26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Utata ripoti ya IMF

  • Mbunge ahoji Serikali kuzuia kuchapishwa, Ndugai amshangaa
  • Serikali yatoa ufafanuzi, yasema maoni yake hayakuzingatiwa

MAREGESI PAUL-DODOMA

SERIKALI imesema haijalizuia Shirika la Fedha Duniani (IMF) lisichapishe ripoti ya hali ya uchumi wa Tanzania.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa kauli iliyotolewa na Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), wakati alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Katika maelezo yake, Dk. Mpango alisema ripoti hiyo ya IMF haijachapishwa kwa kuwa Serikali ya Tanzania bado iko kwenye mazungumzo na shirika hilo kwa kuwa baadhi ya mambo hayajakaa sawa.

“Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kwenye mjadala huu kwa sababu katika majadiliano ambayo yanaitwa ‘article four consultations’, timu ya IMF ilikuwa hapa nchini kuanzia Novemba 26 mpaka Desemba 7, mwaka jana.

 “Baada ya hapo walitoa taarifa na kwa utaratibu ni kwamba wakitoa ile rasimu ya taarifa, inarudi serikalini ili tuweze kuitolea maoni na wao waweze kuyazingatia kabla ya kuichapisha hiyo ripoti.

“Kwa bahati mbaya, hiyo ripoti nilikuja kuiona tarehe 18 Machi, mwaka huu na baada ya kuwa sisi tumemaliza maoni yetu, maoni yetu hayajazingatiwa kwenye hiyo taarifa yao.

 “Hata nilipokuwa Washington (Marekani), juzi nilizungumza na bwana mmoja anaitwa Abebe Selassie ambaye ni Mkurugenzi wa African Department na hata leo (jana) saa tisa mchana tutaendeleza majadiliano kuhusu jambo hili.

“Kwa utaratibu ulivyo, ni kwamba baada ya executive board ya IMF kuijadili hiyo taarifa, Serikali inakuwa na siku 14 za kuipitia na kusema itolewe au isitolewe.

“Kwa hiyo, mheshimiwa Spika, wasiwahishe mjadala, Serikali bado inazungumza na IMF na hakuna sehemu ambapo tumezuia, ni utaratibu wa IMF yenyewe,” alisema Dk. Mpango.

 Awali, Dk. Mpango alitanguliwa na Mnadhimu Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni, Jenister Mhagama, ambaye alimwomba Mwakajoka afute kauli yake ya kusema Serikali imeizuia IMF isichapishe ripoti ya hali ya uchumi wa Tanzania.

“Mheshimiwa Spika, natumia kanuni ya 64 (i) A, ambayo inasema kwamba mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli.

“Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali tunavyojua sisi, bado tunaendelea kufanya mazungumzo na IMF kuhusu ripoti hiyo na si kweli kwamba Tanzania imezuia ripoti hiyo isitolewe.

“Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mimi ninafahamu, na waziri wa fedha yuko hapa na anafahamu na ana maelezo ya kutosha kuhusu jambo hilo ambalo linapotoshwa na mheshimiwa Mwakajoka, ninamuomba mheshimiwa Mwakajoka afute hizo ‘statement’ zake za kuituhumu Serikali, kwamba imeficha hiyo ripoti na haitaki itolewe.

“Kama hawezi kuifuta kauli yake, basi naomba alithibitishie Bunge kwamba taarifa anazozisema ni sahihi na ripoti aliyonayo ni sahihi na hakuna jambo lolote linaloendelea kwa sasa ndani ya Serikali,” alisema Mhagama.

KAULI YA MWAKAJOKA

Awali, Mwakajoka aliishutumu Serikali kwa kuvibana vyombo vya habari nchini na kuvifanya vishindwe kuripoti ukweli wa matukio mbalimbali.

“Mheshimiwa Spika, juzi tumepata taarifa kwenye mitandao na vyombo vingine vya habari, kwamba IMF wanaomba waruhusiwe na Serikali ya Tanzania watoe habari ya jinsi gani uchumi wa nchi yetu unakwenda.

“Jambo la kushangaza ni kwamba mpaka sasa hivi kuna ukimya juu ya taarifa hizo kwa sababu hata vyombo vya habari vinaogopa kuripoti taarifa hizo,” alisema Mwakajoka.

Hata hivyo, wakati Mwakajoka akichangia hoja hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimshangaa na kuhoji kama kweli anachokisema ni sahihi na mahojiano yao yalikuwa hivi.

Spika: Mheshimiwa Mwakajoka, una uhakika IMF imeomba itoe taarifa hiyo?

Mwakajoka: Ndiyo Mheshimiwa Spika, wameiomba Serikali ya Tanzania iruhusu ili wachapishe hali ya uchumi wa nchi yetu kwa jinsi ambavyo wameangalia, lakini wamezuiliwa wasiitoe.

Spika: Hivi Tanzania inaweza kuizuia IMF wasichapishe taarifa yao?

Mwakajoka: Ndiyo, kwa mujibu wa sheria ni lazima nchi ihusike na Tanzania haijaruhusu ili wachapishe ile taarifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,663FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles