23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WENYE ULEMAVU SASA WATHAMINIWA

Na MWANDISHI WETU, Kagera

KWA binadamu wengine, mabadiliko yanaweza kutokea baada ya muda mrefu hata miaka miwili au mitatu.

Kwa watu wenye ulemavu mbalimbali katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera mabadiliko ni sasa.

Hili limejidhihirisha kupitia mradi wa kutetea haki za watu wenye ulemavu ambao upo katika hatua zake za awali za utekelezaji.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo uliopewa ruzuku ya Sh milioni 70 na Shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Civil Society (FCS) ni Restuta John wa Kijiji cha Ruzoka wilayani Biharamulo anasema baba yake aliposikia kuwa anatakiwa kwenda kwenye mafunzo, hakusita kama ilivyo desturi yake kwa watoto wa kike kwa kuwa alitamani kuona mabadiliko ya mwanawe.

“Nilipofungua mlango kuwakaribisha wageni kutoka Parokia ya Rulenge na Halmashauri ya Biharamulo ambao walifika kutusajili sisi walemavu, sikuyaamini macho na masikio yangu…sikuwa naamini kuwa kuna siku wenye ulemavu wangeweza kuitwa na Serikali au chombo chochote kusikilizwa au kupewa semina,”anasema Restuta.

Anasema alikuwa akirejea tukio la Kanisa Katoliki Rulenge, linalotekeleza mradi huo wilayani Biharamulo kufika nyumbani kwake na kwa wengine na kuchukua maelezo kuhusu watu wenye ulemavu na shida nyingine, ambapo walemavu  wapatao 9000 walisajiliwa katika zoezi hilo lililofanyika katika vijiji 79.

Anasema kwa mara ya kwanza  katika historia ya maisha ya baadhi yao, mradi huu umewanufaisha mamia kwa mamia ya wananchi wenye ulemavu kujitokeza na kutoka nje ya  walezi kuwaruhusu kutoka nje kuhudhuria mafunzo.

Naye Emmanuel Nganagiza kutoka Kijiji cha Katoke anasema; “kuanzia sasa, watu wote wenye ulemavu hawatakubali kukaa na kufungiwa ndani ya nyumba tena kwa kuwa mradi huu umetufungua macho.”

Mratibu wa Mradi huo, Fr. Honoratus Ndaula anasema; “mradi unachangia juhudi za halmashauri na serikali kuu kuyafahamu matatizo na changamoto za watu wenye ulemavu na kujiandaa kuyakabili.”

Kauli ya Padri Ndaula iliungwa mkono na wadau wengine wakiwamo wawezeshaji na wanufaika.

Nao viongozi kutoka Kata ya kabindi na Nyabusozi walifurahia mradi huo kwa madai kuwa umewatoa shimoni na kufanya waonekane kama binadamu wengine wenye haki zao.

Wanasema ilikuwa haijawahi kutokea kwa serikali au wadau wengine kupita mlango kwa mlango kusajili watu wenye ulemavu.

“Wazazi, walezi, ndugu na jamaa sasa wanafahamu wajibu wao kwa watu wenye ulemavu, kwa  sasa wanawaona watu hao si kero wala laana bali wana fursa ya kubadilisha maisha yao na ya wenye ulemavu,” anaeleza Anatoly Rubeja wa Kata ya Bisibo.

Anaongeza kusema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni jinsi ya kuwapatia mahitaji yao muhimu kama chakula, mavazi na malazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles