kudai eti hiyo ni demokrasia.

“Demokrasia inategemeana na taasisi imara na ni kuhusu haki za wachache, kuisimamia Serikali na uwiano, uhuru wa kutoa maoni na kuzungumza na uhuru wa habari na haki ya kuandamana na kuishitaki Serikali na mfumo huru wa mahakama, na kila mtu anapaswa kufuata sheria,” alisema.

Akitetea misingi ya demokrasia na utawala bora, Obama alikiri upungufu uliyo nayo, akisema inaweza kuwa kikwazo cha baadhi ya mambo.

“Ndiyo, demokrasia inaweza kuwa hovyo na inaweza kuchelewesha mambo na inaweza kukatisha tamaa. Lakini ni bora. Ufanisi unaodaiwa kutolewa na utawala wa kiimla, ni ahadi ya uongo.

“Msichague mwelekeo wa utawala wa kiimla kwa sababu hauna uwiano, bali unatoa fursa ya kujilimbikizia utajiri na madaraka kwa walio juu, na hufanya iwe rahisi kuficha rushwa na ukiukaji wa sheria.

“Licha ya kasoro zake zote, demokrasia ya kweli hulinda vyema dhana kuwa Serikali ipo kumtumikia mtu na si njia nyingine. Na ni aina pekee ya Serikali ambayo inatoa uwezekano wa dhana kuwa ya kweli,” alisema.

Wakati Obama akikosoa hayo mbele ya umati wa watu 15,000 katika uwanja wa kriketi jijini Johannesburg, aliwahimiza watu kuendeleza mawazo ambayo Mandela aliyapigania, ikiwamo demokrasia, utangamano na elimu bora kwa wote.

“Lazima tuanze kwa kufahamu kuwa licha ya sheria nzuri zilizoko kwenye katiba au vipengee vizuri kwenye katiba au kauli nzuri nzuri kuwahi kutolewa katika majukwaa ya kimataifa au Umoja wa Mataifa katika miongo ya hivi karibuni, masuala ya unyanyasaji na dhuluma za kale bado yangalipo,” alisema.

Obama alisema kila siku matukio yanayogonga vichwa vya habari ni ya kushangaza, kuna siasa za hofu, uhasama na kubana matumizi kwa kasi ambayo haikutarajiwa ikilinganishwa na miaka michache iliyopita.

Pia alisema kuwa mfumo wa kidunia umeshindwa kutimiza wajibu wake.

“Tunahitaji kutambua kuwa mfumo wa kiulimwengu umekosa kutimiza ahadi yake,” alisema.

Alitaja miongoni mwa sababu za kufeli kwa mfumo huo ni kushindwa kwa Serikali mbalimbali kuwajibika, na watu wenye ushawishi kushindwa kusuluhisha tofauti na upungufu katika jumuiya ya kimataifa.

“Hivi sasa tunaona kitisho cha kurudia njia hatari ya zamani ya kutatua shida badala ya kidiplomasa na demokrasia,” alisema.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na mjane wa Mandela, Grace Machel, walikuwa miongoni mwa wageni wakati wa hotuba ya Obama, ambayo imetajwa kuwa ya kiwango cha juu tangu aondoke madarakani.

Kabla ya hapo, Obama aliitembelea Kenya, akitokea Tanzania alikokuwa kwa mapumziko ya siku nane katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti akiwa na familia yake.

Mandela aliyefariki dunia mwaka 2013, amebakia kuwa shujaa duniani kote kufuatia mapambano yake ya muda mrefu kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi, ulioendelezwa na wazungu walio wachache nchini humo na ujumbe wake wa amani na maridhiano  alipoachiliwa huru baada ya miaka 27 ya kufungwa gerezani.

Hotuba ya Obama imekuja siku moja tu kabla ya siku kamili ijulikanayo kama Siku ya Mandela, yaani Siku ya kuzaliwa kwa Mandela ambayo huadhimishwa duniani kote Julai 18 (jana).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles