24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa nzito Shirika la Ndege Tanzania

makameNa Pendo Fundisha, Mbeya

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewasimamisha kazi vigogo wawili wa  Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL),  kwa   uzembe katika utendaji kazi  ikiwamo kuteua watu wasiokuwa na sifa ‘vilaza’  kwenda kwenye mafunzo ya urubani   Canada.

Waliosimamishwa kazi ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa ATCL,  i Jonathan Mfinanga na  Kapteni Sadicki Muze. Wote wanatuhumiwa kuteua watu wasio na sifa   kwenda   Canada kwa mafunzo ya urubani wa ndege.

Akitoa agizo la kusimamishwa kazi kwa watendaji hao jana,   Profesa Makame alisema Serikali ipo katika mchakato wa kununua ndege mbili.

Hivyo kabla ya kuwasili  ndege hizo ni vema baadhi ya wataalamu wakapelekwa   Canada   kupata mafunzo, alisema.

Alisema  Serikali imekwisha kulipia Dola za Marekani bilioni 40 na kwamba ifikapo September 14, mwaka huu  ndege hizo zitakuwa zimewasilia nchini.

Waziri alisema kwa sababu hiyo,  ni vema   ATCL ikaandaa marubaini wake kwa ajili ya kurusha ndege hizo.

“Marubani wanaotakiwa ni wanne lakini    awali nililetewa majina ya marubani tisa ambao baadhi yao waliondolewa kutokana na kukosa sifa.

“Lakini orodha ya majina iliyobaki ililetwa kwangu kwa ajili ya kuipitia na niliwauliza wahusika kwamba mna uhakika na hawa watu?  Wakaniambia ndiyo tuna uhakika nao.

“…niliwauliza  kwa mara ya pili mna uhakika na haya majina mlioniletea wao wakaniambia ndiyo mkuu.

“Sasa leo (jana) asubuhi naletewa taarifa kwamba kuna tatizo limejitokeza kwa wale watu watano wanaotakiwa kuondoka kesho (leo) kwenda   Canada kwa ajili ya mafunzo ya ndege yanayoanza Agosti 8, mwaka huu,” alisema.

Alisema licha ya kutoa agizo la kuteuliwa watu wenye uwezo,  bado watendaji hao wamefanya uzembe na kuteua watu ambao hawana sifa za urubani ‘vilaza’.

“Wamechagua marubani lakini kidogo mchakato haukwenda vizuri, kwa kuwa na mimi nilitoa maelekezo nikasema hapana   hivi sasa  kwenye shirika la ndege ama mashirika yote watu lazima wawe na nidhamu wakifanya kitu lazima kiwe na uhakika.

“Nimeletewa ripoti ile asubuhi kwamba kuna tatizo limejitokeza nikawaambia kila aliyesababisha tatizo hilo awajibike,” alisema.

Alisema  katika marubani watano ambao serikali ilikuwa ikiwapeleka nje kujifunza mmoja ‘kilaza’ amekutwa na kasoro ambazo hazikidhi vigezo vya urubani.

“ Leo (jana) nimepigiwa simu na mtu, halafu nikajihakikishia upande mwingine nikaambiwa kuna tatizo na kwamba hatuwezi kulitatua kwa vile  wale marubani wanatakiwa kusafiri kesho (leo).

“Hivyo tukianza mambo mengine itatuchelewesha na kozi inaanza Agosti 8. Sasa nikawaambia wale  waliohusika na uzembe hata kama ni kidogo hatuwezi kukubali  ni lazima wasimamishwe kazi mara moja,”alisema.

Alisema mtu  wa  kwanza ni   Jonathan Mfinanga,  ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa ATCL   na Kapteni Sadick Muze  ambaye ni Mkurugenzi wa Operesheni na Uendeshaji.

“Watu hawa wawili ni lazima wachukue dhamana, hatuwezi  kuendelea na mtu anafanya jambo la kizembezembe halafu akaachwa wakati niliwaita mara mbilimbili na nikatoa  maelekezo  lakini bado wamefanya wanavyojua wao,”alisema.

Waziri   alisema amekwisha kutoa  maelekezo   atafutwe mtu mwingine atakayekaimu nafasi hizo na  Serilikali inaendelea na utatuzi wa suala   lililojitokeza huku marubani waliotakiwa wakitarajiwa kuondoka leo.

Wakati huohuo, Waziri  Mbarawa  ameliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), zianze kubomoa nyumba zote zilizojengwa kwenye hifadhi  ya reli na barabara kuu zote nchini  kuilinda miundombinu hiyo isiharibiwe.

Profesa Mbarawa alikuwa akikagua daraja la Reli ya Tazara lililopo Mbalizi, nje kidogo ya mji wa Mbeya.

“Sheria iko wazi, lazima muisimamie msisubiri waziri aseme. Mwananchi yeyote aliyeifuata miundombinu ya reli, lazima mumvunjie nyumba yake ili miundombinu iliyojengwa kwa kutumia fedha nyingi, iweze kudumu.

“Lazima hilo lifanyike kwa sababu Serikali ipo katika hatua za kuboresha miundombinu ya reli ya kati na reli ya Tazara   kuhakikisha mizigo yote ya ndani na nje ya nchi inayopitia kwenye Bandari ya Dar es Salaam, inafirishw kwa njia ya reli.

“Mizigo inayopita katika reli ni asilimia nne tu kutoka bandarini, hivyo lazima tujipange kuanza kutafuta masoko na kuchukua mizigo hiyo   kulinda miundombinu ya barabara inayoharibiwa na uzito mkubwa wa magari,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles