ASHA KIGUNDULA-DAR ES SALAAM
KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck, amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake, huku akimtaja kipa wa KMC, Jonathan Nahimana kuwa mchezaji wake bora wa mchezo wao.
Simba ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ushindi huo uliifanya Simba kufikisha pointi 31 na kuendelea kujikita katika msimamo wa ligi hiyo, baada ya kucheza mechi 12, ikishinda 10, sare moja na kupoteza mchezo mmoja.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, Vandenbroeck aliwasifu wachezaji wake kwa kupambana na kufanikisha kupatikana kwa pointi tatu.
“Kikindi cha kwanza kila timu iliweza kufunguka na kutafuta mabao, nimpongeze kipa wa KMC kwa kuokoa mipira mingi ya hatari.
“Kipindi cha pili tuliingia na mfumo wa kushambulia na kufanikiwa kupata mabao mawili yaliyotupa pointi tatu,”alisema kocha huyo na kuongeza.
“Ligi imekuwa ngumu kwakuwa michezo inapishana kwa siku mbili.
“Tumekuwa na
mechi za karibu na ngumu, kwangu nina furaha kwa wachezaji wangu kuonyesha
kiwango kizuri ambacho kinaleta matokeo mazuri.”
Akizungumzia mchezo dhidi ya Watani wao wa jadi, Yanga utakaochezwa Januari 4
mwakani, alisema: “ Ninachohitaji ni wachezaji kupambana ili
kupata pointi tatu katika kila mchezo na si kuweka nguvu kwenye baadhi ya
michezo.”
Simba inaongoza kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 31, baada ya kucheza mechi 12 ikishinda mechi 10 ikitoka sare mechi moja dhidi ya Tanzania Prisons na kufungwa mechi 1 na Mwadui FC ya Shinyanga.