29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kifusi chaua watatu mgodini Arusha, wengine wajeruhiwa

ELIYA MBONEA-ARUSHA

MIILI ya watu watatu waliofukiwa na gema katika machimbo ya moram yaliyopo Moshono Kata ya Moivaro jijini Arusha, imeipolewa huku ikiwa imeharibika kwa kutoboka macho na kukatika mikono.

Gema hilo lilianguka jana asubuhi na juhudi za uokoaji zilianza saa 2 asubuhi ambapo hadi majira ya mchana kwa vikosi vya askari polisi, zimamoto vikishirikiana na wananchi walifanikiwa kuipata miili hiyo na gari lililofunikwa gema hilo.

 Katika tukio hilo pia watu wawili walijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

 Kukatika kwa ngema hilo kunadaiwa kusababishwa na mvua zilizonyesha jana usiku katika baadhi ya maeneo ya mji wa Arusha. Mwaka 2013 katika machimbo hayo gema lilianguka na kuua watu 13.

Mkuu wa wilaya ya Arusha, Fabian Daqarro alisema wanaendelea na juhudi za kuokoa miili hiyo na hawata simama mpaka wafanikiwe kuitoa kwenye vifusi.  

“Miili mitatu imetolewa na watu wawili waliojeruhiwa wamekimbizwa Hospitali ya Mount Meru, tupo hapa kuhakikisha miili ya waliofunikiwa inapatikana,” alisema DC Daqarro na kuongeza:

 “Ngema hili ni kubwa limeanguka baada ya mvua kunyesha usiku wa jana,” alisema.

 Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, alisema kwa kushirikiana na vikosi vya Jeshi la Zimamoto, Polisi na Jeshi la Wananchi watahakikisha zoezi linafanikiwa.

 Naye Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, alisema taarifa hizo walizipata mapema asubuhi na wakatoa mashine ya Jiji kwa ajili ya kusaidia uokozi.

 Alisema Halmashauri ya Jiji huchukua ushuru wa Sh 20,000 kwa kila gari linaloingia kuchukua Moramu huku ushuru mwingine ukichukuliwa na Wizara ya Madini.

Lema 

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akizungumzia eneo la tukio alisema suluhisho la mgodi huo si kuufunga badala yake mamlaka husika zitafute ufumbuzi wa kudumu. 

“Hapa kuna familia zinategemea machimbo haya kulisha familia na kujipatia riziki,” alisema Lema.

Mchimbaji wa moramu kwenye mgodi huo, Leston Joeli aliliambia MTANZANIA kuwa hapo ndipo wanapopata riziki za kuendeshea maisha yao ya kila siku ikiwamo kusomesha watoto wao.  

“Hapa ndipo riziki ya kula na watoto wetu inapopatikana, tunafanya kazi Jumatatu Saa 1 asubuhi mpaka Jumamosi 11 jioni. Hili ni tukio la bahati mbaya, kulikuwa hakuna dalili zozote za hili ngema kuanguka. 

 “Sasa kwa vile watu tayari walikuwa wameshaingia kufanya kazi chini, lilipodondoka likawafunika wakiwa na gari aina ya Isuzu iliyokuwa ikipakia moramu,” alisema Joel.

 Kwa upande wake mpakiaji wa moramu kwenye mgodi huo Apolinary Amandus alisema hali hiyo huwa inajitokeza pindi kuta za mlima huo zinapopoteza uimara.

Akizungumzia kuhusu tahadhari wanazochukua pindi kunapokuwa na mvua au hali ya hatari kwenye eneo hilo, dereva wa magari yanayobeba moramu, Geofrey John, alisema huwa wanapewa tahadhari ya kutokukaribia kwa muda.

 “Moramu hii inaendesha maisha ya watu, hapa mgodini  tunanunua lori moja kwa Sh 60,000 pamoja na ushuru wake na sisi tunaenda kuuza kati ya Sh 100,000 hadi 110,000,” alisema John.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles