VITENDO vya kuwatumikisha watoto katika ajira mbalimbali zikiwamo za mashambani, vimekuwa vikikemewa na kupigwa vita kila kukicha.
Katika kuonesha msisitizo, juzi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwaonya watu wanaoajiri watoto kwenye mashamba ya tukumbaku mkoani Tabora na kuwataka waache mchezo huo, kwani ni kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania kila mwenye umri chini ya miaka 18 ni mtoto na analindwa na Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009.
Sheria hiyo ni waraka unaoshughulikia masuala mengi ya kitaifa yanayohusu sheria ambapo inakusanya yote na kuyaweka kwenye waraka mmoja.
Sheria hii pia imechukua mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa yanayohusu haki za mtoto na vilevile kutoka kwenye sera ya taifa ya watoto.
MTANZANIA tunasema kuwa licha ya uwapo wa sheria hiyo ya mtoto lakini pia ni lazima ukawepo muundo unaolenga kumpa mtoto kinga katika ngazi za kitaifa na hivyo kuweka viwango kwa ajili ya utoaji haki kwa watoto.
Vipengele vilivyomo kwa ajili ya watoto wanaohitaji matunzo nje ya makazi yao, na vilevile kanuni za kudhibiti ajira za watoto zimepewa nguvu zaidi katika sheria hii mpya.
Sheria hii inatambua kwamba watoto wana haki ya kupewa jina na utaifa na kusajiliwa mara baada ya kuzaliwa.
Na ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kumnyanyasa mtoto eti kwa sababu ni msichana au mvulana, au kwa sababu ya umri wake au dini au asili yake au kwa sababu yeye ni fukara.
Watoto wana haki   ya kutoa maoni yao kuhusu uamuzi unaofanywa   ambao unagusa maisha yao, na ni wajibu wa watu wazima kuzingatia maoni ya watoto pale wanapofanya uamuzi huo.
Watoto wana haki ya kuwafahamu wazazi wao na kuishi nao katika mazingira ya kuwajali na yenye amani. Watoto  nao wana wajibu wa kuwaheshimu na kusaidia shughuli za familia kutokana na uwezo wao.
Kutokana na hali hii Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wakazi wa Mkoa wa Tabora kuwapeleka watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya ya mkoa huo katika kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalumu.
Kutokana na hali hiyo aliwataka wana jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na kuacha kuwatumia watoto wadogo kama vibarua mashambani.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alitumia fursa hiyo kusisitiza viongozi wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha wanahitimu elimu ya sekondari.
Suala la mimba mashuleni linahitaji usimamizi madhubuti, ili kuwalinda watoto wa kike waweze kumaliza elimu ya msingi na sekondari na baadae waweze kujiunga na elimu ya juu.
Kifungu cha 4 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 kinamwelezea mtoto kama mtu mwenye umri chini ya miaka 14, isipokuwa kwa ajira zilizo katika sekta hatarishi, mtoto maana yake ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18.
Zipo sheria kadhaa zinazoelezea ajira kwa watoto kama vile Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sheria ya watoto na sheria ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi zikiwa ni miongoni mwa nyingi. Lakini linapokuja suala la ajira na kazi, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ndio inayokidhi hasa.
Sisi MTANZANIA tunaunga na Serikali kuwataka wazazi na walezi kutambua kwamba sheria inakataza mtoto kuajiriwa.
Sheria pia inaendelea kukataza ajira kwa watoto chini ya miaka 18 katika maeneo ya migodini, viwandani, kama mabaharia katika meli au kazi nyingine inayotambulika kua ni hatarishi.