25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

KILICHOBAKI KWA BUFFON NI LIGI YA MABINGWA

NA BADI MCHOMOLO


KUNA wachezaji wengi wenye majina makubwa duniani walifanikiwa kutwaa Kombe la dunia zaidi ya mara moja, lakini hadi wanastaafu hawakufanikiwa kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mshambuliaji hatari wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil, Ronaldo De Lima, ambaye aliwahi kucheza soka kwenye klabu kubwa kama vile Barcelona, Inter Milan, AC Milan na Real Madrid, hakuwa na bahati ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mbali na kuuteka ulimwengu wa soka kwa kuwa namba 9 bora duniani, lakini hadi anaamua kustaafu soka mwaka 2011, aliishia kutwaa Kombe la dunia mara mbili akiwa na kikosi imara cha Brazil.

Baada ya kuchukua Kombe la dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1994, akawa anapambana kuhakikisha anatwaa Ligi ya Mabingwa kabla ya 2002 kupata tena Kombe la dunia.

Wanasema mchezaji ili aweze kuweka historia kubwa kwenye soka duniani aweza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or), Kombe la dunia na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa upande wa Ronaldo aliweza kutwaa Kombe la dunia, Ballon d’Or pamoja na mataji mengine mbalimbali, lakini hakuweza kuzisaidia klabu zote alizopita kutwaa Ligi ya Mabingwa (UEFA).

Haikumaanisha kuwa sio mchezaji bora, lakini kukosa Kombe hilo kwa mchezaji mkubwa kama huyo kwake ni kitu ambacho kimemfanya aonekana kuwa na mapungufu katika maisha yake ya soka.

Wiki iliopita mlinda mlango wa timu ya Taifa ya Italia, Gianluigi Buffon, alitangaza kustaafu soka la timu hiyo mara baada ya kushindwa kufuzu Kombe la dunia 2018 nchini Urusi.

Timu hiyo imeshindwa kufuzu baada ya kuchezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Sweden katika mchezo wa kwanza, huku mchezo wa marudiano ukimalizika kwa suluhu, hivyo Italia ikaondolewa kwenye michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958.

Mapema mwaka huu kipa huyo ambaye anakipiga katika klabu ya Juventus, alisema kuwa atahakikisha analipigania Taifa hadi Kombe la dunia na ndipo aweze kustaafu, lakini ndoto zake za kushiriki michuaono hiyo kwa mara ya mwisho mwakani ilifikia tamati wiki iliopita.

Akili ya Buffon kwa sasa ni kuhakikisha anapambana ili kuacha historia kama ilivyo kwa wachezaji wengine ambao wamestaafu wakiwa na mataji makubwa muhimu, lakini kutokana na umri wake hali inaweza kuwa ngumu kwa upande wake.

Mchezaji huyo kwa sasa ana umri wa miaka 39, kuna uwezekano mkubwa mwishoni mwa msimu huu ikawa ndio mwisho wake wa kucheza soka, hivyo Juventus ina kazi kubwa ya kufanya ili kutwaa taji hilo.

Juventus wana wakati mgumu wa kuchukua taji hilo kutokana na ubora wa timu ambazo zinashiriki Ligi ya Mabingwa msimu huu kama vile PSG, Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, Manchester City, zikiwa kwenye ubora wa hali ya juu na wachezaji wenye uwezo mkubwa.

Kama Buffon ameshindwa kuipigania Italia kufuzu Kombe la dunia mwakani, basi inawezekana akawa na bahati ya kutwaa Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake ya soka, ila sio rahisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles