Christina Gauluhanga, Dar es salaam
MKURUGENZI wa Shirika la The Green Icon, Tajiel Urioh amesema, takwimu za mwaka 2014 za Shirika la World Resources Institute (WRI), zinaonesha kuwa kiwango cha gesi joto zilizozalishwa Tanzania zilikuwa 286.49 ambayo ni sawa na asilimia 0.59 ya gesi yote Duniani.
Hayo aliyasema ajana jijini Dar es Salaam wakatiwa uzinduzi wa kampeni ya ulinda uhai iliyoandaliwa na Shirika la Mulika Tanzania kwa kushirikiana na asasi nyingine ambapo alisema kuwa kiwango hicho ni kikubwa hivyo jitihada mbalimbali zinahitajika za kukabiliana na mabadilio ya tabianchi.
“Takwimu hizi zinaonyesha kiwango ni kikubwa cha gesi joto kinatoka mwenye sekta ya misitu na kubadilika kwa matumizi ya ardhi (asilimia 72.7), inafuatiwa na sekta ya Kilimo (asilimia 17.3), nishati (asilimia 7.8), taka (asilimia 1.6) na Viwanda (asilimia0.5),” alisema Urioh.
Alisema changamoto ya ukataji miti jambo ambalo linaondoa uoto wa asili linachangia kuongezeka ambapo nchi inapoteza takribani hekta 468,000 za misitu kwa mwaka huu.
Akizungumzia ongezeko la watu alisema kwa Jiji la Dar es Salaam ifikapo 2050 idadi ya watu itafikia milioni 130 kutoka milioni 45.
“Takwimu za Benki ya Maendeleo ya Afrika inaonyesha ifikapo 25 Dar es salaam itakuwa na asilimia 85 ifikapo 2025,mpaka kufikia 2040 nusu ya wakazi watakuwa wakiiishi mijini,” alisema
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Dar es Salaam, Masarida Zephania alisema mradi huo wa kuelimisha wanafunzi kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na kuwepo kwa majanga.
“Kuna mambo mengi yanaweza kutokea ni vyema wanafunzi wakajua namna ya kukabiliana nazo na pia kuzigeuza kuwa fursa na vilevile wanafunzi wanapaswa kufuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania,” alisema Zephania.
Naye, Mkurugenzi wa Mulika, Hussein Melele alisema wamedhamiria kuhamasisha vijana katika kampeni hiyo ili iwe chachu ya maendeleo kwa jamii.
“Mabadiliko yana athari kubwa ndani ya jamii hivyo tutaendelea na kampeni hii ambayo tumeanza nayo kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari,” alisema Melele.