24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Yanga moto kuikabili Biashara

 ASHA KIGUNDULA-DAR ES SALAAM

MABINGWA mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara,Yanga leo inashuka dimbani kuumana na Biashara United ya Mara, katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dare s Salaam. Yanga itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuvuna pointi tatu katika mchezo wake uliopita uliochezwa Uwanja wa Samora mjini Iringa, baada ya kuilaza bao 1-0 Tanzania Prisons.

Wanajangwani hao wanafahamu kuwa wanahitaji ushindi ili kuzidi kujongea juu ya msimamo wa Ligi Kuu msimu huu.

Pia wanataka ushindi ili kujiweka katika hali nzuri kisaikolojia, wakati wakisubiri kuumana na Watani wao wa jadi, Simba, mchezo utaochezwa Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, mchezo huo hautakuwa mwepesi kwa Yanga kwani wapinzani wao Biashara nao wanahitaji matokeo mazuri ya pointi tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Biashara United inayofundishwa na Francis Baraza, inahitaji ushindi kwa udi na uvumba, huku ikitaka kuendelea kuweka rekodi ya kutoa kichapo kwa mabingwa hao. Biashara iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu wa msimu uliopita uliochezwa Uwanja wa Karume, Musoma.Wachezaji David Molinga, Papy Tshishimbi, Mrisho Ngassa na Denis Kaseke, wanaweza kuleta shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo yenye makao yake makuu, Mtaa wa Twiga, Dar es Salaam. Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 21, ikicheza mechi 10, ikishinda sita, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja.

Biashara United inashika nafasi ya 15 miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo, ikiwa na pointi 15, ikishinda michezo minne, sare tatu na kuchapwa mara sita.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema afya za wachezaji wake zipo vizuri kwa ajili ya kucheza mchezo huo.

“Mchezo dhidi ya Biashara ni muhimu kwetu kushinda ili kuongeza ari ya kikosi kuelekea mchezo na Simba, kwa ujumla hali ya wachezaji wangu zipo vizuri,”alisema Mkwasa.

Kwa upande wa Baraza alisema wanafahamu wapo kwenye nafasi isiyoridhisha hivyo watapambana kuhakikisha wanavuna pointi tatu dhidi ya Yanga, ili kujongea juu ya msimamo wa ligi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,476FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles