ISIJI DOMINIC
KWA mara ya kwanza, aliyekuwa moja wa viongozi waandamizi wa Chama cha Jubilee alitoa kauli ambayo inaweza ikafichua mazungumzo yaliyosababisha kuundwa kwa chama hicho na hususan ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.
Viongozi hawa wawili ambao walikuwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) huko Hague, Uholanzi kufuatia machafuko ya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, waliunganisha vyama vyao (TNA ya Uhuru na URP ya Ruto) wakafanya kampeni nchi nzima. Walifanikiwa kushinda katika uchaguzi mkuu 2013 chini ya Katiba mpya.
Rais Uhuru mara kadhaa aliwahi kunukuliwa akisema baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi itakuwa zamu ya Ruto lakini baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Rais Uhuru amekuwa kimya kuhusu Ruto kumrithi badala yake akisisitiza anataka kutimiza ahadi zake na muda ukifika atawashangaza wengi.
Ukaribu wa Rais Uhuru na mpinzani wake kisiasa ambaye pia ni moja wa vinara wa muungano wa NASA, Raila Odinga, kufuatia lile tukio la Machi 9 mwaka jana umetafsiriwa kuzua hofu kwa kambi ya Ruto ambao wanahisi huenda Uhuru akamtosa katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Wao wamekuwa wakisisitiza makubaliano yalikuwa Rais Uhuru akimaliza muda wake atamuunga mkono naibu wake. Hata hivyo, David Murathe, wakati bado akiwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee na akiwa ziarani Maghabiri mwa Kenya alisema Ruto anapaswa kustaafu siasa pamoja na Uhuru mwaka 2022.
Kauli hiyo ya Murathe ambaye ni mbunge wa zamani na mtu ambaye yupo karibu sana na Rais Uhuru imeelezwa kuwa huenda ikawa pia ni maoni ya Rais au ni kauli yenye nia ya kutaka viongozi hususan ndani ya Jubilee kuwacha kufikiria siasa za 2022 na badala yake kuwatumikia wananchi.
Rais Uhuru alipoulizwa na waandishi wa habari aliyowaalika Ikulu jijini Mombasa katika mkesha wa Mwaka Mpya kuhusu kauli ya Murathe, alikataa kuhusishwa na matamshi ya mwanasiasa huyo akisisitiza hayupo tayari kuongea siasa za 2022.
Lakini ndani ya Chama cha Jubilee hususan wanaomuunga mkono Naibu Rais, wamemjia juu Murathe huku wakimtaka Rais Uhuru amtimue ndani ya chama. Hata hivyo bila kusubiri atimuliwe, Murathe aliwasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa wake wa Makamu Mwenyekiti. Mbunge wa Kipkelion Magharibi, Hillary Koskei, na mwenzake wa Belgut, Nelson Koech, wamemshutumu Murathe kwa kujaribu kuvuruga chama.
“Hivi Murathe ni nani kumwambia Ruto astaafu siasa 2022. Imefika wakati sasa tunalazimika kumuuliza Rais Uhuru atuambie kwanini Murathe bado yupo Jubilee. Kwanini bado anaruhusiwa kuzunguka akijaribu kuvuruga chama kwa kutoa matamshi yasiyokuwa na maana?” alisema Koskei.
Naye Koech alisema Murathe hajapewa kibali kuongea masuala ya ndani ya Jubilee kwasababu achaguliwe kukaimu nafasi aliyonayo na muda wake kukaa ofisini ulimalizika tangu Desemba 2017.
Japo Naibu Rais amekwepa kuzungumzia kauli ya Murathe, alisema atamuunga mkono yeyote atakayemshinda 2022 wakati Jubilee itakapofanya uchaguzi wa ndani kumchagua mgombea urais. Alisema chama hicho kiliundwa kwa misingi ya kidemokrasia hivyo kila mgombea wa nafasi mbalimbali lazima akubali matokeo muda ukishafika.