Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WAPO ndugu, jamaa na rafiki zetu ambao huwa na kawaida ya kukosa usingizi. Kuna ambao hudai hali hiyo huwatokea mara nyingi na sasa wameizoea kabisa.
Hatua hiyo huwaweka katika hatari ya kupata matatizo mengi zaidi pasipo wao kujua.
Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Said Bakari anazungumzia suala hili akisema kuwa ni tatizo ambalo baadae huathiri afya ya akili.
“Wengi hawajui jambo hili, kuna watu wenyewe hupenda ama kuonekana wanapenda kufanya kazi, hivyo hawana muda wa kupumzika kabisa. Wanapaswa kujua kwamba kufanya hivyo kunawaweka katika hatari ya kuathiri afya ya akili,” anasema.
Daktari huyo anasema watu wanapaswa kujua kwamba ubongo na akili navyo huhitaji kupumzika kama ilivyo kwa viungo vingine vya mwili wa binadamu.
“Mtu akifanya kazi nyingi pasipo kupumzika na akakosa usingizi baadae hali hiyo humsababishia kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi na hivyo kujikuta akiharibu kazi ofisini kwake,” anasema na kuongeza:
“Aliyekosa usingizi hataonesha dalili sawa na yule aliyeanza kutembea barabarani, kwamba ataanza kuleta vurugu, watu wataona kiwango chake cha kufanya kazi kinashuka.”
Anasema wapo pia ambao hupata maumivu makali ya kichwa, hushindwa kuona vema na hata kupooza mwili.
“Unakuta mtu analalamika anasumbuliwa na maumivu ya kichwa mwaka wa pili, kwa mfano akipimwa hakuna ugonjwa anaokutwa nao au haoni na akipimwa macho hayana tatizo, wengine wanalamika tumbo linauma lakini wakipimwa pia hakuna matatizo. Akili ikipata mshtuko husababisha matatizo makubwa,” anasema.
Anasema wengine huugua akili kutokana na matatizo ya kifamilia.
“Unakuta mama na baba hawaelewani kwa kipindi cha muda mrefu baadae hali hiyo huweza kusababisha matatizo ya akili hata kwa watoto wao,” anasema.
Dalili
Anasema mtu mwenye matatizo ya akili mara nyingi huonekana kuwa na mawazo ambayo huwa hayapo katika hali ya uhalisia.
“Yaani ile ‘thinking capacity’ yake au na imani yake inakuwa imetoka kabisa nje ya uhalisia, kwa mfano unasikia wote tunajua sisi ni binadamu na si Mungu na tunaamini kwamba Mungu yupo lakini anakuja mtu na kuanza kusema yeye ni Mungu na anasimama na msimamo wake huo.
“Unakuta anaanza kufanya vitu anavyodhani ni vya kimungu anapoulizwa ametoa wapi anatoa utetezi ambao mkiutazama mnaona kabisa anakabiliwa na tatizo la akili.
“Wakati mwingine hutokea mtu na kudai wanadamu wote ni wake, yupo mmoja ambaye alitueleza karibu watoto wote wa Tanzania ni wa kwake na anao wengine wengi Marekani, alisema amezaa na rais mmoja mkubwa duniani na kwamba hakuna mtu atakayemuambia amuelewe lolote, sisi tulijua moja kwa moja hilo ni tatizo la akili.
“Tunajua kuna njia tano za utambuzi, kugusa, kunusa, kuonja, kuona na kusikia lakini watu walio katika hali ya kuchanganyikiwa huwa wanahisi vitu ambavyo havipo.
Anasema kukosa usingizi ni sababu kubwa ya maradhi ya akili kwa kuwa husababisha kutetereka afya ya akili kwa haraka.
Madhara
Anasema iwapo mtu hatawahi hospitalini kupata tiba, tatizo hilo huanza kumuathiri yeye mwenyewe.
“Hii ni kwa sababu hushusha kiwango chake cha kufanya kazi kama awali, hivyo uchumi wake utatetereka na jamii yake nayo huathirika maana hulazimu watu kuwa karibu naye wakimuhudumia.
“Afya ya mwili wake nayo hutetereka kwani kinga zake hushuka kwa kiwango kikubwa, magonjwa haya huleta matatizo pia kwenye ndoa nyingi na mwisho husababisha vifo,” anasema.
Yanatibika
Daktari huyo anasema magonjwa hayo yanatibika kama maradhi mengine ingawa yapo machache ambayo hayatibiki.
“Huwa tunatumia dawa kutibu maradhi haya lakini kama yametokana na hitilafu za kemikali (ya kurithi) huwa hayatibiki ingawa zipo dawa zinazosaidia kurekebisha kemikali hizo,” anasema.
Anasema huwa pia watumia njia ya ushauri wa kisaikolojia na matibabu ya jamii ambapo tunaelimisha jamii inayomzunguka mgonjwa ili wasimtenge kutokana na hali aliyonayo.