29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

KOMBE LA DUNIA 2018 LITAKUWA LA KIHISTORIA

MWANDISHI WETU NA MITANDAO


NI miaka mitatu imepita tangu ulimwengu wa soka kuishuhudia timu ya taifa ya soka ya Ujerumani ikitawazwa mabingwa wapya wa Kombe la Dunia juu ya ardhi ya Brazil mwaka 2014, baada ya kuifunga Argentina bao 1-0.

Michuano ya mwaka huo ilikuwa ni ya kufurahisha kama sio kushangaza, ikiwa na matokeo yaliyowaacha wengi midomo wazi na historia pia.

Moja ya kitu cha kukumbukwa zaidi ni kichapo cha aibu walichokipata mabingwa mara tano wa kombe hilo na waliokuwa wenyeji wa michuano hiyo, Brazil, cha mabao 7-1 kutoka kwa Ujerumani. Haikuwa siku nzuri kabisa kwa wananchi wa Brazil.

Na sasa, kwa mara nyingine tena tutapata wasaa maridhawa wa kuishuhudia tena michuano hiyo ikirindima nchini Urusi mwakani.

Msimu huu kuna timu ambazo zimefanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza lakini, nyingine zimerejea na nguvu mpya baada ya kupita miaka kadhaa bila ya wadau wa soka kuziona katika msimu mmoja au miwili ya michuano hiyo.

Timu hizo ni Tunisia, Morocco, Senegal, Saudi Arabia, Sweden, Poland ambazo zote hizo hazikushiriki michuano ya Kombe la Dunia 2014, huku Iceland ikifuzu kwa mara ya kwanza katika historia yao ya mchezo wa soka.

Morocco ndilo taifa pekee kati ya hayo yaliyofuzu ambalo halijashiriki michuano hiyo kwa muda mrefu, ambapo ilifuzu kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 19, mara ya mwisho wakishiriki michuano ya mwaka 1998 ambayo bingwa wake alikuwa ni Ufaransa.

Hata hivyo, shukrani zimwendee kocha mwenye historia nzuri na timu za Afrika, Herve Renard, ambaye uzoefu wake wa kufanya kazi kwenye mazingira yenye changamoto nyingi za soka Afrika uliisaidia Morocco kurudi tena kwenye mashindano hayo makubwa.

Renard anakumbukwa kwa kuzifanya Zambia na Ivory Coast kutwaa mataji ya kihistoria ya Mataifa Afrika katika miaka ya 2012 na 2015. Lakini, bila kujituma kwa mastaa wa timu hiyo wakiongozwa na nahodha Mehdi Benatia, Morocco ingetazama michuano hiyo kwenye runinga.

Morocco walimaliza kundi lao na alama 12, ikishinda mechi tatu, sare tatu; ikifunga mabao 11 na bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa katika mechi sita za hatua ya makundi.

Timu nyingine ambayo kwa muda mrefu haikuonekana katika michuano hiyo na imekuja kufuzu mwaka huu ni Senegal. Mara ya mwisho kuonekana ilikuwa ni mwaka 2002, walipotinga robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Hata hivyo, hatua hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa safari yao katika michuano hiyo ambapo walijikuta wakipoteza mchezo mbele ya Uturuki kwa bao 1-0 lililofungwa na Ilhan Mansiz dakika ya 90 na nne za nyongeza, katika mtanange uliolazimika kwenda hadi dakika 30 za nyongeza baada ya zile tisini kumalizika kwa suluhu.

Senegal ya miaka hiyo ilikuwa si ya mchezo mchezo, ambapo wachezaji kama Papa Bouba Diop, Ferdinand Coly, Papa Malick Diop, El Hadji Diouf, Henry Camara na wengineo, na iliweza kuzisumbua timu kubwa duniani, lakini baada ya michuano hiyo haikuweza kufuzu kwenye misimu mitatu mfululizo ya Kombe la Dunia.

Kurudi kwao kwa ajili ya michuano ya mwakani kunachangiwa na uwepo wa wachezaji wengi bora na vijana, wakiongozwa na kocha Aliou Cisse ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha Senegal kilichocheza dhidi ya Uturuki mwaka 2002 akiwa nahodha.

Unaweza pia kusema historia ya mafanikio ya kocha huyo Cisse yameisaidia Senegal kutinga kwenye michuano hiyo baada ya kukosekana kwa muda mrefu.

Mataifa mengine ya Poland na Sweden, ambayo yanatoka katika ukanda wa Ulaya, pamoja na Saudi Arabia ambao wapo Asia nayo yalipambana vilivyo na kujihakikishia nafasi hiyo baada ya kupita miaka 11 ya kutoshiriki michuano hiyo, mara ya mwisho wakionekana mwaka 2006.

Katika kipindi cha miaka yote hiyo, Poland na Sweden zilikumbwa na ugumu wa kuchuana na mataifa ambayo kimsingi yanajiweza duniani, kama vile Ujerumani, Hispania, England, Ureno na mengineyo.

Kwa mapana, tumeziangazia zile timu ambazo zimefuzu kushiriki michuano hiyo lakini hatujazitupia macho timu nyingine ambazo zimekosa tiketi ya kushiriki michuano mwakani ambazo ni Chile, Uholanzi, Ghana, Algeria, Ugiriki, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Italia ambao ndio waliowaacha wengi midomo wazi kwani haikutegemewa kwa taifa lenye historia kubwa na michuano hiyo kushindwa kufuzu.

Italia walipangwa Kundi G na nchi za Macedonia, Albania, Israel, Liechtenstein na Hispania, na kiukweli, timu iliyokuwa ikiwapa upinzani ilikuwa ni Hispania ambao walimaliza kundi hilo wakiwa nafasi ya kwanza na kuilazimisha Italia kucheza mechi ya mchujo ili waweze kwenda Urusi.

Kwa mfumo wa kufuzu katika bara la Ulaya, ni mshindi mmoja tu kwa kila kundi anayekuwa na uhalali wa kushiriki michuano hiyo hivyo Italia haikuwa najinsi zaidi ya kuvaana na Sweden kwenye mechi hiyo ya mchujo (play off).

Hata hivyo, Italia ilishindwa kufurukuta mbele ya Sweden na kukubali kichapo cha jumla ya bao 1-0, baada ya kucheza mechi hizo mbili dhidi ya Sweden.

Lawama zote za matokeo hayo ya Italia kuikosa tiketi ya kushiriki michuano hiyo zilitupwa kwa kocha, Giampiero Ventura kwa kukosa mbinu za kiufundi kulingana na hadi ya timu hiyo ya taifa na kulifanya taifa hilo lianguke kwenye aibu kubwa ya soka.

Vyombo vya habari viliyataja matokeo hayo kama ‘ngumu kumeza’ na kila kona ikihimiza kocha huyo abwage manyanga na hatua za lazima zichukuliwe ili kuirudisha Italia kwenye mstari ulionyooka.

Tunapata funzo gani kama Tanzania na timu yetu ya Taifa Stars? Ni kwamba, hakuna mafanikio yanayopatikana kwa njia rahisi na ndiyo maana Iceland imefanikiwa kutinga michuano hiyo kwa mara ya kwanza kwenye historia yao ya soka kutokana na kutekeleza mipango yao kwa vitendo na sio maneno kama ilivyozoeleka hapa nchini.

Aidha, inaweza kuwa ni kosa kuifananisha Iceland na Tanzania kutokana na maendeleo ya soka katika nchi za nje kuwa juu zaidi yetu kwa namna moja ama nyingine, lakini kwa kuzingatia misingi ya soka ambayo ni mipango madhubuti na kujituma kwa sana, hakutakuwa na sababu ya maana ya kujitetea kama tusipoona timu yetu ya Taifa Stars ikishindwa kufikia Watanzania wanapopataka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles