Derick Milton, Simiyu
Baadhi ya kampuni za ununuzi wa zao la pamba wilayani Bariadi mkoani Simiyu, zimeanza kulipa madeni wanayodaiwa na wakulima wa zao hilo katika wilaya hiyo.
Moja ya kampuni hiyo ni C&C Company Ltd ya mkoani Mara, ambapo imetoa kiasi cha Sh bilioni moja kwa ajili ya kulipa ililokuwa ikidaiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga amesema kuwa fedha zitalipwa kwa wakulima ndani ya wiki hii.
“Leo wameanza na Sh bilioni moja ambazo zote zitalipwa kwa wakulima wote ambao wanaidai kampuni hii Sh bilioni tano kupitia Amcos zao, kesho wanaleta bilioni mbili na Jumapili watamalizia bilioni moja,” amesema Kiswaga.
Aidha, Kiswaga amewataka viongozi wa Amcos kutumia fedha hizo kwa ajili ya kuwalipa wakulima tu madeni yao, huku akiagiza maofisa ushirika wa wilaya hiyo kusimamia zoezi la ulipaji hadi kukamilika.