WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewasimamisha kazi vigogo wawili wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), kwa uzembe katika utendaji kazi ikiwamo kuteua watu wasiokuwa na sifa ‘vilaza’ kwenda kwenye mafunzo ya urubani Canada.
Waliosimamishwa kazi ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, i Jonathan Mfinanga na Kapteni Sadicki Muze. Wote wanatuhumiwa kuteua watu wasio na sifa kwenda Canada kwa mafunzo ya urubani wa ndege.
Akitoa agizo la kusimamishwa kazi kwa watendaji hao jana, Profesa Makame alisema Serikali ipo katika mchakato wa kununua ndege mbili.
Hivyo kabla ya kuwasili ndege hizo ni vema baadhi ya wataalamu wakapelekwa Canada kupata mafunzo, alisema.
Alisema Serikali imekwisha kulipia Dola za Marekani bilioni 40 na kwamba ifikapo September 14, mwaka huu ndege hizo zitakuwa zimewasilia nchini.
Waziri alisema kwa sababu hiyo, ni vema ATCL ikaandaa marubaini wake kwa ajili ya kurusha ndege hizo.
“Marubani wanaotakiwa ni wanne lakini awali nililetewa majina ya marubani tisa ambao baadhi yao waliondolewa kutokana na kukosa sifa.
“Lakini orodha ya majina iliyobaki ililetwa kwangu kwa ajili ya kuipitia na niliwauliza wahusika kwamba mna uhakika na hawa watu? Wakaniambia ndiyo tuna uhakika nao.
“…niliwauliza kwa mara ya pili mna uhakika na haya majina mlioniletea wao wakaniambia ndiyo mkuu.
“Sasa leo (jana) asubuhi naletewa taarifa kwamba kuna tatizo limejitokeza kwa wale watu watano wanaotakiwa kuondoka kesho (leo) kwenda Canada kwa ajili ya mafunzo ya ndege yanayoanza Agosti 8, mwaka huu,” alisema.
Alisema licha ya kutoa agizo la kuteuliwa watu wenye uwezo, bado watendaji hao wamefanya uzembe na kuteua watu ambao hawana sifa za urubani ‘vilaza’.
“Wamechagua marubani lakini kidogo mchakato haukwenda vizuri, kwa kuwa na mimi nilitoa maelekezo nikasema hapana hivi sasa kwenye shirika la ndege ama mashirika yote watu lazima wawe na nidhamu wakifanya kitu lazima kiwe na uhakika.
“Nimeletewa ripoti ile asubuhi kwamba kuna tatizo limejitokeza nikawaambia kila aliyesababisha tatizo hilo awajibike,” alisema.
Alisema katika marubani watano ambao serikali ilikuwa ikiwapeleka nje kujifunza mmoja ‘kilaza’ amekutwa na kasoro ambazo hazikidhi vigezo vya urubani.
“ Leo (jana) nimepigiwa simu na mtu, halafu nikajihakikishia upande mwingine nikaambiwa kuna tatizo na kwamba hatuwezi kulitatua kwa vile wale marubani wanatakiwa kusafiri kesho (leo).
“Hivyo tukianza mambo mengine itatuchelewesha na kozi inaanza Agosti 8. Sasa nikawaambia wale waliohusika na uzembe hata kama ni kidogo hatuwezi kukubali ni lazima wasimamishwe kazi mara moja,”alisema.
Alisema mtu wa kwanza ni Jonathan Mfinanga, ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa ATCL na Kapteni Sadick Muze ambaye ni Mkurugenzi wa Operesheni na Uendeshaji.
“Watu hawa wawili ni lazima wachukue dhamana, hatuwezi kuendelea na mtu anafanya jambo la kizembezembe halafu akaachwa wakati niliwaita mara mbilimbili na nikatoa maelekezo lakini bado wamefanya wanavyojua wao,”alisema.
Waziri alisema amekwisha kutoa maelekezo atafutwe mtu mwingine atakayekaimu nafasi hizo na Serilikali inaendelea na utatuzi wa suala lililojitokeza huku marubani waliotakiwa wakitarajiwa kuondoka leo.
Wakati huohuo, Waziri Mbarawa ameliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), zianze kubomoa nyumba zote zilizojengwa kwenye hifadhi ya reli na barabara kuu zote nchini kuilinda miundombinu hiyo isiharibiwe.
Profesa Mbarawa alikuwa akikagua daraja la Reli ya Tazara lililopo Mbalizi, nje kidogo ya mji wa Mbeya.
“Sheria iko wazi, lazima muisimamie msisubiri waziri aseme. Mwananchi yeyote aliyeifuata miundombinu ya reli, lazima mumvunjie nyumba yake ili miundombinu iliyojengwa kwa kutumia fedha nyingi, iweze kudumu.
“Lazima hilo lifanyike kwa sababu Serikali ipo katika hatua za kuboresha miundombinu ya reli ya kati na reli ya Tazara kuhakikisha mizigo yote ya ndani na nje ya nchi inayopitia kwenye Bandari ya Dar es Salaam, inafirishw kwa njia ya reli.
“Mizigo inayopita katika reli ni asilimia nne tu kutoka bandarini, hivyo lazima tujipange kuanza kutafuta masoko na kuchukua mizigo hiyo kulinda miundombinu ya barabara inayoharibiwa na uzito mkubwa wa magari,” alisema.