Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
SHAHIDI wa kwanza upande wa mashtaka katika kesi ya kutoa maneno ya uchochezi kwa kumwita Rais “dikteta uchwara”, inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amedai maneno hayo yalikuwa ya kuwashawishi Watanzania wapingane na utawala uliopo madarakani.
Shahidi huyo, E 4128 Ndege, alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa.
“Nilimsikia mshtakiwa akisema ‘mamlaka ya Serikali mbovu ya dikteta uchwara yanapaswa kupingwa na Watanzania ukiachwa unaweza kuliingiza taifa gizani’.
“Mimi na Kikweri tulikuwepo, tulitafsiri maneno hayo na kuyatolea taarifa, niliandika maelezo yangu mwenyewe nikakabidhi kwa Kimweri ambaye ni bosi wangu,” alidai Ndege.
Shahidi huyo alikuwa akiongozwa na Wakili wa Serikali, Mohammed Salum, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala.
Baada ya Hakimu Mwambapa kusikiliza ushahidi wa shahidi huyo wa kwanza, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, mwakani.
Juni 30 mwaka huu, Lissu alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kufunguliwa kesi ya uchochezi Na. 233/2016. Alisomewa shtaka la kutoa maneno ya uchochezi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 28, mwaka huu, kwa kumuita Rais wa nchi ni “dikteta uchwara” kinyume cha kifungu Na. 32 cha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.