24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Aina tano za vyakula hatari

vyakulaVeronica Romwald na Hamidu Abdallah (DSJ), Dar es Salaam

AFYA za wananchi mbalimbali zipo hatarini, kutokana na ulaji wa vyakula mbalimbali ambavyo ni hatari kiafya. MTANZANIA linaripoti.

Wataalamu wa chakula na lishe wameainisha aina tano za vyakula ambavyo ni hatari katika mwili wa mwanadamu, vikitajwa kusababisha maradhi mbalimbali.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, walaji wa nyama ya nundu ya ng’ombe, ngozi ya kuku, clips na bisi wapo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza, ikiwamo shinikizo la damu na ugonjwa wa moyo.

Taarifa hiyo inakuja siku mbili, baada ya Mtaalamu wa Lishe wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ulumbi Kilimba, kulieleza gazeti hili kuhusu athari za ulaji wa chipsi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Lishe wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Julieth Shine, alisema si chipsi pekee ambazo ni hatari, bali vyakula vyote ambavyo hukaangwa kwa kutumbukizwa kwenye mafuta ni hatari kiafya.

“TFNC hatujawahi kufanya utafiti kujua kiwango halisi cha mafuta kilichomo katika chipsi, lakini mara zote huwa tunashauri watu waepuke ulaji wa vyakula vilivyopikwa kwa kutumbukizwa kwenye mafuta, kwani si salama kwa afya,” alisema.

Alisema hiyo ni kwa sababu vyakula hivyo hunyonya kiwango kikubwa cha mafuta pindi vinapokaangwa jikoni.

“Mwili ukipokea kiwango kingi cha mafuta (lehemu) matokeo yake ni kwamba huenda kujihifadhi kwenye mishipa ya damu hatimaye mtu hujikuta akiwa amepata shinikizo la damu na magonjwa ya moyo,” alisema.

Alisema mafuta ambayo huwa na hatari kubwa zaidi ni yale yanayotokana na wanyama.

“Katika jamii zetu wapo watu ambao hupendelea kula nyama ya nundu inayopatikana kwenye nyama ya ng’ombe pamoja na ule utando wa mafuta unaotokea katika maziwa fresh yaliyochemshwa, watu hawa wanajiweka kwenye hatari kwani nyama na utando vina kiwango kingi cha lehemu,” alisema.

Alisema ngozi ya kuku nayo ina lehemu nyingi na kwamba inapaswa kuondolewa kabla ya kuchemsha kitoweo hicho na kukiandaa kwa ajili ya kula.

“Tunashauri kuku achunwe ngozi kabla ya kuchemshwa na kuungwa kwa ajili ya mlo, lakini pia watu waepuke kula nyama iliyonona ni vema wale samaki na mbogamboga kwa wingi,” alisema.

Mtaalamu huyo pia alisema watu wanapaswa kupunguza ulaji wa clipsi na bisi, kwani vyakula hivyo hutengenezwa kwa chumvi nyingi ambayo baadaye huleta madhara mwilini.

“Bisi na clipsi hutengenezwa na kuwekewa chumvi nyingi, baadhi ya watu hupendelea kuongeza chumvi kwenye vyakula nao wanajiweka kwenye hatari ya kupata shinikizo la damu.

“Wapo wengine pia hupenda matumizi ya sukari nyingi matokeo yake uzito wa mwili unaongezeka, kinywa kinajaa bakteria na meno kuoza,” alisema.

Alishauri watu waepuke kunywa vinywaji vilivyotengenezwa kwa  sukari nyingi badala yake ni vema wanywe juisi za matunda ambazo hazijaongezwa sukari ya aina yoyote au maji ya madafu kwani ni salama zaidi kwa afya.

“Wafanye mazoezi, kila siku wajitahidi kula vyakula vinavyotokana na makundi haya… vile vyenye asili ya nafaka, ndizi za kupika na vya asili ya mizizi kama vile mihogo na viazi, mbogamboga, matunda, asali, sukari na mafuta (kwa kiasi)na vyakula vya jamii ya kunde.

Mtaalamu huyo wa lishe, alishauri ulaji wa vyakula vyenye nyuzi nyuzi kwani husaidia katika uyeyushwaji wa chakula tumboni na huweza kupunguza baadhi ya saratani, magonjwa ya moyo na kisukari.

“Wapendelee kula saladi na matunda mara kwa mara, wale matunda badala ya juisi tena na maganda yake pale inapowezekana, wale ugali dona na vile vya jamii ya kunde kwani vina nyuzi nyuzi kwa wingi pamoja na maji ya kutosha,” alisema.

Siku mbili zilizopita Mtaalamu wa Masuala ya Chakula na Lishe wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ulumbi Kilimba, alisema walaji wengi wa chipsi wapo katika hatari ya kutengeneza sumu kwenye miili yao bila kujua.

Alisema ulaji wa Chispi ni hatari kwa afya ya binadamu, kwani husababisha maradhi mengi yasiyo ya kuambukiza hasa figo, moyo, shinikizo la damu, kisukari na saratani za aina zote.

Alisema sahani moja ya chipsi kavu huwa na mafuta yanayokaribia nusu kikombe cha chai ambayo ni sawa na ujazo wa mililita 250.

Mwisho

 

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Nataka kujua kula samaki kupita kiasi je kuna madhara yoyote yatakayo mpata binadamu (mtumiaji)!?? na je kama madhara yapo yanasababishwa na samaki gani?? Kambale,. Perege,. Ningu,. Sato,. Sangara,.au dagaa??

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles