WASHINGTON, MAREKANI
SPIKA wa Bunge kutoka Chama cha Republican, Paul Ryan amesema hatamtetea tena mgombea urais wa chama hicho, Donald Trump baada ya kutoa kauli zinazodhalilisha wanawake.
Ryan ameapa kuanzia sasa atajikita kusaidia wagombea wa chama hicho katika ngazi ya ubunge na useneta.
Hata hivyo, Ryan hajabatilisha uamuzi wake wa kumuidhinisha mgombea huyo.
Trump naye amemjibu Ryan kupitia mtandao wa Twitter, akisema hapaswi kupoteza muda kumpigania.
Awali, mpinzani wa Trump kutoka chama cha Democratic Hillary Clinton alitilia  shaka hatua ya Trump kuomba radhi kutokana na matamshi hayo aliyoyatoa miaka 11 iliyopita.
Kwenye kadhia hiyo ya video, Trump anaonekana akisema alivyoomba kushiriki mapenzi na mwanamke aliyeolewa.
Aidha, anatoa matamshi ya kudhalilisha kuhusu wanawake.
Lakini wakati wa mdahalo Jumapili usiku, Trump alisema maneno yake kwenye kanda hiyo ya video yalikuwa ‘mazungumzo ya mzaha faraghani’.
Maofisa 38 wakuu wa Republican, wakiwemo maseneta, wabunge na magavana, wameondoa uungaji mkono wao kwa Trump, tangu kutokea kwa video hiyo Ijumaa iliyopita.